Chadema: Tunataka Katiba Mpya au mabadiliko kabla ya 2025
Muktasari:
Msimamo huo umetangazwa leo Ijumaa Julai 28, 2023 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Uhuru maarufu kama Uwanja wa Mayunga mjini Bukoba.
Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepinga mchakato wa Serikali wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa kikidai ni mbinu ya kuandaa Taifa kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 bila Katiba Mpya.
Msimamo huo umetangazwa leo Ijumaa Julai 28, 2023 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Uhuru maarufu kama Uwanja wa Mayunga mjini Bukoba.
‘’Ofisi ya Waziri Mkuu imeviandikia barua vyama vya siasa na asasi za kiraia kuvitaka kuwasilisha maoni kuiwezesha Serikali kuandika upya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa. Hii inaonyesha nia ya kuiandaa Taifa kuingia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025 bila Katiba Mpya,’’ amesema Mnyika
Mtendaji mkuu huyo wa Chadema amesema tatizo la Watanzania siyo sheria ya uchaguzi wala vyama vya siasa, bali ni Katiba inayompa mamlaka Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumteua Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi (NEC) inayosimamia uchaguzi kati ya chama hicho tawala na vyama vishidani.
‘’Katiba tuliyonayo ndiyo inayowaruhusu watendaji na viongozi wa halmashauri ambao ni makada wa CCM kuwa wasimamizi wa uchaguzi,’’ amesema Mnyika
Huku akionyesha msisitizo, Mnyika amesema; ‘’Sisi tunataka ama Katiba Mpya au mabadiliko makubwa ya katiba ya sasa kuondoa kasoro zote zinazofanya chaguzi zetu zisiwe huru na haki ikiwemo Rais na mgombea wa CCM kuwateua viongozi na wasimamizi wa uchaguzi ambao yeye na wagombea wengine kutoka vyama vingine wanashindana,’’
Amewasihi Watanzani wote bila kujali imani, itikadi na maeneo yao kufanya suala la Katiba Mpya kuwa kipaumbele chao cha kwanza kwa faida, maslahi na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu (Bara) amesisitiza umuhimu wa Katiba mpya itakayoweka misingi ya kuwadhibiti viongozi wanaokiuka viapo vyao bila kujali itikadi wala vyama vyao.
‘’Tunataka Katiba itakayowadhibiti viongozi na kulinda maslahi ya Taifa bila kujali ni CCM wala chama gani kiko madarakani,’’ amesisitiza Lisuu
Kuhusu chaguzi zijazo mwaka 2024 na 2025, Mnyika amewataka wana Chadema wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kwa tiketi ya Chadema kujitokeza kutangaza nia na kushiriki ujenzi wa chama hicho kikuu cha upinzani.
‘’Kupitia kampeni yetu ya +255Katiba Mpya, Chadema tunafanya usajili na utoaji wa kadi za uanachama kidijitali; hii siyo tu inalenga kuimarisha uhai wa chama, bali pia kuwezesha mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia ya kidijitali ikiwemo ujumbe mfupi wa maneno,’’ amesema Mnyika
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalim ametumia mkutano huo kuwasihi Watanzania kuulinda Muungano huku wakipigania mabadiliko ya muundo wake kwa sababu una manufaa nyingi kwa Taifa.
‘’Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kupiga kura kuuvunja Muungano wetu; lakini pia nitakuwa wa kwanza kupiga kura kudai marekebisho ya muundo wa Muungano kwa kuwa na Serikali kamili ya Tanganyika na Zanzibar kuondoa kero na malalamiko kutoka pande zote mbili,’’ amesema Mwalimu
Ametoa mfano wa kero kwa upande wa Zanzibar kuwa ni hisia kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano ndiyo maana Mawaziri wa Afya, Elimu na Madini wanaiwakilisha Zanzibar Kimataifa hata katika mambo yasiyo ya Muungano.