Chadema yasisitiza kufanya kongamano Mwanza licha ya zuio la polisi

Monday July 19 2021
chadema pc
By Peter Saramba
By Saada Amir

Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo ((Chadema) kimesisitiza kufanya kongamano la Katiba Mpya jijini Mwanza bila kujali zuio la polisi.


Msimamo huo umetangazwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatatu Julai 19.


"Hatuhitaji kibali cha mtu kukutana kwenye vikao vya ndani kujadiliana kuhusu maslahi na hatma ya Taifa letu. Katiba ya nchi ni Katiba ya Taifa, siyo Katiba ya chama chochote cha siasa. Hapaswi kuwepo kiongozi yeyote kuzuia mijadala na upatikanaji wa Katiba," amesema Mbowe.


Ametangaza kuwa kongamano lililoshindika Jumamosi ya Julai 16 kwa kuzuiwa na polisi sasa utafanyika Jumatano ijayo Julai 21.


"Kama polisi wanataka kutuzuia wajiandae kufanya hivyo wakiwa tayari kutukamata viongozi na wanachama wote kwa sababu sote hatutaondoka Mwanza hadi tufanye kongamano la Katiba mpya," amesisitiza Mbowe.


Amesema baada ya kongamano la Mwanza na vikao vingine vya ndani vya chama hicho, Chadema itatangaza operesheni ya nchi nzima itakayohusisha mikutano ya hadhara kwa sababu ni haki na wajibu wa kikatiba na kisheria.

Advertisement

Kiongozi huyo ametumia mkutano huo kulaani kitendo cha polisi kuzuia kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) akisema lilikuwa zuio haramu katika macho na misingi ya Katiba na sheria.

Advertisement