Chadema wahoji bajeti kutogusia Katiba Mpya

Chadema wahoji bajeti kutogusia Katiba Mpya

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetaka suala la Katiba Mpya na tume huru ya uchaguzi kuingizwa kwenye bajeti ya Serikali kwa sababu ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetaka suala la Katiba Mpya na tume huru ya uchaguzi kuingizwa kwenye bajeti ya Serikali kwa sababu ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Hayo yamebainishwa leo Jumamosi Juni 12, 2021  mkoani Dar es Salaam na katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akizungumzia bajeti ya Serikali mwaka 2021/22 iliyosomwa bungeni Juni 10, 2021.

Mnyika amesema Katiba mpya ndio mradi muhimu kwa Taifa kwa sasa kwa sababu itajenga misingi ya ujenzi wa Taifa kwa miaka zaidi ya 50 ijayo.

"Jambo la kipaumbele kuliko yote ni kufikiria kuandika Katiba mpya kwa sababu ndio mchakato muhimu kwa maendeleo ya nchi," amesema Mnyika.

Mwanasiasa huyo amewataka Watanzania kujadili kuhusu suala la Katiba mpya kama kipaumbele muhimu ambacho Serikali inapaswa kukifanyia kazi katika bajeti ya mwaka 2021/22.

Kuhusu suala la gharama za kuendesha mchakato huo, Mnyika amesema wananchi wako tayari kutozwa "kodi ya katiba mpya" ili kufanikisha mchakato wa kupata katiba mpya.

"Najua Serikali itatuambia kwamba hawana fedha za kuanzisha mchakato wa Katiba mpya, watuambie. Sisi tuko tayari kulipa kodi ya Katiba mpya badala ya hizi kodi walizozianzisha za laini ya simu na kodi ya majengo kwa kupitia Luku," amesema.

Ameitaka Serikali kuziondoa kodi za laini ya simu na kodi ya majengo itakayolipwa kupitia Luku kwa madai kwamba zitawaumiza wananchi hasa wapangaji ambao watalazimika kulipia majengo yasiyokuwa yao.

Mnyika amesisitiza kwamba ni muhimu mradi wa Katiba mpya kuingizwa kwenye bajeti ya serikali ya mwaka 2021/22 kwa sababu mchakato usipoanza mwaka huu, katiba mpya itachelewa kupatikana.