CRDB yataja siri ya kutwa tuzo ya benki bora Tanzania

Muktasari:

Baada ya CRDB kutunukiwa tuzo ya beki bora nchini, Mkurugenzi wake, Abdulmajid Nsekela amesema mageuzi ya kibiashara ni miongoni mwa chachu za mafanikio hayo.

Dar es Salaam. Wiki moja baada ya kutunukiwa tuzo ya benki bora Tanzania, Benki ya CRDB imesema mageuzi ya kijigitali na kibiashara yaliyojikita katika kutengeneza thamani endelevu ni sehemu ya chachu ya ushindi huo.

CRDB ilitunukiwa tuzo hiyo Julai 13, 2022 na jarida maarafu la masuala ya fedha na uchumi la nchini Uingereza, Euromoney.

Akizungumza leo, Julai 20, 2022 wakati wa shukrani baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela amesema mageuzi hayo yalianza kufanyika mwaka 2019.

“Mwaka 2019, Benki hiyo ilianza ikifanya mageuzi katika biashara yake ambayo yamejikita katika kutengeneza thamani endelevu, kuongeza ujumuishi wa kifedha na kujenga uchumi jumuishi kupitia bidhaa, huduma, na mifumo bunifu ya utoaji huduma,” amesema.

Amesema tuzo hiyo ni uthibitisho wa nafasi ya benki hiyo na mageuzi yaliyosababisha ukuaji wake na kunufaisha wateja wake na taifa kwa ujumla.

Ameeleza kuwa waandaji wa tuzo hiyo wametambua mchango wa mageuzi wa kidijitali yaliyofanyika na kusaidia kuchochea ongezeko la ujumuishi wa kifedha nchini.

“Tumekuwa pia tukishiriki kikamilifu katika kusaidia sekta mbalimbali za maendeleo nchini hususani kilimo, na ujusariliamali ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu,” aliongezea.

Kwa mujibu wa Nsekela, CRDB imetambuliwa kwa kuwa na uwezo katika uwezeshaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali na sekta binafsi akitolea mfano Mradi wa Umeme wa Maji wa Nyerere (JHPP) na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Mbali na Julai 13, benki hiyo iliwahi kutunukiwa tuzo hiyo mwaka 2004.

Pamoja na tuzo hiyo, mwaka jana CRDB ilitajwa kama benki bora Tanzania na inayoongoza kwa ubunifu na jarida maarufu duniani la masuala ya fedha la Global Finance, huku Taasisi ya Utafiti wa ubora Ulaya ikiitunikia tuzo ya ubora.