Chadema, ACT Wazalendo walaani Polisi kuua watuhumiwa

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Benson Kigaila akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam

Muktasari:

Vyama vya Chadema na ACT Wazalendo vimelaumu mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi kwa watu watatu waliodaiwa kuwa ni majambazi wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, vikitaka Serikali ifanye uchunguzi kubaini ukweli.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepia siku nne tangu Jeshi la Polisi mkoani Mara lilipowaua watu watatu kwa madai ya kufanya ujambazi na kukutwa na bunduki, vyama vya Chadema na ACT Wazalendo vimelaani hatua hiyo na kutaka uchunguzi ufanyike kwa mauaji hayo.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 22, ambapo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishiwanu alidai kuwa watu hao walifanya vitendo vya ujambazi.

Waliouawa katika tukio hilo ni Mauro Togoro, Mwise Simon, Mgale Mikori Mgale, huku James Mwita alikamatwa na baadaye kutorokea kusikojulikana.

Kati ya waliouawa yumo Mgale Mikori ambaye ni mjomba wa Katibu wa Baraza la Wanawake la Chadema, Catherine Ruge, aliyekamatwa nyumbani kwake.

Akizungumzia tukio hilo leo Septemba 27 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila amesema ukataji uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa watuhumiwa hao haukufuata misingi ya haki za binadamu.

“Maelezo ya polisi ni kwamba majambazi hao wanne walichukuliwa usiku wa saa nane kwa ajili ya kuonyesha walipo wenzao na walikoficha silaha, kwanini isiwe mchana?” alihoji.

Alisema taarifa ya kuuliwa kwao zinatia shaka kwani iliwezekanaje majambazi waliokuwa na polisi wakimbie na kuhoji kama hawakuwa na pingu.

“Ilikuwaje kama kweli walikuwa majambazi na wanakwenda kuonyesha walipo wenzao kwanini hawakuwafunga pingu mpaka wakaanza kukimbia wanatoroka,” alisema.

Amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua ya kuunda tume ya majaji kuchunguza tukio hilo, akisisitiza kuwa wanakijiji wapo tayari kutoa ushahidi iwapo hilo litafanyika.

Kadhalika, amemtaka kuchukua hatua ya kuwafuta kazi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Massauni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura na makamanda wengine katika Mkoa wa Mara na Wilaya ya Serengeti.

“Polisi ambao badala ya kwenda kulinda raia wanakwenda kuuwa watu maana yake wanajenga uhalifu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Chama cha ACT Wazalendo kimelaani ukamataji usiofuata haki za binadamu na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho, imefafanua kuwa Septemba 18, mwaka huu watu sita waliuawa na jeshi hilo jijini Dar es Salaam, kadhalika hilo limefanyika Septemba 21, ambapo watatu waliuawa.


“Ni wazi kuwa bado operesheni za Jeshi la Polisi zimejengeka kwenye mtazamo katili na sura ya kikaburu. Polisi wanavyokuja kukukamata, tayari wameshakuhukumu.

“Ikiwa Polisi wanajipa haki za kukamata, kuhukumu na kutoa adhabu tena adhabu za kifo kwa watuhumiwa ni dhahiri kuna ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu,” amesema.

Chama hicho kimependekeza kuundwa tume ya kuchunguza mauaji hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani aongeze usimamizi wa oparesheni za jeshi hilo, hatua zichukuliwe kwa wanaohusika na mageuzi ya utendaji wa chombo hicho kutoka kutumia nguvu hadi utaalamu, sayansi na weledi.