Chama cha wahasibu chamkumbuka Dk Mengi

Muktasari:

Licha ya mafanikio yake kwenye ujasiriamali, Dk Reginald Mengi alikuwa mhasibu aliyethibitishwa na bodi ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu za fedha (CPA) na mwachama hai wa TAA.

Dar es Salaam. Kuenzi mchango wa waanzilishi wake, Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) kimetoa vyeti kimetoa vyeti kwa wenyeviti wake wastaafu na kumtambua marehemu Reginald Mengi.

Akitoa vyeti hivyo, mwenyekiti wa TAA anayemaliza muda wake, Dk Fred Msemwa amesema Dk Mengi alikuwa mhasibu makini aliyesimamia maadili ya taaluma hiyo.

 “Wazee wetu walikianzisha chama hiki na wametuachia tukiendeleze kupigania haki zetu huku tukitimiza wajibu kwa jamii,” amesema Dk Msemwa.

Kwa miaka mingi aliyohudumu kwenye baraza la chama hicho, Dk Mengi alikuwa mwenyekiti wa kamati ya maadili.

Dk Msemwa amesema wahasibu wana mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania hivyo ni lazima wawe pamoja ili kukumbushana umuhimu wa kutanguliza uzalendo katika utekelezaji wa majukumu sambamba na kutetea na kulinda hadhi ya taaluma yao.

TAA ilianzishwa mwaka 1983 na Hatibu Senkoro akachaguliwa kuwa mwenyekiti wake wa kwanza mpaka mwaka 1987 alipolithiwa na Ernest Massawe aliyekiongoza hadi mwaka 1991.

Kwa miaka tofauti, wenyeviti wengine walichaguliwa akiwamo Biharialal Tanna (1991-1993), Leonard Mususa (1993-1997), Cosmas Lamosai (1997-2001) na Mercy Sila (2001-2005). Baadaye alifuata Nada Margwe (2005-2009) na Oswald Urassa (2009-2015) halafu Dk Msemwa (2015-2019).

Hivi sasa, chama hicho kimemchagua Peter Mwambuja kuwa mwenyekiti wake wa 10 tangu kilipoanzishwa.