Prime
Chanzo ghorofa kupigwa mnada kwa mkopo wa Sh10 milioni-2
Dar es Salaam. Hii ni sehemu ya pili ya simulizi ya familia ya mfanyabiashara Johan Harald Abrahamsson kuondolewa katika nyumba ya makazi yake, yenye thamani ya Sh2.5 bilioni iliyopigwa mnada kwa sababu ya mkopo wa Sh10 milioni alioudhamini.
Nyumba hiyo iliyoko kitalu namba 16, Jangwani Beach wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, ilipigwa mnada na Exim Bank (Tanzania) Limited, kwa amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara mwaka 2017.
Takribani miaka tisa Abrahamsson amekuwa akipambana mahakamani bila mafanikio na sasa amefungua tena shauri la maombi mchanganyiko ya kibiashara namba 8901/2026 akipinga mchakato wa utekelezaji wa amri ya mahakama hiyo.
Wajibu maombi katika shauri hilo ni Exim Bank, kampuni ya Dascar Limited (mdhaminiwa wa mkopo), dalali wa Mahakama aliyeendesha mnada huo, Mas & Associates Company Limited and Court Broker na mnunuzi, Yusuph Shabani Matimbwa.
Abrahamsson anadai kuwa amri ya ukamataji na kupiga mnada nyumba hiyo ilipatikana kwa njia za udanganyifu na kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, madai na tuhuma ambazo zimekanushwa na Exim na Matimbwa, huku Exim ikibua pingamizi la awali.
Majibizano ya nyaraka baina ya pande hizo mbili, Abrahamsson dhidi ya Exim na Matimbwa na viambatanisho vilivyowasilishwa na pande zote kama vielelezo vinairejesha Mahakama kwenye chimbuko la mgogoro huo na kuibua utata wa baadhi ya mambo yanayolalamikiwa na Abrahamsson.
Katika sehemu ya kwanza kimsingi tulibainisha madai na tuhuma za Abrahamsson kuhusiana na jinsi mambo yalivyoendeshwa mpaka nyumba yake hiyo ikakamatwa na kupigwa mnada.
Katika sehemu hii ya pili tutaangalia zaidi chimbuko la mgogoro huo na yote yaliyotokea nyuma yake.
Chimbuko la mgogoro
Mwaka 2002, Abrahamsson aliidhamini kampuni ya Dascar Limited kupata mkopo huo wa Sh10 milioni, kwa dhamana ya hati na ahadi ya yeye kuulipa mkopo huo iwapo wakopaji wangeshindwa.
Mpaka mwaka 2008, Dascar haikuwa imelipa mkopo huo.
Hivyo Exim ilifungua kesi ya kibiashara namba 51/2008, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara dhidi ya Dascar (mkopaji) na Abrahamsson (mdhamini), ikidai ilipwe Sh40,063,788.00 (zaidi ya Sh40 milioni), yaani mkopo Sh10 milioni, riba na adhabu Sh30,063,788.00 (zaidi ya Sh30 milioni).
Katika hati ya madai Exim iliomba mdhamini, Abrahamsson alipe kiasi cha mkopo alioudhamini, Sh10 milioni na mkopaji Dascar alipe riba na adhabu Sh30 milioni.
Wakati wa usuluhishi, Abrahamsson alilipa mkopo wote aliokuwa ameudhamini.
Hata hivyo, kesi iliendelea na Mahakama katika hukumu yake Agosti 11, 2009 iliyotolewa na Jaji Fredrick Werema, ilisema kwa kuwa Abrahamsson alishatekeleza wajibu wake Exim haina madai tena dhidi ya Abramsson.
Exim ilikata rufaa namba 92/2009, Mahakama ya Rufani, ambayo katika hukumu yake Februari 24, 2016, iliipa ushindi Exim, huku ikisema kuwa mdhamini ana wajibu sawa na mkopaji, kulipa deni la msingi, riba, adhabu na gharama nyinginezo kulingana na mkataba wa mkopo.
Hivyo Exim, ilirudi Mahakama ya Biashara ambako aliomba utekelezaji wa hukumu hiyo, huku akidai kuwa wakati huo deni lilikuwa limeshafikia Sh113,489,432.00 ( zaidi ya Sh113.4 milioni).
Hata hivyo, katika utekelezaji wa hukumu hiyo, Exim ilimbebesha mdhamini, Abrahamsson pekee mzigo wote wa deni hilo, ambapo iliomba amri ya kukamata na kupiga mnada nyumba hiyo.
Abrahamsson kupitia wakili wake Fatma Karume alipinga maombi hayo akieleza kuwa nyumba hiyo haikuwa imewekwa rehani kama dhamana ya mkopo huo, hivyo kisheria haiwezi kukamatwa na kupigwa mnada.
Pia wakili Karume alieleza kuwa nyumba hiyo ni ya makazi ya familia ambayo kisheria haipaswi kukamatwa na kupigwa mnada.
Mke wa Abrahamsson, Jacquiline Donath Kweka pia alifungua mashauri mbalimbali kupinga kuuzwa nyumba hiyo.
Alieleza kuwa nyumba hiyo ilipatikana na kumilikiwa kwa pamoja kama wanandoa na ni makazi ya familia ambamo wamekuwa wakiishi wao na watoto wao wawili tangu mwaka 1999.
Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Amir Mruma Oktoba 27, 2017, ilitupilia mbali pingamizi hilo ikieleza kuwa mwombaji hakuweza kuthibitisha kama nyumba hiyo ni ya makazi.
Hivyo Novemba 29, 2017 Mahakama hiyo iliridhia maombi ya kukamatwa na kupigwa mnada nyumba hiyo na ikamteua dalali Mas & Associates kutekeleza amri hiyo.
Kufuatia amri hiyo Jacquiline alifungua shauri la maombi dhidi ya Exim na dalali huyo, akipinga uamuzi huo wa kukamatwa na kupigwa mnada nyumba hiyo.
Pia Desemba 15, 2017 aliomba na akapata amri ya mahakama ya kusimamisha kwa muda mnada wa nyumba hiyo na pande zote zilitakiwa kufika mahakamani Desemba 18, 2017.
Siku hiyohiyo Jacquiline alimpatia dalali huyo amri ya zuio la muda la mnada huo, pamoja na hati ya wito wa kufika mahakamani.
Hata hivyo, Desemba 18, 2017 dalali aliieleza mahakama kuwa tayari alikuwa ameshauza nyumba hiyo kwa mnada tangu jana yake, Desemba 17, 2017 kwa Matimbwa kwa bei ya Sh300 milioni.
Licha ya dalali huyo kupuuza amri hiyo ya mahakama, mahakama hiyo iliamua kuondoa amri yake hiyo ya zuio, na baadaye ikalitupilia mbali shauri hilo.
Jacquline aliendelea kufungua mahakamani hapo mashauri mengine mbalimbali kupinga uuzwaji wa nyumba hiyo lakini yote yalitupiliwa mbali, mengi bila kusikilizwa madai yake ya msingi bali kutokana na mapingamizi ya walalamikiwa.
Mwaka 2023 Matimbwa (mnunuzi) alifungua shauri la maombi namba 117/2023 akiomba amri ya Mahakama kuwaondoa wakazi wa nyumba hiyo na kumkabidhi yeye.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Cyprian Mkeha Machi 25, 2024, iliamuru Abrahamsson aondolewe katika nyumba yao na ikabidhiwe kwake Matimbwa.
Abrahamsson alikata rufaa Mahakama ya Rufani, rufaa namba 306/2024, akipinga uamuzi na amri ya kuondolewa ndani ya nyumba, lakini Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza katika hukumu yake Desemba 8, 2025, ilitupilia mbali rufaa hiyo.
Hivyo Matimbwa kupitia dalali wa Mahakama Accurate Recovery and Auction Limited, aliiandikia barua Mahakama Kuu akiomba amri ya kuendelea na hatua ya kuwaondoa wakazi wa nyumba hiyo na kukabidhiwa.
Machi 27, 2026 Mahakama ya Biashara ilitoa notisi iliyosainiwa na Naibu Msajili, Suzan Kihawa ikiamuru watu waliokuwa wanaishi humo kuondoka ndani ya siku 14 kabla ya kuondolewa kwa nguvu.
Hata hivyo dalali huyo alikaa na notisi hiyo mpaka ikabakia siku moja ndipo akaenda kuibandika katika nyumba hiyo Aprili 9, 2026.
Siku iliyofuata, Aprili 10, 2026, dalali huyo akiwa na kundi la wafanya mazoezi ya kunyanyua vitu vizito, maarufu mabaunsa walivamia nyumba hiyo wakati hakuna mtu yeyote nyumbani hapo.
Hivyo walivunja geti wakaingia na wakachukua kila kitu cha familia hiyo kilichokiwemo ndani na kuondoka navyo na kuweka ulinzi kuzuia mwanafamilia hiyo yoyote kuingia tena humo ndani.
Itaendelea kesho