CPJ yazindua kampeni kumsaka Azory Gwanda
Muktasari:
- Mwandishi wa kujitegemea kwa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda kesho atafikisha siku 500 tangu atoweke, huku Kamati ya Kuwalinda Wanahabari (CPJ) ikizindua kampeni kutaka kujua alipo
Dar es salaam. Wakati kesho zikitimia siku 500 tangu mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda atoweke, Kamati ya Kuwalinda Wanahabari (CPJ) imezindua kampeni mitandaoni inayotaka kujua aliko mwandishi huyo.
Kampeni hiyo imepewa jina la #WhereIsAzorykukumbushia. Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, lengo kubwa la kampeni hiyo ni kuhamasisha, kujenga uelewa kuhusu mwandishi huyo na kuzitaka mamlaka za Tanzania kufanya uchunguzi wa kuaminika na kuweka bayana hatma yake.
“Watu wanaweza kushiriki katika kampeni kwa kutumia hashtag #WhereIsAzoryna #MrudisheniAzory katika mitandao ya kijamii,” mesema Angela Quintal, mratibu wa CPJ Afrika.
CPJ imesema waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini wanachukua tahadhari kwa kuhofia yanayoweza kuwakuta kama Azory.
“CPJ Afrika itaangazia kesi ya Azory katika twitter, facebook na instagram. CPJ ni kamati huru isiyojiendesha kwa faida inayofanya kazi kulinda uhuru wa wanahabari duniani,” imesema taarifa hiyo.
Azory alitekwa na watu wasiojulikana Novemba 21, 2017 huku nyuma akiwa ameacha huzuni na hofu kubwa kwa familia na tasnia ya habari aliyokuwa akiifanyia kazi kabla ya kukumbwa na mkasa huo.
Novemba mwaka jana CPJ ilitoa wito mwingine ikisema ni muhimu uchunguzi kuhusu kupotea kwa Azory ukafanyika kwa kina na umma ufahamishwe.
Ilisema ingawa maofisa wa Serikali ya Tanzania waliahidi kufanya uchunguzi wa tukio hilo lakini mpaka sasa hakuna taarifa zaidi kuhusu mkasa huo.
"Kukosekana kwa uchunguzi wa kuaminika juu ya kupotea kwa mwandishi wa habari Azory Gwanda ni jambo linalosikitisha na kuvunja moyo na linaakisi namna tunavyoguswa kuhusu mazingira ya uhuru wa vyombo vya habari Tanzania,” alisema Quintal.