Chadema: Watanzania tumuenzi Mtei kwa kukamilisha mchakato Katiba Mpya
Katibu Mkuu wa Chedema, John Mnyika akitoa salamu za chama hicho kwenye ibada ya maziko ya Mzee Edwin Mtei nyumbani kwake Tengeru wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha leo Jumamosi Januari 24,2026.bPicha na Filbert Rweyemamu
Muktasari:
- Mzee Edwin Mtei (94),ambaye ni Mwasisi wa Chadema na Gavana wa kwanza wa BoT, alifariki dunia Januari 19, 2026 na anazikwa leo nyumbani kwake Tengeru, Arusha
Arusha. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema kumuenzi mwasisi wa chama hicho, hayati Edwin Mtei (94), kunapaswa kuambatana na dhamira ya dhati ya Taifa ya kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.
Amesisitiza kuwa hilo lilikuwa miongoni mwa maono ya msingi ya waasisi wa chama hicho akiwamo Mtei katika kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria nchini.
Mnyika ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Januari 24, 2026, wakati wa kumbukizi ya maisha ya Mzee Mtei zilizofanyika Arusha, kabla ya maziko yake yaliyopangwa kufanyika mchana wa leo nyumbani kwake Tengeru.
Amesema ni wajibu wa Wanachadema na Watanzania wote wanaoguswa na masuala ya demokrasia kushirikiana katika kutimiza maono ya Mtei, aliyekuwa pia Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Nawaomba Wanachadema na Watanzania wote wanaoguswa na demokrasia nchini. Kuna mambo mawili muhimu ambayo naamini ni sehemu ya kumuenzi Mzee Mtei.
“Kwanza, wazee walipoasisi mageuzi na kuanzisha Chadema walikuwa na wazo la Katiba Mpya. Wakati umefika wa kuyatekeleza maono hayo kwa kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya nchini,” amesema Mnyika.
Ameongeza kuwa jambo la pili katika kumuenzi Mtei ni kuendeleza mapambano ya kidemokrasia ili kuhakikisha mabadiliko ya uongozi yanapatikana kupitia ushindani wa vyama vingi.
“Tanzania imetawaliwa na chama kimoja tangu uhuru. Mzee Mtei alikuwa na maono ya kuona chama kingine kikishika dola. Tuendelee kushirikiana ili siku moja Chadema ishike dola na kuongoza Serikali,” amesema.
Hakuna kulala mpaka kieleweke
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, amesema nyumba ya Mtei ilikuwa kimbilio muhimu la upatanishi wa kisiasa na kijamii, akimtaja kama mpatanishi wa kipekee aliyetoa mchango mkubwa katika historia ya chama hicho na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika kumbukizi hiyo, Golugwa amesema misingi na falsafa aliyoiasisi Mtei, hususan kauli mbiu ya “hakuna kulala mpaka kieleweke”, imeendelea kuwa mwanga na dira kwa viongozi wa Chadema waliopo madarakani ndani ya chama hicho.
“Hakuna kulala mpaka kieleweke ndilo neno ambalo aliliasisi Mzee Mtei. Mara nyingi ukija nyumbani kwake, lazima aseme neno hilo. Nyumba hii ilikuwa ni kimbilio; alikuwa mpatanishi wa kipekee sana,” amesema Golugwa.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche (kulia) akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, Suzan Lyimo (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika wakati wa ibada ya maziko ya Mwasisi wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei nyumbani kwake Tengeru, wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha leo Jumamosi Januari 24,2026. Picha na Filbert Rweyemamu
Ameeleza kuwa viongozi wa sasa wa Chadema wamepokea kijiti cha uongozi kwa ujasiri mkubwa, wakiahidi kuendeleza misingi ya haki, uwajibikaji na mapambano ya kidemokrasia aliyoyaacha Mtei.
Mtei hakuwa msaliti
Mwenyekiti wa baraza la Wazee, Suzan Lymo, amesema mwasisi huyo alikuwa msitahimilivu hakuwa mbinafsi hivyo kuwaomba vijana waache usaliti.
"Maisha ya binadamu ni hadithi tu inategemea hadhithi hiyo unaiwekaje, hadhiti yake itasomwa vizuri amefanya mambo makubwa katika nchi hii ameasisi sera nyingi za fedha.
“Alikuwa mstahimilivu hakuwa mbinafsi kwa vijana wa sasa tunawaomba sana tuache usaliti mzee angekuwa msaliti Chadema isingekuwa hapa tushikamane tulete mageuzi katika nchi yetu," amesema.
Mtei hakupenda uswahili
Rafiki wa Chadema, Jenerali Ulimwengu amesema Mzee Mtei kati ya vitu ambavyo hakuvipenda ni pamoja na 'uswahili', alioutafsiri kama kuahidi mambo yasiyotekelezeka.
"Uswahili ni jambo baya sana na alisema maana ya uswahili ni kusema kitu ambacho unajua si kweli na unatarajia unayemwambia ataamini ni kweli, uswahili ni kutoa ahadi uanzojua hutazitekeleza.
Mwandishi wa habari mkongwe, Jenerali Ulimwengu akizungumza wakati wa ibada ya maziko ya Gavana wa kwanza wa Benki Kuu (BoT) na Mwasisi wa Chadema, Mzee Edwin Mtei aliyezikwa nyumbani kwake eneo la Tengeru wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu
"Uswahili ni upangaji wa maneno mengi ambayo ndani yake hamna kitu, uswahili naongeza mimi ni kuahidi mambo ambayo katika dhamira yako huna nia ya kuyatekeleza na uswahili ni ugonjwa mbaya sana unatufanya tushindwe tuketekeleza tuliyokubaliana."
Alama ya ujasiri
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Ruth Mollel, amesema mwasisi huyo ameacha alama ya ujasiri na uthabiti.
Alitolea mfano namna Mtei akiwa Waziri wa Fedha na Mipango, alitofautiana na Rais Mwalimu Nyerere (hayati), katika sera za fedha na kujiuzulu wadhifa huo.
"Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya baba yetu kwa jinsi alivyokidumisha hiki chama mpaka sasa hivi tuna chama kikubwa na imara sana.
“Ametuachia ‘legacy’ (alama) ya ujasiri na uthabiti kama mtakumbuka alitofautiana na Mwalimu Nyerere na akajiuzulu ni kwa sababu ya misimamo yake na sisi tutaendeleza kusimamia tunachokiamini kwa uthabiti bila kuogopa," amesema.
Salamu za rambirambi
Akiwasilisha salamu za rambirambi za, kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amesema yapo mengi ya kujifunza kwa Mtei kwani alisimama kidete na wenzake kutafuta demokrasia ya vyama vingi nchini.
"Tunaendelea kudai haki, demokrasia na maendeleo ya watu na tutaendelea kujivunia kusimama kwenye mabega ya waliotutangulia kama Mzee Mtei na wengine," amesema.
Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akisaini kitabu cha waombolezaji wakati wa maziko ya Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mzee Edwin Mtei aliyezikwa nyumbani kwake eneo la Tengeru wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha leo Jumamosi Januari 24,2026. Picha na Filbert Rweyemamu
Kiongozi wa zamani wa Chama hicho, Zitto Kabwe amesema wanasiasa na viongozi wa sasa kuna mafunzo makubwa kupitia maisha ya Mzee Mtei.
Amesema Mzee Mtei alieleza kuwa wanaweza kubishana bila kuwekeana chuki na kuendelea kuheshimiana.
"Alionyesha mnaweza kupishana mawazo bila kuwekeana chuki na mkaendelea kuheshimiana ni ukomavu ulioweka taifa pamoja na sasa miaka 60 baada ya uhuru una mashaka haupo na Taifa liko kwenye mtanziko," amesema.
Chaumma
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amesema Mzee Mtei amekuwa mwanademokrasia na mwasisi wa vuguvugu la mabadiliko ya demokrasia nchini.
Amesema moja ya jambo alilowaachia na kama wanamaanisha katika kumuenzi ni uhuru wa mawazo kwani Mtei asingesimama imara katika kuamini uhuru wa mawazo hata ujasiri wa waliosimama usingekuwepo.
"Kama Mzee Mtei asingeamini anachokiamini na akakipigania kwa gharama zozote hata sisi tusingekuwepo na alimiamini na alikuwa tayari kubeba gharama hata kama alibezwa mwanzoni.Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Mzee Mtei aliotuachia tutaendelea kupigania uhuru wa mawazo katika kufikia taifa moja lenye demokrasia,haki na uhuru wa kweli utamalaki,"amesema
CCM
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya, amesema hakuna Mtanzania asiyejua kazi alizofanya Mzee Mtei.
"Hakuna asiyejua kazi aliyofanya Mtei na amekuwa mtendaji kwa Watanzania wote, tumefika hapa kuwapa pole wana Chadema na Watanzania wote kwani aliwatumikia wote na tunamuombea kwa uaminifu na uadilifu wake, amesema
Ujumbe wa miwsho kwa familia
Familia ya Mtei, imesema ujumbe wa mwisho alioacha kwao Mzee huyo ni kuwataka wapendane, washirikiane, wawatunze na kuwaenzi wazee.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mzee Edwin Mtei aliyezikwa leo Jumamosi nyumbani kwake Tengeru wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu
Ujumbe huo aliutoa Julai 12,2024 katika kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa ambapo siku 11 baada ya kutoa ujumbe huo,alipata kiharusi na hakuongea tena hadi alipofariki Januari 19, 2026 baada ya hali yake kubadilika ghafla.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Januari 24, 2026 na mtoto wa Mtei, Mashinda Mtei, aliyekuwa akisoma historia fupi ya Mzee Mtei.
Alianza kwa kueleza kuwa histori hiyo ya baba yao aliichapisha na kuwakabidhi mwaka 2010 akisisitiza wasifanye makosa wakati ikitakiwa kusomwa, hivyo kuisoma kama alivyoandika.
"Julai 12, 2024 wakati tukisheherekea miaka 92 ya maisha yake alitusihi nanukuu "Pendaneni sana,shirikianeni,muwatunze na kuwaenze wazee wetu."
"Siku 11 baadaye alipata kiharusi na hakuongea tena, kwa hivyo huo ujumbe ndiyo neno lake la mwisho kwetu sisi."