Daladala 15 zaitwa kuongezea nguvu ‘mwendokasi’

Dar es Salaam. Ni kupunguza tatizo la usafiri kwa abiria wanautumia usafiri wa umma Barabara ya Morogoro.

Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra), kukubali kusajili kwa muda daladala 15 kusafirisha abiria katika barabara hiyo ya Morogoro.

Daladala hizo ambazo zinatakiwa ziwe na uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25, zitakuwa zikifanya safari zake Mbezi Luis kwenda Makumbusho kupitia Barabara ya Morogoro.

Katika ruti hiyo, zitapita Manzese, Barabara ya Kawawa kisha kuelekea Mwananyamala.

Ikumbukwe tangu mradi wa mabasi Yaendayo Haraka ‘mwendokasi’ uanze  rasmi mwaka 2016, daladala ambazo zilikuwa zikifanya safari zake hadi Mbezi zilisitishwa.

Maamuzi haya yanatolewa ikiwa ni wiki moja tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila atembelee Kituo cha mabasi ya 'mwendokasi' cha Kimara ambacho kilikuwa na changamoto ya msongamano wa abiria huku magari hayo yakiwa machache.

Katika ziara ya RC Chalamila baadhi ya maoni ya wananchi aliyoyakusanya mengi yalihusu kuwapo kwa mshindani katika barabara ambayo magari ya 'mwendokasi' pekee yanapita.

Hata hivyo, kutokana na changamoto za usafiri huo wa mwendokasi unaosababisha abiria kukaa vituoni muda mrefu, abiria wamekuwa wakitumia usafiri wa kukodi wa bajaji au bodaboda ambao nauli yake ni kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), mkoa wa Dar es Salaam, Rahim Kondo alisema ujio wa daladala huo ni moja ya sababu ya kutaka kupunguza changamoto za usafiri wa umma katika barabara hiyo, lakini kuondoa bajaji hizo barabarani ambazo kwa sasa zimeonekana kuwa nyingi.

Kondo alisema tangazo la kuziita daladala hizo lilitolewa Oktoba 13 na tayari mwitikio umekuwa mkubwa licha ya kutotaja idadi ya daladala mpaka sasa ambazo tayari wamezisajili.

Katika tangazo hilo ilitaja moja ya vigezo vya mmiliki wa daladala kusajiliwa ruti hiyo, ni pamoja na  kuwa na gari yenye usajili kuanzia namba ECA, dereva wa gari kuthibitishwa na Latra.

Kigezo kingine ni leseni atakayopewa itakuwa ya muda wa mwaka mmoja na kuhuisha inategemea hali ya huduma za usafiri katika barabara hiyo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi kuhusu hatua hiyo walisema ni nzuri, licha ya kuonyesha wasiwasi kuwa idadi hiyo ya mabasi ni machache, walau wangeingiza hata 30.

“Hii barabara inahudumia watu wengi kwa usafiri wa umma na ndio maana unaona hata  bajaji zimekuwa nyingi lakini bado zinapata wateja, nadhani wangeongeza kutoka daladala 15 na kuwa 30,”amesema Bisura Rahim mkazi wa Mbezi.

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa  jina la Casian Filbert amesema, anatamani  wasajili na zingine zinazotoka Mbezi kwenda Kariakoo na Mbezi kwenda Posta, kwa kuwa hao ndio wanateswa na usafiri wa mwendokasi ambao umeshindwa kutimiza haja ya usafiri kama ilivyokusudiwa wakati mradi huo umeanzishwa.

Mwendesha bajaji, Isaya Lyimo amesema pamoja na kusajiliwa kwa daladala hizo, wana imani bado watapata abiria kwa kuwa usafiri wao ni wa kukodi na watu wanaupenda kwa kuwa mtu akishapanda ni mpaka afike safari yake.