Chadema: Muswada wa vyama vya siasa uondolewe bungeni

Muktasari:

  • Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Chadema, kimezungumzia muswada wa vyama vya siasa kikisema haupaswi kupitishwa kwani utakwenda kukandamiza demokrasia nchini.

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Chadema Kanda ya Pwani limeitaka Serikali kuuondoa bungeni muswada wa vyama vya siasa kwa kuwa unalenga kuua demokrasia nchini Tanzania.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 24, 2018 na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kanda hiyo, Frederick Sumaye amesema muswada huo ni mwiba kwa demokrasia na ukipitishwa utafuta suala la demokrasia Tanzania.

“Kama Serikali yetu ni sikivu iuondoe huu muswada kwa sababu inaua demokrasia ya vyama vingi ambayo imeainishwa kwenye katiba,” amesema Sumaye ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu

Amesema endapo wabunge wa CCM watapitisha muswada huo watakuwa wamepigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la demokrasia.

“Tunawaomba wabunge wote kwa pamoja wapinge muswada huu, moto si wa wapinzani peke yao hata wao utawaunguza,” amesema.

“Nawatahadharisha wabunge wa CCM kama muswada huu utapita ni kweli demokrasia itakufa na hata ndani ya CCM mtu mmoja ndiye atakuwa na mamlaka ya kuamua nani awe mbunge au Rais,” ameongeza.

Waziri mkuu huyo wa utawala wa awamu ya tatu amesema “Umma wa Watanzania unataka mabadiliko na hawaridhishwi na mambo yanavyoendelea ila hofu ndiyo inawafanya wanyamaze, tunaamini ipo siku watapiga kelele.”