Chongolo aridhishwa maboresho Bandari ya Tanga

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema uboreshaji unaofanywa na Serikali katika Bandari ya Tanga utasaidia kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya usafiri wa majini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Tanga. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema uboreshaji unaofanywa na Serikali katika Bandari ya Tanga utasaidia kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya usafiri wa majini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Chongolo ameyasema hayo leo Ijumaa, Agosti 12, 2022 wakati alipofika katika bandari hiyo ili kujionea ujenzi wa upanuzi wa gati ambao umekamilika kwa asilimia 90.

Amesema Bandari ya Tanga ndiyo bandari pekee ambayo ipo katikati ya Dar es Salaam na ya nchi jirani ya Kenya ambayo ni Bandari ya Mombasa hivyo ina fursa ya kuhudumia ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema  wanaopewa dhamana ya usimamizi na utekezaji katika utoaji huduma wa bandari hiyo kuhakikisha wanatoa huduma zenye ubora wa kimataifa ili kuweza kuketa tija .

"Miradi hii inagharimu fedha nyingi za Serikali, sasa ninyi mlioaminiwa muhakikishe thamani ya mradi huu inaendana na ubora katika utoaji huduma tunataka matokeo chanya," amebainisha Chongolo.

Aidha, maboresho yanayofanywa kwenye bandari hiyo ni kuongeza kina ujenzi wa gati ambao ulianza rasmi mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.

Pia amesema kukamilika kwa mradi huo kukafungue fursa kwa wakazi wa Tanga wapate kipaumbele katika fursa za ajira za muda ambazo za kutumia nguvu ili waweze kufaidika.

"Itapendeza na kuleta tija kwa vijana wa Tanga nao wanufaike na mradi huu wapate hata zile kazi za kutumia nguvu hii itawanufaisha vijana wetu kiuchumi lakini pia wataona umuhimu wa uwepo wa miradi hii," amesema

Awali, akisoma taarifa Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha alisema ujenzi umekamilika kwa asilimia 90 na kwamba utakamilika Novemba mwaka huu.

Mrisha amesema mradi huo utakapokamilika wanatarajia bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kupokea tani milioni tatu kwa mwaka ukitofautisha na sasa ina uwezo wa kuhudumia tani 700.18.

"Kabla ya maboresho uwezo wa kupokea shehena ulikuwa tani 700.18 kwa mwaka hivyo tutakapokamilisha tija itakuwa kubwa zaidi " amesema Mrisha.

Kwa upande wake, Katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga amepongeza jitihada za Serikali katika uboreshaji wa mradi huo.

"Nimefurahishwa na maboresho haya, lakini Watanzania na watu wa Tanga wanahitaji uhakika wa upatikanaji wa vyanzo vya mapato ambayo yatakwenda kuwatatuliza changamoto za kimaendeleo katika maeneo hayo," amesema  Lubinga.