Wamiliki daladala wapendekeza nauli iongezeke

Dar es Salaam. Wakati wamiliki wa mabasi ya mkoani wakipendekeza nauli ya usafiri huo kuongezeka kwa Sh10,000, wale wa daladala wametaka ipande kutoka Sh500 kuwa Sh800 na mwanafunzi iwe Sh300.

Maoni hayo yalitolewa jana jijini Dar es Salaam na wamiliki hao katika mkutano wa wadau wa sekta ya usafirishaji nchini kupokea maoni kuhusu marejeo ya nauli za mabasi ya mikoani na daladala, uliofanyika.

Katibu wa Wamiliki wa Mabasi ya mkoani, Priscus Joseph alisema katika mapendekezo yao kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji, mafuta kupanda kila mwezi na kuadimika kwa dola walau kila abiria anayesafiri nauli anayopaswa kulipa iongezwe Sh10,000.

“Kwa mfano nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga ni Sh20,000 kwa basi la semi-luxury, hivyo ikiongezwa Sh10,000 iwe Sh30,000, huku kwa ruti ya Dar es Salam –Mwanza ambayo kwa basi la aina hiyo ni Sh65,000  sasa iende kuwa Sh75,000,” amesema Joseph.

Kwa upande wa daladala, Mwenyekiti wa Wamiliki ya Daladala mkoa wa Dar es Salam, Sabri Mabruk alisema umbali wa kilometa kumi ambayo kwa sasa watu wanalipa Sh500 iwe Sh800, wakati kilometa 15 iwe Sh1,200 badala ya Sh550 ya sasa na ile ya kilometa 20 ambayo sasa watu hulipa Sh1,600 badala ya Sh600.

Wakitoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya bei hizo, ukusanyaji maoni ya kupandisha nauli hizo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latraa CCC), Daud Daud alisema wanakubaliana kwamba gahrama za uendeshaji zimeongezeka zikichangiwa na mafuta na mabadiliko ya dola.

Kutokana na hali hiyo, alisema wakati Latra inaenda kufanya ongezeko la nauli hilo, iangalie isije kwenda kumuumiza mtumiaji wa mwisho na kutoa mapendekezo matatu ili kukabiliana na hali hiyo.

Daudi aliyataja mapendekeo hayo kutumia magari ya gesi, kununua vifaa yakiwemo matairi yanayodumu kwa muda mrefu na kufanya mchakato wa kuiomba Serikali kupunguza kodi pale wanapoingiza mabasi kwa ajili ya huduma za wananchi.

“Pia  kuna haja ya kuiomba Serikali kwa hatua za dharura kupunguza gharama za maisha kwa kuweka ruzuku, kwani kuongezeka kwa nauli kutaathiri usafirishaji wa bidhaa ndogo na kubwa ikiwemo mchele, sukari, kiberiti na bidhaa nyinginezo muhimu,” amesema Daud.

Jingine alisema ni kutumia vipuri ambavyo ni sahihi, kwani wengi wameonyesha kutumia matairi ambayo yanatumika kwa kilometa 40,000 na kutakiwa kubadilisha tena, ila ukienda kwenye matairi ya viwango ambayo gharama yake pia ipo juu, yataweza kuwapa kilometa nyingi zaidi  na hivyo kupunguza gharama za uendeshaj.

Kwa upande wao wananchi akiwemo Omar Sagafu amesema busara na hekima vinatakiwa kutumika katika kwenda kufanya uamuzi wa upandishwaji nauli.

“Hapa ni kwamba hata Serikali kama inaweza kutoa ruzuku katika mafuta kama ilivyofanya kipindi cha nyuma ifanye hivyo ili pia wananchi wa chini ambao wengi ndio wanaotumia usafiri wa umma, wapate afueni,” amesema Sagafu.

Shaban Hussein, mkazi wa Kariakoo, amesema hakubaliani na kupanda kwa nauli hizo ukizingatia tayari gharama za maisha na bidhaa kwa sasa zipo juu.

“Wamiliki wa mabasi katika hili wasiangalie tu upande wao, bali waangalie pia na upande wa wananchi na hali walizonazo ambao ndio hao wanapata kipato kutumia wao,” amesema Shabani.

Malina Yasin anaona familia zinavyooenda kubeba mzigo huo wa kupandishwa kwa nauli na kutolea mfano walio na wanafunzi watatu mpaka wanne, ina maana kama anapanda magari mawili itabidi kila mmoja apewe Sh1,200  kila siku na mzazi kujikuta Sh5,000 inaishia yote kwa wanafunzi hapo bado yeye ya kwenda kusaka riziki.

“Nadhani Serikali iliangalie hili kwa jicho la karibu, kwa kuwa maisha yeyewe tunayoishi kwa sasa ni adhabu tosha, wakiongeza nauli tena wanataka tukimbilie wapi na sisi Tanzania ndio nchi yetu,” amesema Melina.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema katika mapendekezo waliyoyapokea kutoka kwa wasafirishaji wa mabasi ya mikoani ni ya magari ya basi Semi-luxury (daraja la kati), ambayo nauli yake ni Sh56 kwa kila kilometa huku yale ya Luxury huwa wanaacha bei ya soko iamue.

Katika mapendekezo yao alisema ABC alipendekeza daraja hilo la kati nauli iwe  na nyongea kutoka Sh56.88 hadi Sh92.8 kwa kilometa, wakati Happy Nation ikipendekeza kutoka Sh56.88 hadi Sh84.6 kwa kilometa na Super Feo ikitaka iwe Sh45 kwa kilometa.

‘Kwa hiyo kwa ujumla mapendekezo yao yapo kuanzia asilimia 47.8 mpaka asililimia 79.1,” amesema.

Hata hivyo, Suluo alisema kwa daladala hawakupeleka maoni yoyote kutoka kwa wamiliki, isipokuwa sheria inawaruhusu Latra kuitisha maoni pale wanapoona inabidi kwa wakati husika na kwa sasa wamefanya hivyo kutokana na ongezeko la bei ya mafuta.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyekuwepo wakati wote wa kikao hicho aliwapongeza wamiliki kutumia njia ya demokrsaia katika kulijadili hilo kuliko kutumia migomo ambayo amesema haina tija kwa nchi katika kufikia masuluhisho. 

“Basi ukilinunua unanunua kwa pesa zako, lakini tayari ukishalisajili, umeshaingia kwenye ubia na Serikali, wala huwezi kuendesha  gari lako na kusema ulipindue kwa makusudi ila tunaamini  gari likipata ajali linapata kwa  bahati mbaya na wala sio kwa matakwa ya mwenye gari wala dereva,” amesema Chalamila.