Chadema yataka sababu kuyumba NHIF

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

  • Chama cha Chadema kimeitaka Serikali kuweka wazi sababu za hali mbaya inayoukabili Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) badala ya kueleza Hali hiyo pekee.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka Serikali kutoa taarifa ya sababu za hali mbaya ya kifedha iliyoutokea Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), badala ya kukiri peke yake.

Kauli hiyo imetolewa leo, Septemba 20, 2022 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu Jumaa alipotoa maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichoketi Septemba 17 na 18 mwaka huu.

Mwalimu amesema kamati Kuu ya Chadema imeazimia kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya uchunguzi katika mfuko huo.

"Kamati Kuu imemtaka CAG kufanya ukaguzi maalumu kwenye mfuko huo na kujua mwenendo wa fedha za wananchama.

"Sio kuambiwa hali mbaya pekee, bali tupewe taarifa ya sababu za kufikiwa kwa hali hiyo, kazi hii ifanywe na CAG," amesema.

Kuhusu muswada wa bima ya afya kwa wote uliowasilishwa bungeni hivi karibuni, Mwalimu amesema kamati kuu imeitaka Serikali kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kutoa maoni juu ya suala hilo.

Amesema kutokana na unyeti na ukubwa wake, halipaswi kuamuliwa kama hati ya dharura, bali linahitaji uwazi na muda wa kutosha.

"Tunapinga hati ya dharura, kwa sababu wanaopeleka kwenye hati ya dharura ndiyo waliofilisi mfuko wa awali wa bima," amesema.

Pamoja na hayo, amesema mambo mengine yaliyoazimiwa na Kamati Kuu hiyo ni kufutwa kwa tozo za miamala ya benki, simu na ving'amuzi, kuimarishwa kwa njia za usimamizi wa bei ya chakula na kuchukua hatua za wazi dhidi ya wabafhilifu waliotajwa na CAG Zanzibar.