Changamoto za kudhibiti kaboni katika viwanda

Dar es Salaam. Upungufu wa bajeti, wakaguzi wa mazingira na kutokuwepo utii wa sheria ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kudhibiti uzalishaji wa hewa ya kaboni nchini.

Changamoto hizo zinaathiri ukaguzi zaidi ya asilimia 60 ya viwanda katika Mkoa wa Dar es Salaam na halmashauri zake na hivyo kutoa mwanya wa ukiukwaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Fredrick Mulinda, ofisa mazingira mwandamizi katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) anasema baraza hilo linakabiliwa na changamoto za kibajeti za kufanya utafiti wa kiwango cha kaboni kinachozalishwa kwenye viwanda nchini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, hadi Februari mwaka huu kulikuwa na jumla ya viwanda 80,976, kati yake 62,400 vikiwa vidogo sana, 17,274 vidogo, 684 vya kati na vikubwa 618.

“Hatuna bajeti na vifaa, nadhani ilitakiwa kiwepo kitengo cha utafiti wa kaboni kwenye viwanda, magari chenye bajeti ya kutosha, tunaweza kuwa na wataalamu wachache lakini tukashirikisha taasisi nyingine zenye wataalamu, kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” anasema Mulinda.

“Bila kufanya ukaguzi na utafiti katika uzalishaji wa kaboni, inakuwa changamoto kwa Serikali kufanya mabadiliko ya sheria na mipango ya muda mrefu ya kukabiliana na uzalishaji wa kaboni,” aliongeza.

Taarifa za Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), zinaeleza kuwa kati ya mwaka 1994 na 2014, kiwango cha gesijoto kinachozalishwa na sekta tano za viwanda, kilimo, nishati, ardhi na menejimenti ya taka, kilisababisha ongezeko la kaboni kutoka tani milioni 100 hadi milioni 145.

Hatua hiyo ni sawa na ongezeko la tani milioni 45 ndani ya miaka 20 au makadirio ya ongezeko la kaboni 187,500 kwa mwezi.

“Hizo ndizo takwimu za kitaifa hadi mwakani tutakapotoa ripoti mpya. Hicho kiwango kinaweza kuwa kimepanda, lakini ni vigumu kujua hali ilivyo sasa kitakwimu,” alisema Profesa Eliakimu Zahabu, mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Kaboni, kilichopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Ofisa Mazingira Mkoa wa Dar es Salaam, Valence Urassa anasema athari za mabadiliko ya tabianchi katika mkoa huo zitaendelea kuwa tishio endapo hakutakuwa na utayari wa kutii sheria na kuongezwa idadi ya wakaguzi wa mazingira.

Urassa anasema viwanda 12 tu kati ya 233 vilivyoanzishwa kati ya 2015/2019 kwenye jiji hilo ndiyo vilivyofanyiwa ukaguzi kipindi cha Novemba hadi Desemba mwaka jana kwa ngazi ya mkoa, sawa na asilimia tano.

“Tuna changamoto nyingi za ndani, mfano maofisa wachache wa ukaguzi, tulitakiwa kuwa na maofisa watatu lakini kwa sasa yupo mmoja tu, ndiyo maana tulifikia viwanda 12 tu ngazi ya mkoa wenye maelfu ya viwanda,” alisema Urassa katika mahojiano na gazeti hili.

“Lakini pia, watu wanatakiwa kutii sheria na kanuni ili kuendelea kulinda athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi,” anasema Urassa.

Kanuni zinaelekeza kuwa ukaguzi ufanyike kila baada ya miezi sita, lakini ofisi hiyo imekuwa ikikabiliwa na mkwamo wa kutotekeleza kalenda hiyo licha ya kaguzi nyingine zinazofanyika ngazi za halmashauri.

Kwa mujibu wa mwongozo wa mwaka 2021 kuhusu uwekezaji katika Mkoa wa Dar es Salaam, jiji hilo lina asilimia 43.1 ya viwanda vyote vinavyozalisha bidhaa kamili nchini, ikiwamo bidhaa za vyakula, ambavyo baadhi vinahusika kuchangia uzalishaji wa gesijoto kama ilivyoelezwa na Urassa.

Urassa anasema kati ya Novemba hadi Desemba mwaka jana, halmashauri ya Ilala ilikagua viwanda 34 kati ya 42, Temeke 17 kati ya 55, Kinondoni vinane kati ya 40, Ubungo 22 kati ya 75 na Kigamboni saba kati ya 21. Hii ni sawa na asilimia 37.7 tu ya ukaguzi wa viwanda hivyo 233 vilivyokaguliwa mwezi huo.

“Katika ukaguzi huo, asilimia 20 ya viwanda vilibainika kuchafua hewa kwa njia ya moshi na athari zake ni magonjwa ya kifua, ngozi na uharibifu wa mabati kutokana na ongezeko la kaboni.

Pia ukaguzi ulibaini asilimia karibu 50 ya uchafuzi wa njia za mfumo wa majitaka unaotishia viumbe hai,” alisema Urassa.

“Tumebaini viwanda vingi vinamwaga maji machafu kwenye mito kama Ng’ombe, Mbezi, Mzinga na Ruhanga. Kuna wakati ukipita Mto Ruhanga unakuta maji yanayotiririka ni ya rangi ya njano au kijani kutoka viwandani na tumekuwa tukiwachukulia hatua za kisheria kwa kuwatoza kati ya Sh1 milioni hadi Sh5 milioni.”

Kuhusu changamoto hizo, John Noronha, meneja ufuatiliaji na tathmini wa USAID, anasema ukosefu wa taarifa za msingi unakwamisha ubunifu wa mipango ya kukabiliana na changamoto hizo.
“Kwa hiyo inabidi wadau wajadili nini kifanyike ili tuendako tuwe na ufumbuzi.”