Chadema yatoka na maazimio

Chadema yatoka na maazimio

Muktasari:

  • Baada ya Jeshi la Polisi kumkamata na kumhusisha Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe na tuhuma za mauaji na makosa ya ugaidi, chama hicho kimeweka msimamo mkali, huku pia wakiyahusisha makosa hayo na hujuma za kisiasa.

Dar/Mwanza. Baada ya Jeshi la Polisi kumkamata na kumhusisha Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe na tuhuma za mauaji na makosa ya ugaidi, chama hicho kimeweka msimamo mkali, huku pia wakiyahusisha makosa hayo na hujuma za kisiasa.

Mbowe na baadhi ya viongozi wa Chadema walikamatwa Julai 21 jijini Mwanza wakati wakijipanga kufanya kongamano la Katiba lililopigwa marufuku jijini humo.

Hata hivyo, Mbowe alisafirishwa kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam ambako alipekuliwa nyumbani kwake, huku taarifa iliyotolewa na Polisi juzi ikieleza kuwa Mbowe alikamatwa akihusishwa na makosa ya ugaidi na njama za kutaka kuua viongozi wa Serikali.

Lakini akizungumza juzi na waandishi wa habari kupitia mtandao wa Zoom, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anayeishi nchini Ubelgiji, alisema tuhuma hizo ni hujuma za kisiasa zinazofanywa na Serikali ya CCM.

“Makosa hayo ni mlolongo mrefu wa makosa ya kubambika ya jinai ambayo Mbowe na viongozi wake kwa sababu tu ya kuwa viongozi wa Chadema wanapewa.

“Ni mlolongo wa vita dhidi ya Chadema inayoendeshwa na CCM na Polisi na vyombo vya usalama. Ni vita ya kisiasa,” alisema Lissu.

Alipoulizwa kuhusu undani wa makosa anayokabiliwa Mbowe, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisita kuzungumza akisema atakuwa anatoa ushahidi unaotakiwa kutolewa mahakamani.

“Kuna vitu vingine siwezi kuvitoa kwa sababu ni sehemu ya ushahidi, unachotakiwa kujua ni kwamba anatuhumiwa kwa kosa fulani, ushahidi uliopo utafikishwa mahakamani. Ukitaka kujua ni nani na nani (aliotaka kuwaua) utaukuta mahakamani,” alisema Misime.

Alipoulizwa sababu ya kumkamata Mbowe kwenye maandalizi ya kongamano la Katiba kwa makosa mengine, Misime alisema, “Hamna sheria inayosema kwamba mtu akamatwe namna gani. Wakati wowote tunapojiridhisha na ushahidi wetu tutamkamata mahali popote.”

Katika maelezo ya Lissu, aliyedai kuiona karatasi ya mashitaka, alisema kosa la ugaidi analotuhumiwa Mbowe limetokana na mchuano wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo walinzi wake sita walikamatwa.

“Mwaka jana baada ya uchaguzi kulikuwa na vita kali. Kwa Mbowe moja kwa moja kulikuwa na vita kubwa ambapo biashara za Mbowe ziliharibiwa,” alisema Lissu akiwataja baadhi ya wakuu wa wilaya aliodai kuwa walihusika.

Kuhusu walinzi hao ambao walifunguliwa kesi Na.63 ya 2020 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, alisema miongoni mwa makosa sita wanayotuhumiwa nayo ni pamoja na ugaidi na uhujumu uchumi.

“Lengo la kumuunganisha mwenyekiti ni kuhakikisha anakosa dhamana ili hii shughuli za kudai Katiba ishindikane,” alisema Lissu.

Huku akitoa mfano wa Mwalimu Julius Nyerere na wenzake waliotiwa hatiani kwa makosa ya uchochezi mwaka 1958, Lissu alisema huo ni mwendelezo wa ukandamizwaji wa kikoloni.

Alisema miongoni mwa waathiriwa wa unyanyasaji huo ni yeye mwenyewe ambaye mpaka sasa ana kesi sita mahakamani, huku pia akiwataja aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wengine wa Afrika, akiwemo Rais wa zamani wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela.

Katika hatua nyingine Lissu amekosoa ukamataji na upekuzi uliofanywa nyumbani kwa Mbowe akisema; “Upekuzi wa Mwenyekiti umefanyika usiku, sheria za Tanzania zinasema searching zifanyike mchana.”

Hata hivyo, akijibu madai hayo Kamanada wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alikanusha akisema kama kuna malalamiko ya mchakato mzima wa ukamataji yapelekwe mahakamani.

“Kama tumepekua kisheria au siyo kisheria tuwasubiri mahakamani. Kwa sababu hata kukamata wanasema hatukukamata kihalali na makosa si halali, mbona wanaanza mambo ya mahakamani kabla hatujafika?

“Ni sheria gani iliyosema usiku mtu hapekuliwi? Usiku hakuna makosa? Kwa hiyo ukiambiwa kuna mali ya wizi iko sehemu fulani, ukapekue asubuhi ili ukute imehamishwa?”

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 40, upekuzi hufanywa mchana usipokuwa kwa idhini ya mahakama.

“Hati ya upekuzi inaweza kutolewa na kutekelezwa siku yoyote (ikiwemo Jumapili) na inaweza kutekelezwa kati ya muda wa jua kuchomoza na jua kuchwa lakini mahakama inaweza, kwa maombi ya ofisa polisi au mtu mwingine ambaye imeelekezwa, kumruhusu kutekeleza katika muda wowote.”

Msimamo wa Chadema

Akieleza maazimio yaliyotolewa na Kamati Kuu ya Chadema juzi, Lissu alisema wamekubaliana kuunda kamati itakayoendesha kampeni ya kimataifa duniani kote kuieleza dunia kuhusu ukandamizwaji wa demokrasia nchini.

Huku akimkosoa Rais Samia Suluhu Hassan, Lissu alisema kamati hiyo atakayeiongoza mwenyewe itaieleza dunia kuhusu ukandamizwaji wa vyama vya upinzani.

“Tutaiambia dunia kwamba sheria zote za ukandamizaji zinaendelea na kwamba hawataki Katiba mpya.

Pia alisema wataiambia dunia iweke mashinikizo ya kiuchumi, ya kisiasa hadi Serikali ifuate haki za kibinadamu kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tanzania.”

Alisema uamuzi mwingine uliofikiwa na Kamati kuu ni kuundwa kwa kamati ya ndani ya nchi kwa ajili ya kuratibu utafutwaji wa Katiba mpya.

“Kampeni ya Katiba inaendelea na kongamano la Mwanza liko pale pale. Tutajipanga tutarudi. Tutafanya makongamano kama hayo mikoa mbalimbali,” alisema.

Kukutana na Rais Samia

Alipoulizwa kama kuna mkakati wa kumaliza mvutano wao na Serikali kwa njia ya mazungumzo, Lissu alisema wameshamtafuta Rais Samia kutaka kuzungumza naye lakini hadi sasa hawajaitwa.

“Mimi mwenyewe nilimpigia simu Rais ikapokelewa na (anamtaja), nikaambiwa nitatafutwa, lakini mpaka sasa sijatafutwa,” alisema.

Aliongeza kuwa chama hicho kilishamwandikia barua Rais Samia tangu Machi mwaka huu, kuomba kukutana naye lakini hawajaitwa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu alipoulizwa kuhusu maombi ya Chadema kukutana na Rais, alisema: “Kama wameomba na wamefuata utaratibu, basi watajulishwa kwa utaratibu walioufuata.”

NCCR Mageuzi, ACT wajitosa

Wakati huo huo, vyama vya NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo vimelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia huru viongozi 15 wa Chadema, akiwemo Mbowe waliokamatwa.

Katika tamko lao la pamoja walilotoa jana, Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe wameomba kikao kati ya viongozi wa Serikali na wa vyama vya siasa kujadiliana namna njema ya kufanya siasa bila uhasama.

“Ni wakati sasa wa viongozi kuzungumza (political dialogue),” imesema taarifa hiyo ya ukurasa mmoja.

Hadi jana mchana, viongozi 15 wa Chadema waliokamatwa na polisi alfajiri ya kuamkia Julai 21 walikuwa wanaendelea kuhojiwa.

Imeandikwa na Elias Msuya, Peter Saramba, Mgongo Kaitira na Saada Amir, Mwanza