Chuo cha uhasbu Arusha kuikabili mikopo ‘kausha damu’

Mkuu wa Chuo cha IAA Profesa Eliamani Sedoyeka akiwa kwenye banda la chuo hicho kwenye maonyesho ya vyuo vikuu yanayofanyika Mnazi mmoja Dar es Salaam
Muktasari:
- Chuo cha Uhasibu Arusha (AIA) kimesema kina mpango wa kuanzisha programu mpya ya mafunzo ya fedha na mikopo kwa kundi la wanawake wajasiriamali na waendesha bodaboda, lengo likiwa ni kuwaepusha na mikopo ‘kausha damu’.
Dar es Salaam. Kufuatia utitiri wa taasisi na kampuni na watu binafsi kujihusisha na utoaji wa mikopo kwa wananchi kinyume cha sheria, Chuo cha Uhasibu Arusha (AIA) kimesema kina mpango wa kuanzisha programu mpya ya mafunzo ya fedha na mikopo kwa kundi la wanawake wajasiriamali na waendesha bodaboda.Programu hiyo italenga kuwafuata wajasiriamali hao katika maeneo yao ya kazi na kuwapa elimu juu ya eneo sahihi kwa kukopa na namna ya kutumia mikopo hiyo ili kuepukana na athari zitokanazo na mikopo yenye riba na masharti ambayo siyo rafiki kwa mkopaji maalufu kama ‘kausha damu.’Aina ya mikopo inayosemwa na AIA ni ile inayosababisha maumivu kwa wakopaji wakati wa marejesho, ambapo baadhi ya taasisi zimekuwa zikitoa masharti magumu ikiwamo kutaifisha mali hasa nyumba, magari na samani za ndani endapo mhusika atashindwa kulipa kwa wakati.Hayo yameelezwa leo Julai 20,2023 na Mkuu wa AIA Profesa Eliamani Sedoyeka kwenye maonesho ya 18 ya vyuo vikuu nchini, yaliyoratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU); yakiwa na kaulimbiu "Kukuza ujuzi nchini kupitia elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia kwa uchumi imara na shindani”.AIA tuna wajibu wa kuielimisha umma faida mbalimbali za mikopo na kuwa makini kabla ya kuchukua mikopo, kupitia mchango wetu kwa jamii tumekuwa tukitoa walimu wa shule ya msingi na sekondari wenye ujuzi wa masuala ya usimamizi wa fedha na mikopo na tupo mbioni kuanzisha programu kwa makundi mbalimbali ya jamii kuwaelimisha masuala ya mikopo.Amesema wengi wa wakopoaji wa mikopo hiyo wanaona ina faida lakini kitaalamu mikopo hiyo inaumiza hivyo mafunzo yao wanalenga kuwafungua wananchi kuhusu athari ya mikopo hiyo.Juni mwaka huu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia kwa Gavana wake Emmanuel Tutuba ilipiga marufuku taasisi, kampuni na mtu binafsi wasio na leseni kufanya biashara ya kukopesha watu fedha.Tutuba kupitia taarifa yake amesema kwa watakaokiuka katazo hilo hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo cha miaka miwili jela.Katazo hilo la BoT lilizingatia kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 ambazo inatoa katazo hilo.Katika hatua nyinge Profesa Sedoyeka amesema chuo hicho kimeanzisha kozi za shahada ya kwanza kwa kwanafunzi wa fani ya usimamizi na utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa fedha, uandishi na utangazaji wa habari kupitia teknolojia za kisasa.Maonyesho ya 18 ya Vyuo Vikuu vimeanza Julai17 na tamati ni Julai 22 huku zaidi ya vyuo na taasisi 80 zikishiriki.