CRDB yatenga Sh700 bilioni kuwakopesha wajasiriamali

Muktasari:

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abdalla Hussein Kombo amebainisha kuwa, sekta ya ujasiriamali inachangia asilimia 33 kwenye pato la Taifa (GDP), sawa na theluthi moja, zinachangiwa na biashara ndogo.

Dar es Salaam. Serikali imeipongeza Benki ya CRDB kwa kukusanya zaidi ya Sh700 bilioni za kuwakopesha wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini katika maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani (World MSME Day).

Pongezi hizo zimetolewaleo Juni 27 na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abdalla Hussein Kombo aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo akisema jitihada zinazofanywa na benki hiyo zinaonyesha dhamira ya dhati iliyonayo katika kuchochea sekta ya ujasiriamali nchini.

“Takwimu zinaonyesha ni asilimia 96 ya biashara nchini ni biashara ndogo na za kati, ambapo watu milioni 24 wameajiriwa katika sekta hii.

“Hivyo jitihada hizi zinazofanywa na Benki ya CRDB ni muhimu sana katika kuboresha sekta hii ambayo inatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu,” amesema Kombo.

Waziri Kombo amebainisha kuwa, sekta ya ujasiriamali inachangia asilimia 33 kwenye pato la Taifa (GDP), ikimaanisha kuwa, katika kila Sh100 basi Sh33 ambazo ni sawa na theluthi moja, zinachangiwa na biashara ndogo.

Kwa upande wa Zanzibar, Waziri Kombo amesema Serikali inajivunia ushirikiano na Benki ya CRDB kupitia programu ya “Inuka na Uchumi wa Bluu” kuwainua wajasiriamaili kwa kutenga Sh60 bilioni.

Amesema programu hiyo ambayo inatoa ufadhili wa mitaji kwa wajasiriamali bila riba inatajwa kuwa moja ya programu bunifu zenye msukumo mkubwa wa kuwainua wajasiriamali nchini.

“Wizara yangu ni miongoni mwa sekta zilizonufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya CRDB kupitia programu ya Inuka, kwani imetengewa Sh36.5 bilioni kila mwaka kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo wanaojihusisha na fursa zilizopo kwenye uchumiwa buluu,” amesema.

Awali, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema wanatambua na kuthamini shughuli za kijasiriamali katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla jambo ambalo limeifanya benki hiyo kushirikiana na wadau ndani na nje ya nchi.

“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wakati dunia ikishuhudia misukosuko ya kiuchumi iliyochangiwa na janga la UVIKO-19 na vita vya Ukraine, Benki yetu kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa ilikusanya zaidi ya Sh 700 bilioni ambazo zinaendelea kusaidia biashara za wajasiriamali ambazo nyingi ziliziathirika kwa kiasi kikubwa,” amesema Raballa.

Katika kipindi hicho, Raballa amesema wameshirikiana na wadau wa ndani na kimataifa likiwamo Shirika la Fedha la Ufaransa Proparco, Shirika la Fedha Kimataifa (IFC), Mashirika ya Marekani ya Maendeleo ya Kimataifa USAID na DFC, Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), na Mfuko wa Dhamana Afrika (AGF) kukusanya kiasi hicho cha fedha.

 “Najivunia kuwajulisha kuwa kupitia jitihada hizi, Benki yetu imekuwa kinara katika kuwawezesha wajasiriamali kwani hadi Mei 2023 tulikuwa tumetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh3.4 trilioni kwa wajasiriamali zaidi ya 200,000, na wengine zaidi ya 50,000 wakinufaika kwa mafunzo tuliyoyatoa,” amesema Raballa.

Raballa amesema hivi karibuni Benki ya CRDB kupitia Taasisi yake ya CRDB Bank Foundation imeendelea kupanua wigo wa kuwainua wajasiriamali wadogo kupitia

programu endelevu ya “IMBEJU” inayolenga kufanya uwezeshaji wa biashara changa na wajasiriamali vijana na wanawake kupitia mafunzo, ushauri, na mitaji wezeshi.

Akizungumza kwenye mjadala wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza ameipongeza benki hiyo kwa uwezeshaji wa wajasiriamali wanawake kupitia CRDB Malkia inayojumuisha akaunti ya Malkia na Mikopo maalum ya wanawake ijulikanayo kama WAFI (Women Access to Finance Initiatives).

Amebainisha kuwa wanawake wajasiriamali wamenufaika na Sh700 bilioni zilizokusanywa na Benki ya CRDB kusaidia wajasiriamali baada ya changamoto za janga la UVIKO-19.

“Benki ya CRDB ni miongoni mwa wadau wetu muhimu kwani, licha ya kutukopesha ili nasi tuwawezeshe wanachama wetu, wao ni walezi wazuri,” amesema Mwajuma.