Chaguzi ndogo zilivyotikisa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Muktasari:
- Tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama hivyo mwaka 1995, Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na mitikisiko ya kisiasa mara kwa mara ambayo imesababisha migawanyiko kwenye jamii.
Tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama hivyo mwaka 1995, Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na mitikisiko ya kisiasa mara kwa mara ambayo imesababisha migawanyiko kwenye jamii.
Uhasama huo ulisababisha watu wasishirikiane katika msiba, harusi, vikao na shughuli mbalimbali.
Mitikisiko hiyo imesababisha uhasama wa kisiasa ambao ni kati ya chama kikuu cha upinzani wakati huo CUF chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu , Hayati Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye mara kadhaa alikuwa akidai anapokwa ushindi wa urais wa Zanzibar.
Maalim Seif na wafuasi wake baada ya kuhamia ACT-Wazalendo kimekuwachama kikuu cha upinzani na kukihenyesha CCM.
Uhasama wa kisiasa Zanzibar ulipungua kuanzia mwaka 2010 baada ya mabadiliko ya Katiba ambayo yalianzisha mgawanyo (kugawana) madaraka kati ya mshindi wa uchaguzi mkuu na anayeshikilia nafasi ya pili.
Rais Aman Abeid Karume na Maalim Seif walikutana na kumaliza tofauti za kisiasa zilizounda mwafaka uliochangia kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2010.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Chama cha Mapinduzi (CCM) na CUF zilishirikiana kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo kwa kiasi kikubwa ilituliza joto la kisiasa kwa miaka mitano (2015-2020) baada ya hapo matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na chaguzi ndogo yameanza kutikisa Serikali hiyo.
Julai 18 mwaka huu ulifanyika uchaguzi mdogo katika jimbo la Konde wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na kumpata mbunge wa jimbo hilo.
Uchaguzi huo ulishirikisha vyama vya siasa 12 na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) Zanzibar, chini ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo, Yassin Khamis ilimtangaza Sheha Faki Mpemba (CCM) kuibuka kidedea kwa kupata kura 1,796 na kuwabwaga wapinzani wake.
Alifuatiwa na Mohamed Said Issa wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 1,373 kati ya kura 5,050 zilizopigwa na kura 30 zikikataliwa.
Uchaguzi huo ulikuwa unaziba pengo lililoachwa wazi kutokana na kifo cha Khatib Said (ACT –Wazalendo).
Hii ni mara ya pili kufanyika uchaguzi tangu iwepo Serikali moja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar na chaguzi hizi ziliangaliwa kama kipimo cha jinsi utayari wa maridhiano unaohubiriwa na viongozi wakuu wa nchi unavyoweza kufanya kazi katika mazingira ya ushindani wa kisiasa.
Uchaguzi wa kwanza ulifanyika Machi 28 mwaka huu katika jimbo la Pandani wilaya ya Wete kisiwani Pemba ili kumpata mwakilishi wa jimbo hilo katika baraza la wawakilishi baada ya aliyekuwa mwakilishi awali, Abubakar Khamis Bakar (ACT Wazalendo) kufariki dunia.
Katika uchaguzi huo wa Pandani, Professa Omar Fakhi Hamad (ACT- Wazalendo) aliibuka kidedea kwa kupata kura 2,361 sawa na asilimia 52.5 akifuatiwa na Mohamed Juma Ali (CCM) aliyepata kura 1,934 sawa na asilimia 43.
Pia siku hiyo ulifanyika uchaguzi mdogo katika wadi (kata) ya Kinuni Wilaya ya Magharibi B, mgombea wa CCM, Maryam Rajab Masinga aliibuka kidedea baada ya kupata kura 2,376 sawa na asilimia 87.6, akifuatiwa Hamad Hassan Hamad (ACT- Wazalendo) aliyepata kura 313 sawa na asilimia 11.6.
Nafasi hiyo ilitokana na aliyekuwa diwani mteule, Suleiman Mohamed Hassan (CCM) kufariki dunia siku chache baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.
Hata hivyo chaguzi hizi zote, chama cha ACT-Wazalendo kimezilalamikia, ukiwemo wa Pandani ambao kiliibuka mshindi wakisema zimevurugwa, dhuluma imetawala, nguvu nyingi kutumika na kuendesha mambo kinyume na utaratibu.
Manung’uniko ya chaguzi
Wananchi, wanachama na wafuasi wa ACT Wazalendo wanasema kadri chaguzi zinavyoendeshwa hawaoni nia ya dhati ya kudumisha na kuendeleza serikali ya umoja wa kitaifa.
Hatua hiyo inawafanya kumuomba Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud kuingilia kati na kumueleza Rais Mwinyi ukweli kuhusu hali hiyo na hatima yao katika serikali hiyo wakidai wamechoka na dhuluma wanazofanyiwa katika chaguzi hizo.
“Tunaomba sana uchaguzi huu uingiliwe kati kama ni kurudiwa au kama ni kutangaza aliyeshinda kihalali ijulikane, lakini dhuluma iliyofanyika inarudisha machungu ya yale yaliyofanyika nyuma,” anasema Khatib Khamis wa Chakechake.
Khamis anasema hawatakubali kejeli, lugha za kebehi na dharau wanazofanyiwa kwa kuwa wakati wakiingia kwenye Serikali walilenga kudumisha umoja, Amani, mshikamano ambao sasa inaonekana CCM hawautaki.
Mzee mwingine, Yusuph Ali Mzee anasema “tumechoka, tumenyanyaswa, tumedhulmiwa na kuuawa sote humu hakuna asiye na kovu katika chaguzi zilizopita leo tumeingia Serikali ya Umoja wa Kitaifa tukiamini wenzetu kwamba ni waungwana lakini wanafanya yale yale, tufike mahali tuseme hapana.”
“Tunataka mazungumzo na Dk Mwinyi kama kweli yupo tayari kutika Serikali ya umoja wa kitaifa basi tuone vitendo vyake, watu wanatumia nguvu kubwa kuumaliza upinzani lakini Mungu ndiye anajua,” alisema Said Yusuph Omary.
Viongozi wa ACT Wazalendo watema nyongo
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT-Wazalendo, Salim Bimani anasema chaguzi hizo zinavurugwa na NEC, CCM na vyombo vya dola wakitumia nguvu kubwa na kuwanyima haki wengine.
Anasema kwa historia ilivyo katika jimbo la Konde, miaka yote CCM hawajawahi kupata kura zaidi ya 700, lakini inashangaza katika uchaguzi huu wamepata zaidi ya kura 1,000.
Anasema katika mazingira na namna chaguzi zinavyoendeshwa ni dhahiri wanatikisa maridhiano na muundo wa SUK, huku pia akisema Rais Mwinyi anahujumiwa na watu wanaomsaidia.
Julai 22 kamati ya uongozi ya chama hicho ilikaa Unguja na kusikitishwa na mwenendo wa chaguzi za marudio kugubikwa na kile walichodai hujuma na uvunjifu wa haki za binadamu na misingi ya kidemokrasia.
Hata hivyo, Bimani anasema kamati hiyo imeelekeza sekretarieti ya chama hicho Taifa kuitisha kikao cha kamati kuu ya dharura kitakachofanyika hivi karibuni kisiwani Pemba kujadili mustakabali wa ushiriki wa chama hicho katika SUK. Mbali na kujadili mustakabali wa SUK, pia sekretarieti hiyo itajadili hali ya kisiasa na kidemokrasia na mwelekeo wa chama wakati wa kuelekea katika uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Kauli ya CCM
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdulla Juma Mabodi anasema wapinzani wamezoea kulalamika na kwamba ushindi huo wameupata kihalali baada ya kuwashinda kwa mbinu na kusoma udhaifu wao.
“Kwanza tumefanya kampeni za kisayansi, tulikuwa na timu kubwa, tukaanza kwenda mwendo wa ‘nyakunyaku’ yaani hii ni njia ya kwenda nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa na kuwafikia wananchi wote,” amesema.
Anasema wananchi wameanza kuelewa sera za chama hicho na kuwashinda wenzao ambao mara nyingi wanapenda kutumia siasa za kuhamasisha vurugu.
Msimamo wa Othman
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman ambaye ni mjumbe wa Kamati kuu ya ACT-Wazalendo alionekana kukerwa na mazingira ya chaguzi hizo.
“Mambo haya hayavumiliki ikizingatiwa tayari kulikuwa na ahadi kwamba kutafanyika uadilifu, lakini kwa sasa inashuhudiwa dhuluma juu ya dhuluma ambayo inatengeneza kiza,” alisema.
“Kama uchaguzi ndio wa namna hii unavyoendeshwa maana imeshakuwa ndio mwelekeo, tumetoka Pandani tumekwenda Konde staili ni hii, sasa mimi kwa fikra zangu, viongozi wa chama na wazee mpo, kama hakuna dhamira ya kubadilika inayoonyeshwa kwa vitendo tumekaa miaka yote hatukushiriki kwenye uchaguzi nchi ilikwenda.”
Kauli ya Dk Mwinyi
wiki iliyopita baada ya kusali swala ya Ijumaa katika msikiti wa Wireless Unguja, Dk Mwinyi aliwaeleza waumini na wananchi wote kwamba katika suala la kudumisha amani na mshikamano lazima kuwapo na misukosuko, lakini jamii haina budi kuvuka salama.
Bila kugusia suala la uchaguzi huo, Dk Mwinyi alisema hakuna jambo lisilozungumzika pindi inapotokea mitihani, hivyo ni vyema jamii ikakaa chini na kuzungumza kwa azma ya kupata mwafaka ili kudumisha amani, mshikamano na umoja uliopo kwa kuwa hakuna maendeleo bila utulivu wa amani.
NEC wanena
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Konde Yassin Khamis anasema tuhuma zinazotolewa sio za kweli maana uchaguzi uliendeshwa kwa mujibu wa taratibu zote za NEC akidai hakuna haki iliyokiukwa.
“Sisi tulitimiza wajibu wetu vizuri kwa kufuata sheria na taratibu”