Chadema yawakana Halima Mdee na wenzake

Wednesday November 25 2020
mnyika pic
By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema hawatambui orodha ya wabunge wa chama hicho wa viti maalum walioapishwa na Spika Job Ndugai mjini Dodoma leo Jumanne Novemba 24, 2020.

 Kimesema kamati kuu ya chama hicho ndio hukaa na kupitisha majina hayo lakini haijafanya hivyo,  hata mchakato wa kuyapeleka majina ya wabunge wa viti maalum wa chama hicho Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pia haukufanyika.

Walioapishwa leo ni HalIma Mdee, Grace Tendega, Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed.

Wengine ni Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mnyika amesema, “

Advertisement

hakuna orodha iliyopelekwa na chama, waulize Bunge na NEC  hiyo orodha imepelekwa na nani?”

Alipoulizwa chama kitachukua hatua gani baada ya kutokea kwa jambo hilo, Mnyika amesema, “tumeshaona tutakaa na kujadiliana na kueleza hatua tutakazochukua. Kwa sasa tambueni hatukupeleka orodha.”

Hata hivyo, Halima wakati akizungumza baada ya kuapishwa kwa niaba ya wenzake alisema wamepata baraka za chama hicho huku akimtaja mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Halima ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) amesema, “nikushukuru kwa kiapo kufanyika na kukamilika, nikishukuru chama changu kupitia wao sisi tumepata nafasi hii ya kukiwakilisha chama chetu. Viti hivi sio hisani ni sehemu ndogo ya ushindi mkubwa ambao chama chetu kilipata.”

“Nikuhakikishie mheshimiwa spika tutafanya kazi kwa uaminifu kama kambi rasmi ya upinzani bungeni na kwa uadilifu mkubwa kwa viwango vilevile tulivyokuwa tunavifanya. Kuna vijana wapya sisi kama dada zao tunakuhakikishia watafanya kazi bora. Niwahakikishie wana Chadema tutafanya kazi mliyotutuma kwa uaminifu na uadilifu mkubwa sana.”

Huku akiwa makini amesema, “kwa mujibu wa matakwa ya sheria ya nchi chama chetu kimekidhi kigezo vya kupata viti maalumu, viti hivi si hisani ila ni sehemu ndogo ya ushindi mkubwa ambao chama chetu kimepata.

Advertisement