Chongolo: Wizara zote zianishe matumizi fedha za IMF

Chongolo: Wizara zote zianishe matumizi fedha za IMF

Muktasari:

  • Katibu mkuu CCM ameziagiza wizara zote zilizopokea fedha za mkopo kutoka IMF kutoa mchanganuo wa matumizi ili wananchi wajue namna zitakavyowanufaisha kwenye maeneo yao.

 Arusha. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameziagiza wizara zote zilizopokea mgao wa fedha za mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kutoa mchanganuo wa matumizi kama ilovyofanya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa mwenyekiti wa chama hicho ambaye ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan  katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Chongolo amesema kuchanganua matumizi ya fedha hizo kutaonyesha uwazi kwa wananchi.

"Nampongeza sana Waziri wa Tamisemi (Ummy Mwalimu), amefanya mchanganuo wa matumizi ya fedha zote, wizara nyingine nazo zifanye hivyo," amesema Chongolo.

Chongolo pia amezitaka kamati za siasa za mikoa na wilaya kufatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa katika maeneo yao kwani zikipotea watawajibika.

"Kama fedha zitapotea ina maana mtakuwa hamjawajibika," ametahadharisha katibu mkuu huyo wa chama tawala.

Awali, Chongolo alisema CCM imeridhishwa na utendaji wa Rais Samia kwani ndani ya miezi saba ametekeleza vyema ilani na kufanya mambo makubwa.