CRDB inampa diaspora uzoefu wa huduma kama nyumbani

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi (katikati) akiwa na maafisa wa Benki ya CRDB walipotembelea ofisi za ubalozi jijini Frankfurt. Benki ya CRDB kupitia kitengo cha Diaspora imefanya ziara ya wiki mbili kutembelea Watanzania wanaoishi barani Ulaya kuwaeleza juu ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nyumbani.

Muktasari:

Kama kuna kitu kinachowaumiza vichwa wafanyabiashara wengi basi ni kuhudumia kundi la watu/raia wanaoishi nje ya mipaka ya nchi zao (Diaspora).

Kama kuna kitu kinachowaumiza vichwa wafanyabiashara wengi basi ni kuhudumia kundi la watu/raia wanaoishi nje ya mipaka ya nchi zao (Diaspora).

Kwa miongo mingi, jiografia imekuwa miongoni mwa sababu nyeti zinazokwamisha jitihada hizi za jumuiya ya wafanyabiashara kulifikia kundi hili.

Diaspora ni raia walioamua kwenda kutafuta mkate wao nje ya mipaka ya nchi zao wakiziacha familia zao pendwa ili baadaye waweze kuzikwamua kiuchumi.

Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya diaspora wapatao Milioni 2 duniani kote. Kundi hilo lina mchango sawa na Watanzania wengine wanaoishi nchini katika maendeleo ya Taifa licha ya jamii kuwatazama kwa sura tofauti.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alisema kuwa mchango wa diaspora nchini umeendelea kuongezeka siku hadi siku.

Alisema kuwa kulingana na takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) fedha zilizotumwa nchini (remittance) na kundi hilo zimeongezeka kutoka katika Dola za Marekani takriban Milioni 400 mwaka 2020 hadi kufikia Dola za Marekani Milioni 569 kwa mwaka 2021.

Hivyo, kama wana mchango mkubwa katika uchumi na maendeleo ya Taifa kiasi hiki kwanini wapate shida tena ya kufikiria namna gani ya kuwatumia fedha wapendwa wao walioko nchini, washindwe kujenga kwao au kuwanunualia watu bidhaa au zawadi?

Na ndiyo maana, Benki ya CRDB ikaamua kuiona fursa ya diaspora kwa kubuni huduma ya kibenki kuhudumia kundi hilo ikiliunganisha na familia zao moja kwa moja.

Kaimu Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa anasema kuwa kama benki, wamekuwa wakijitahidi kutengeneza huduma bunifu, rafiki na bora ambazo zinakidhi mahitaji mbalimbali ya wateja ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa muda mrefu.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Edmund Kitokezi (wa pili kutoka kulia) akiwa na maafisa wa Benki ya CRDB walipotembelea ofisi za ubalozi jijini Stockholm. Benki ya CRDB kupitia kitengo cha Diaspora imefanya ziara ya wiki mbili kutembelea Watanzania wanaoishi barani Ulaya kuwaeleza juu ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nyumbani.

Anasema kwa upande wa diaspora, benki ilikaa na kuanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya wateja wanao-ishi nje ya mipaka ya Tanzania mwaka 2014 ikiwa na lengo la kuhakikisha diaspora wanapata huduma sawia na wale waliopo nchini.

“Kulikuwa na mtu ambaye alikuwa anafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alipata ufadhili wa masomo katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani, na mshahara wake ulikuwa unaingia moja kwa moja kupitia Benki ya CRDB Plc. Hivyo tulikuwa tunawaza namna gani tunamwezesha mtu kama huyo kupata huduma za fedha kama vile yuko nyumbani Hapa Tanzania,” anaeleza Raballa.

Anafafanua kuwa walianzisha huduma ya kibenki ya diaspora (diaspora banking) ikianza kama dawati na baadaye kuitanua zaidi kwa kuanzisha akaunti maalum ya Tanzanite.

Raballa anakiri kuwa baada ya muda waliamua kutanua wigo wa huduma hiyo kwa kuwezesha wateja hao kutumia fedha za aina nne duniani za Dola ya Marekani, Paundi, Euro na Shilingi pale wanapokuwa katika nchi za Ulaya, Uingereza, Amerika au hata zile zinazotumia Shilingi kwa Afrika.

“Watanzania sasa kupitia akaunti hiyo wanaweza kuwekeza na kutuma fedha ndani ya nchi yao kwa kutumia fedha hizo kubwa duniani,” anaongeza zaidi.

Raballa anasema tangu kuanzishwa kwa akaunti ya Tanzanite wateja waliojiunga na akaunti hiyo ni zaidi ya 30,000 (wakifungua kwa fedha za aina mbalimbali). Bado benki inaendelea kuona ukuaji wa akaunti hiyo kutokana na ukweli kwamba inazidi kupokea maombi ya diaspora kujiunga na huduma hiyo.

Faida ya akaunti ya Tanzanite kwa Benki, Taifa na Diaspora

Kwa upande wa Taifa, anasema diaspora wanapofanya kazi nje ya nchi na kisha kupata kipato, wanapotuma fedha hizo nyumbani huhesabiwa kama fedha zilizotoka nje ya nchi (remittance) na huchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa.

“Na kuchangia huko katika pato la Taifa kunaambatana na Serikali kupata kodi kupitia makato ya uendeshaji wa akaunti kama hizi za Tanzanite.” anaeleza Raballa.

Anaendelea kusema kuwa kwa upande wa Benki ya CRDB Plc inapata wateja na kupitia mikopo ambayo diaspora wanachukua ikiwamo ile ya ununuzi wa nyumba, ujenzi na mingine mingi benki imekuwa ikiongeza vyanzo vya mapato.

Raballa anaeleza kuwa moja ya malengo ya kimsingi ya benki ni kuhakikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanapata huduma za kibenki bila ya usumbufu na wanamudu kusaidia familia zao sambamba na kushiriki katika matukio mbalimbali ya familia.

Na hilo kulingana na Raballa, limefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa diaspora mwenyewe, kupitia huduma za diaspora za benki yetu, anakuwa anaweza kuwekeza ili baadaye apate faida kubwa au kujenga au kununua nyumba.

Pia, diaspora anapata fursa ya kuweka akiba fedha zake katika akaunti ya Tanzanite kupitia majukwaa ya kimataifa ya uhamishaji fedha ya Western Union, Ria Financials na World Remit ambayo yamein-gia makubaliano na benki hiyo.

Kama hiyo haitoshi, diaspora anapojiunga tu basi hupata ulinzi wa moja kwa moja wa bima maalum ya KAVA assurance ili kumkinga yeye na mwenza wake/ familia yake pale anapopata majanga yasiyotegemewa.

Diaspora pia mwenye akaunti hii anaunganishwa moja kwa moja na huduma ya benki mtandao (Internet Banking) ambapo anaweza kufanya miamala yote mtandaoni hii ni pamoja na kufanya malipo ya Serikali (kodi mbalimbali).

Yanapotokea majanga ya msiba kwa Diaspora aliye na akaunti ya Tanzanite ughaibuni, pale ambapo hati ya madai inapowasilishwa kwa benki kutoka kwa kampuni itakayousafirisha mwili, Benki ya CRDB Plc itagharamia kiasi cha Sh15 milioni na kuhakikisha mwili unafika Tanzania kwa familia yake.

Mbali na hilo, kwa kuwa mwili hauwezi kuja wenyewe, Benki itahusika na kugharamia ndugu mmoja aliyeko ughaibuni kuja nchini kushiriki maziko ya mpendwa wake kwa kulipiwa tiketi ya kwenda na kurudi.

Haishii hapo, baada ya mwili kufika nyumbani familia lazima iwe imetenga bajeti ya mazishi, na hapa benki hiyo inagharamia kiasi cha Sh5 milioni kama mkono wa pole kwa familia ya marehemu ili waweze kumsitiri mpendwa wao bila ya wasiwasi wowote.

“Jambo lingine ni kwamba mteja huyu bado ana fursa ya kununua muda wa maongezi. Anakabidhiwa TemboCard Visa Gold ambayo inamwezesha kufanya miamala katika benki yoyote ile kule alipo. Kingine ni kwamba mteja huyu anakabidhiwa Meneja Mahusiano maalumu ambaye atakuwa anawasiliana naye kwa ajili ya kusaidiwa mambo mbalim-bali yanayohusu huduma hiyo akiwa ughaibuni,” anaeleza.

Vigezo vya kujiunga na akaunti ya Tanzanite

Raballa anasema ili diaspora aweze kujiunga masharti yake ni rahisi kwani anahitajika kuwa na passport (bayometriki) au kitambulisho cha Nida, Kibali cha Makazi au VISA au kuorodheshwa katika kundi la diaspora wanaoishi katika nchi fulani, au uthibitisho wa hati ya malipo ya gharama za umeme na maji.

Upanuzi wa Benki ya CRDB barani Afrika

Raballa anasema si kama benki hiyo imeridhika na uwepo wake katika nchi mbili pekee za ukanda wa Afrika Mashariki (Tanzania na Burundi) bali ipo katika kufanya tafiti zitakazowezesha benki hiyo kukidhi matakwa halisi ya eneo husika kama vile walivyofanya wakati wanaingia Burundi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela na Katibu Mkuu Wizara la Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, wakitia saini hati ya makubaliano baina ya Benki ya CRDB na Wizara kwa ajili ya utengenezaji wa mfumo wa kidigitali kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora).

“Ili uweze kusonga mbele lazima ukubali mabadiliko pia upokee mawazo kutoka kwa wale wanaotumia bidhaa/huduma zako. Kwa hiyo kabla ya kuingia katika nchi nyingine, kuna upembuzi yakinifu ambao tumekuwa tukiufanya ili kuifanya biashara yetu izidi kustawi katika mazingira ya nje ya mipaka ya Tanzania,” anasema Raballa.

Anasema kwa sasa benki ipo katika mikakati ya kuingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikianzia na Lubumbashi baada ya upembuzi yakinifu wa benki kujiridhisha kuwa ni eneo sahihi kutokana na mwingiliano mkubwa wa nchi hizo.

“Tunafahamu kuwa Kongo ni nchi isiyo na bandari na ina wafanyabiashara wake wengi nchini wanafanya biashara kupitia bandari ya Dar es Salaam kuchukua mizigo kwa ajili ya kwenda kuuza nchini kwao. Hivyo, ni eneo linalohitaji msaada wa taasisi ya fedha itakayorahisisha mzunguko wa biashara kupitia ununuzi.”

Hivyo anakiri kuwa benki bado inaendelea kufanya utafiti wa nchi nyingine za Afrika na inaamini hata ndani ya nchi hizo kuna Watanzania ambao wanahitaji huduma kama hizo.

Mikakati iliyopo kwa ajili ya diaspora

Raballa anasema benki haiwezi kulala bado iko macho kuendelea kuboresha ustawi wa diaspora wa Tanzania wanaoishi ughaibuni.

Na moja ya mikakati yake ni huduma ya Mzigo Flexi ambayo ni mahsusi kwa Watanzania wanaotaka kuwekeza na kupata faida lakini hawawezi kuwekeza katika biashara wanazoweza kusimamia na badala yake hutafuta watu wengine kuwasaidia.

Ndani ya huduma hii, mteja anawekeza kwa miaka mitatu na kupata riba ya asilimia tisa kila mwaka (kwa miaka mitatu akikusanya riba ya asilimia 27).

Kampeni hii imeanza Mei 17. Kwa mteja wa diaspora anaweza kuwekeza kuanzia kiasi cha Sh1 milioni na kuvuna faida ya asilimia 9 kwa miaka mitatu.

“Tunaendelea na michakato ya ndani ya benki ya kuhakikisha diaspora wanaendelea kujihudumia wenyewe kwa kubuni majukwaa mbalimbali ya kidijitali,” anaeleza.

Matarajio ya benki katika ajenda ya diaspora

“Ndugu mwandishi niseme kuwa kutokana na takwimu za Serikali, idadi ya diaspora walioko ughaibuni ni takriban milioni 2, sisi kama benki kinara ambao tumekuwa katika soko kwa muda mrefu tumefanikiwa kufikia diaspora zaidi ya 30,000, bado tuna kazi ya kufanya ya kufikia milioni 1 na pointi tisa ambapo inatulazimu kuendelea kupiga kelele nyingi kuhusiana na umuhimu wa akaunti ya Tanzanite ambayo ni mahsusi kwa diaspora,” anabainisha Raballa.

Baadhi ya watoto wanaoishi nje ya nchi wanaofaidika na huduma ya Diaspora ya Benki ya CRDB

Anasema mbali na hilo, matarajio ya benki ni kuona namna gani wanawafahamu diaspora kwa undani. Anasema diaspora waliopo ughaibuni wanatofautiana fani/sekta hivyo ingewapendeza kama watajua mahitaji halisi ya wahandisi, madaktari, wanafunzi, wanamichezo, walimu, wachimbaji madini, wajasiriamali ili watoe masuluhisho yenye kukidhi makundi ya kitaaluma.

Tathmini ya Janga la Uviko-19

Raballa anasema kuwa licha ya dunia kuathiriwa na janga hilo, na CRDB ikiwa ni sehemu ya dunia hiyo, lakini uendeshaji wa huduma za kibenki za diaspora ziliendelea vizuri kupitia mifumo yake bunifu ya benki mtandao ikichagizwa na Mkakati wake thabiti wa Usimamizi wa Uendelevu wa Biashara (Business Continuity Management).

Maoni ya benki

Raballa anasema benki inashukuru jumuiya ya diaspora kwa kuendelea kutumia huduma za CRDB na benki hiyo itaendelea kuja na mikakati mingi ya kuwawezesha kustawi.