Chadema yampa Msajili masharti

Chadema yampa Msajili masharti

Muktasari:

  • Wakati kikao cha vyama vya siasa na Msajili wa Vyama vya Siasa kikitarajiwa kufanyika Oktoba 21 jijini Dodoma, Chadema kimeweka msimamo wa kutoshiriki, huku kikitoa masharti matatu.

  

Dar es Salaam. Wakati kikao cha vyama vya siasa na Msajili wa Vyama vya Siasa kikitarajiwa kufanyika Oktoba 21 jijini Dodoma, Chadema kimeweka msimamo wa kutoshiriki, huku kikitoa masharti matatu.

Kikao hicho ambacho kinatanguliwa na vikao vingine kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na jeshi la polisi pamoja na Baraza la Vyama vya Siasa, lengo lake ni kuandaa agenda za kikao cha wadau hao.

Akitoa maazimio ya kamati kuu jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Benson Kigaila alisema katika kikao kilichofanyika juzi kwa njia ya mtandao, agenda kubwa ilikuwa kujadili hali ya kisiasa nchini.

Alisema agenda nyingine zilizojadiliwa ni pamoja na kikao walichoalikwa na ofisi ya Msajili wa Vyama kupitia Baraza la vyama vya Siasa kilichofanyika jana, ikiwa ni maandalizi ya kikao cha wadau kitakachofanyika Dodoma, Oktoba 21 na 22, mwaka huu.

“Msajili anatuita tukae kujadili marekebisho ya sheria, ukweli ni kwamba hata siku moja hakuna chama cha siasa hata kimoja kilichowahi kumpelekea msajili malalamiko ya sheria hiyo,” alisema Kigaila.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alipoulizwa kuhusu msimamo huo wa Chadema, alisema: “Sijapokea taarifa yeyote kutoka Chadema na sipokei taarifa kutoka kwenye vyombo. Ninataka wanifikishie hiyo taarifa kwa vile tunazihitaji hiyo siku ya kikao. Tuchukulie mambo kwa uzito wake.”

Kigaila alisema baada ya kikao chao jana, wameazimia kutoshiriki kikao chochote na Msajili wa vyama hadi pale mambo ya msingi waliyopendekeza yatakapopatiwa suluhisho.

“Kimsingi kamati kuu imekubaliana kutoshiriki vikao hivi hadi pale zuio la shughuli za vyama vya siasa ikiwamo mikutano ya hadhara litakapoondolewa, ili tunapoenda kukutana naye tukutane kama vyama huru.

“Jambo lingine kamati kuu imekubaliana, hatutaweza kwenda kwa Msajili hadi mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe atakapoachiwa huru bila masharti ili tunapokwenda kwenye vikao tuwe naye,” alisema Kigaila.

Alisema kabla na wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wapo viongozi na wanachama wa Chadema waliokamatwa na kuwekwa ndani kwa sababu za kisiasa, nao wanapaswa kuachiwa huru.

Akizungumzia suala Rais Samia kukutana na vyama vya siasa, Kigaila alisema wako tayari kukutana naye kwa kuwa ni ombi ambalo chama hicho ililitoa baada ya mwenyekiti kumuandikia barua ambayo aliijibu, lakini hadi sasa amekuwa akikutana na makundi mengine. “Wakati hatujakutana na Rais, tujadiliane mambo yanayotuletea ufa kwenye Taifa, tuko tayari kukutana naye, lakini sio Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu alisema matatizo yoyote ya chama cha siasa, sehemu sahihi pa kuyazungumza ni kwenye kikao hicho kwa kuwa wahusika wote watakuwepo wakiwemo mawaziri, viongozi wa dini na vyombo vya ulinzi na usalama.

Alisema kama Chadema wameweka msimamo wa kutohudhuria, anaheshimu uamuzi wao.

“Kwanza niseme naheshimu uamuzi wao, kikao kina nia njema, kina jambo la heri kama wao hawaji ni uamuzi wao, lakini wangekuja wakazungumza ndani ya hicho kikao labda suluhu inaweza kupatikana, lakini kama wameamua hivyo, basi vyama vingine vitakuja,” alisema Khatibu. Kuhusu kuachiwa kwa Mbowe alisema, jambo hilo liko mahakamani hivyo hawawezi kuingilia uhuru wa chombo hicho na kuwashauri waiachie mahakama itekeleze wajibu wake.

Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasi Tanzania (TCD), Zitto Kabwe alisema hawawezi kuingilia uhuru wa kila chama kushiriki au kutoshiriki kikao hicho, unabakia kwao.