CCM yawaita walioomba ubunge EALA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka

Muktasari:

Jumla ya wanachama 155 wa chama hicho wameshachukua fomu za kuomba kuwania nafasi hizo, baada ya dirisha la uchukuaji fomu hizo kufunguliwa Agosti Mosi, 2022 na kufungwa Agosti 10 mwaka huu.

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi kimewaita wanachama wake wote waliomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Bunge la Afrika Mashariki kufika kwenye kikao cha sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Jumla ya wanachama 155 wa chama hicho wameshachukua fomu za kuomba kuwania nafasi hizo, baada ya dirisha la uchukuaji fomu hizo kufunguliwa Agosti Mosi, 2022 na kufungwa rasmi Agost 10 Mwaka huu.

Taarifa ilitolewa leo Septemba 2 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka imewataka wateule hao kwenda na nyaraka zao zote muhimu zinazohusu sifa za kuwania nafasi hizo.

Shaka amesema pamoja na mambo mengine wagombea hao wameitwa kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki na uratibu wa vikao husika vya chama hicho.

Kwa upande wa Tanzania Bara, “Kikao hicho kitafanyika Jijini Dodoma Septemba 4 hadi 5 mwaka huu, kuanzia saa 3 subuhi Hivyo kila mwombaji anatakiwa kufika Dodoma Septemba 03 mwaka huu ili kuitika wito huo,”amesema

Aidha, kwa wagombea wa upande wa Zanzibar, nyaraka zao zitakuwa zinahakikiwa na kuratibiwa na kikao cha kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho  Zanzibar kama ilivyoelekezwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.

Hivyo kwa wateuliwa hao kutoka Zanzibar hawatalazimika kwenda Dodoma.