Chadema yatia mguu zuio uuzwaji sukari, mchele nje ya nchi

Muktasari:

  • Baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutangaza zuio la uuzaji nje ya nchi bidhaa ya sukari na mchele, Chadema kimeitaka itoe maelezo ya kina juu ya marufuku hiyo.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikitangaza zuio la uuzaji nje ya nchi bidhaa ya sukari na mchele, Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) kimeitaka itoe maelezo ya kina juu ya marufuku hiyo.

Kimesema uamuzi huo umefanyika wakati ambao, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijaweka mikakati ya kutosha kuhusu kilimo cha mazao hayo.

Kauli hiyo ya Chadema inakuja wiki moja baada ya Serikali ya Zanzibar kupitia Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban izuie uuzaji wa bidhaa hizo nje ya nchi.

"Kwa kutekeleza mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 35(1) cha Sheria ya Biashara ya Zanzibar, namba 14 ya mwaka 2013, mimi Omar Said Shaaban, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

"Naagiza katazo la kusafirisha mchele na sukari nje ya Zanzibar kwenda nchi yoyote, kuanzia tarehe 30 Januari, 2023," imeeleza katika taarifa hiyo ya Omar.

Leo, Februari 10, 2023 Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu amewaaeleza waandishi wa habari kuwa kilichofanywa na Serikali hiyo ni sawa na kujifungia.

"Hakijatosha kutoa tu tamko hilo ipo haja ya Serikali (Zanzibar) kutoa maelezo ya kwanini imefikia uamuzi huo na mikakati yao ya kuhakikisha hilo linalotokea halitajirudia," alisema.

Alisema wakati Watanzania wanahangaika kutafuta chakula kufungiana kunahatarisha uzalishaji wa changamoto nyingine.

Kama sababu ya uamuzi huo ni kuviwezesha visiwa hivyo kujitosheleza kwa chakula, alisema nyema Serikali ingekuja na mkakati wa uzalishaji katika kilimo.

Kwa mujibu wa Mwalimu, Zanzibar ina maeneo mazuri yanayowezesha uzalishaji wa bidhaa hizo kiasi cha kutosheleza mahitaji ya wananchi na hata kuuza nje ya nchi.

"Uko wapi mkakati mahususi wa Serikali katika kilimo, naamini kama utawekwa mkazo visiwa hivyo vinaweza kupata chakula cha kutosheleza na kuuza nje," alisema.

Hata hivyo, alisema visiwa hivyo ni kitovu cha biashara kulingana na historia yake, kitendo cha kuweka marufuku kunafifisha fursa hiyo.

"Zanzibar ni kitovu cha biashara na hiyo ni asili na ndiyo heshima ya Zanzibar, biashara lazima itazamwe kuwa fursa pana na siyo changamoto bila kuathiri ustawi na usalama wa wananchi," alisema.

Tatizo lilipo alisema: "Ni ama juhudi za Serikali ndogo au hazipo kabisa katika baadhi ya maeneo na hatimaye tunajikuta katika kufunga, tutajifungia hadi lini."