Chalamila awatumia ujumbe ‘wanaoleta chokochoko mitandaoni’
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema mkoa wa Dar es Salaam ni kutovu cha Kidiplomasia nchini, akiwataka viongozi ndani ya mkoa kuhakikisha unabaki kuwa salama dhidi ya wanaoleta chokochoko.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila ametaja mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama wa jiji hilo dhidi ya alichokiita chokochoko mitandaoni.
Chalamila ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 15, 2026 alipozungumza na wenyeviti na watendaji wa mitaa jijini Dar es Salaam.
Akitaja sababu za kuweka mikakati ya usalama wa mkoa huo, Chalamila amesema Dar es Salaam ndio inaongoza kwa kuchangia Pato la Taifa, ukiwa kitovu cha diplomasia, hivyo unahitaji ulinzi imara dhidi ya vichocheo vya uvunjifu wa amani.
"Mkoa wetu ndio unaohudumia mikoa mingi, ukiwa na uwekezaji wa kimkakati, pili ni kitovu cha diplomasia ndiyo maana unaona tunapokea marais," amesema.
Amesema pia jiji hilo ndilo lenye watu wengi zaidi, likichangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa, hivyo haupaswi kuangaliwa kwa jicho la kawaida.
Amesema, kutokana na sifa hizo za jiji hilo, mkoa huo ukiathiriwa na vurugu utaathiri uchumi wa nchi na kuathiri hifadhi ya chakula na machafuko ya kisiasa nchini.
"Mkoa huu tuuone kuwa ni mkoa muhimu, kila mmoja aone kuwa anawajibu kuhakikisha unakuwa salama," amesema.
Amesema kwenye mitandao, baadhi ya watu wanataka kuleta chokochoko, hali inayohitaji kuimarishwa kwa ulinzi na usalama.
Amefafanua katika kuhakikisha jukumu hilo, Serikali itaendelea kutumia nguvu kubwa katika kukabiliana na tishio lolote la amani.
"Mkoa huu ukifungwa, tayari utakuta hatuna hifadhi ya chakula, na hapo ndipo kasheshe itakapotokea na inaweza kusababisha machafuko ya kisiasa tukaendelea kupigana wenyewe.
"Ndiyo maana nimesema, nguvu ambayo ilishawahi kutumika mahali popote katika kulinda amani, ilikuwa ni majaribio ya kuona je, jambo lolote likitokea katika nchi yetu, tunaweza?" amesema.
Amesema nguvu ambayo huwa inatumika kulinda amani wakati mwingine huwa ya kawaida, akifafanua kuwa nguvu ambazo zitaendelea kutumika katika kulinda amani, pengine hazijawahi kutumika mahali popote.
"Nguvu yenyewe halisi ya ulinzi wa amani, itaanza kujionyesha taratibu yenyewe kadri mtu mwenyewe anavyokuja kwetu," amefafanua.
Akiweka wazi mikakati ya kuimarisha ulinzi, Chalamila ameagiza kila mtaa wa jiji hilo kuwe na sungusungu huku akisisitiza ajenda ya usalama itolewe kila sehemu ikiwemo misikitini na makanisani.
Amezungumzia matukio ya mtoto na Mchina waliouawa Dar es Salaam hivi karibuni, akisisitiza matukio hayo hayakubaliki na yanautia doa mkoa huo.
Aidha, Chalamila amewaagiza viongozi wote wa mkoa huo wakiwemo wakuu wa wilaya, madiwani, wenyeviti na watendaji wa mitaa kuhakikisha wanaimarisha ulinzi katika maeneo yao.
Amewataka viongozi hao kutojibizana na watu wanaoeneza taarifa za vurugu zikiwemo za maandamano badala yake wasimamie ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Akizungumza katika kikao hicho, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal ameahidi kufanyia kazi maelekezo hayo, akiwaagiza viongozi na watendaji wa jiji hilo kuhakikisha maelekezo hayo wanayafanyia kazi.
"Na mimi kwa niaba ya wenzangu na wananchi nikuahidi maelekezo tunakwenda kuyafanya kazi. Maelekezo haya uliyoyatoa kimsingi ndiyo dira ya kiongozi wa nchi yetu," amesema.