Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yatoa msimamo matukio ya utekaji

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanul Nchimbi.

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa msimamo wake kuhusu matukio ya utekaji, kikitaka uchunguzi akisema chama hicho hakiwezi kukubali genge hilo likiumize chama hicho.

Dar es Salaam. Wakati Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanul Nchimbi akieleza jinsi chama hicho kinavyoguswa na matukio ya utekaji na mauaji nchini yanayoendelea nchini, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amekitaka chama hicho kuchukua hatua kwa vitendo hivyo.

Mbali na kueleza kuguswa na matukio hayo, Dk Nchimbi pia amesisitiza kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na kitaalamu kuwabaini wanaohusika.

CCM inakuja na kauli hiyo, ikiwa ni siku tano tangu kutokea kwa mauaji ya kada wa Chadema, Ali Mohamed Kibao yaliyotokea siku moja baada ya kukamatwa na kutekwa na wasiojulikana.

Kibao alikamatwa Septemba 6, 2024 Kibo Complex Tegeta, Dar es Salaam, akiwa kwenye basi la Tashriff akienda nyumbani kwao mkoani Tanga.

Mbali na kada huyo, kumeripotiwa matukio kadhaa ya kupotea, kutoweka na kutekwa kwa watu zaidi ya 80 ambao hadi sasa hawajulikani walipo.

Akizungumza na waandishi waandamizi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 13, 2024, Dk Nchimbi amesema chama hicho kinaunga mkono kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka uchunguzi wa haraka ili watuhumiwa wapatikane na hatua zichukuliwe.

“CCM imekasirishwa sana na jambo hili (mauaji ya Kibao), nilipata taarifa ya ule msiba, Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema) kanipigia simu karibu mara tano. Ujasiri wa kupokea ile simu sikuupata.

“Baadaye nilimwandikia ujumbe kwamba bwana naomba radhi jambo lile lilinivuruga nikashindwa kupokea simu,” amesema.

Kuhusu uchunguzi huo, amesema unapaswa kuwa wa kitaalamu ili wanaobainika wawe ndiyo wahusika halisi, isitokee yeyote kusingiziwa.

“Yale mambo ya unamkamata mtu unamfunga au kumnyonga baada ya miaka 20 unakuja kusema hakuwa mtuhumiwa mnakwenda kuweka maua kaburini kwake ni ujinga,” amesema.

Katika utekelezaji wa uchunguzi huo, amesema CCM itakuwa tayari kupokea mamlaka yoyote ya uchunguzi iwapo Serikali itaona vyombo vyake vimepungukiwa nguvu kulitekeleza hilo.

Amesema kiu ya chama hicho ni kuona wahusika wanabainika na wanachukuliwa hatua kwa njia na mbinu yoyote.

 “Kuhusu anayepaswa kuchunguza ni mamlaka ya Serikali, ikiona inapungukiwa nguvu na kuomba wachunguzi kutoka nje, CCM inaunga mkono.

“Tunachotaka ni wahusika wapatikane, njia yoyote itakayotumika kuwapata ni sawa ilimradi wapatikane,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, wananchi wanapaswa kutoa muda wa uchunguzi ili hatua zichukuliwe, badala ya kushinikiza uharakishwe.

Hata hivyo, amesema yeyote anayefanya vitendo vya utekaji na mauaji, anajaribu kuichafua taswira ya CCM mbele ya umma.

Amesema kama ni genge linalojihusisha na utekaji wa watu linaiumiza CCM. Jambo la utekaji na mauaji madhara yake kwa umma ni kukataliwa ni chama cha kipumbavu pekee ndicho kitakubali matendo yanayoondoa imani yake kwa umma,” amesema.

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amesema kinachofanyika na watekaji hao ni kuvifarakanisha vyama vya siasa.

Amesema na huo ndio mtego ambao Chadema inaonyesha dalili za kuuingia kwa kuweka ukomo wa muda wa uchunguzi dhidi ya matukio hayo.

“Tunavitaka vyama vya upinzani vikatae kufarakanishwa, ndiyo maana sisi CCM tumefanya kila jitihada kukataa mijadala isiyofaa,” amesema.

Hatua ya vyama vya siasa kufarakana, amesema kunawapa ushindi watekaji, akisisitiza umuhimu wa kuungana kukabiliana na genge hilo.

Amesema watu wamekwenda mbali zaidi hadi kufikia hatua ya kulifarakanisha Jeshi la Polisi na raia na kwamba hilo ni moja ya mambo mabaya kwa Taifa.

“Haiwezekani wakitokea polisi wawili, watatu wana tabia mbaya basi wahusishwe watu wote. Polisi ndiyo watu wanaotoa maisha yao kupitiliza,” alisema.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2023 askari polisi 42 wameuawa wakiwa katika mapambano na majambazi, huku 141 wamejeruhiwa katika kipindi hicho.

Kuhusu matukio ya utekaji yaliyoripotiwa Polisi, amesema katika miaka mitano watu 151 wamepotea na waliopatikana ni 141.


Chadema wajibu

Alipoulizwa kuhusu kauli hizo za CCM, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amesema CCM ndiyo inayoongoza Serikali ya nchi na mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, hivyo ana mamlaka ya kudhibiti hali hiyo.

Lissu amedai kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinatuhumiwa na matukio hayo, na kuwa CCM imeshindwa kuwawajibisha viongozi wa vyombo hivyo.

 “Kwa sababu zote hizi, maneno matupu hayavunji mfupa. Kauli ya Dk Nchimbi ni maneno matupu; hayatoshi na hayakubaliki.

“Tunataka kuona vitendo vya kweli na dhati, viongozi na watendaji wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wawajibike kwa kuondolewa madarakani,” amesema Lissu.

Ameitaka Serikali hii ya CCM iruhusu uchunguzi wa kimataifa wa matukio yote ya utekaji nyara na mauaji ya raia.

“Kama ilivyoruhusu FBI (Shirika la Uchunguzi wa Kijinai la Marekani) kuchunguza vitendo vya kigaidi dhidi ya viongozi wa dini Zanzibar zaidi ya miaka 10 iliyopita; na kama ilivyoruhusu Scotland Yard kuchunguza kuchomwa moto kwa Jengo la Benki Kuu ya Tanzania takriban miaka 40 iliyopita,” amesema. 

Ameitaka pia CCM na Serikali yake iruhusu marekebisho makubwa ya muundo, majukumu na uendeshaji wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kujenga weledi, nidhamu na uwajibikaji.

“(CCM) iruhusu mchakato wa Katiba Mpya uendelee ili nchi yetu ipate Katiba Mpya itakayolinda haki za wananchi, kuimarisha uwajibikaji na kujenga misingi imara zaidi ya demokrasia. Hatutaki maneno matupu,” amesema.