Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo yajitenga na mpango wa kuwa chama kikuu cha upinzani

Muktasari:

  • Licha ya minong'ono kuwa mbio za ACT Wazalendo zinalenga kupigania kuwa chama kikuu cha upinzani, chenyewe kimelikana hilo, kikisema hakijawahi kuwa na shabaha hiyo.

Busega. Chama cha ACT Wazalendo, kimeweka wazi msimamo wake kuwa, harakati na mikakati kinayoifanya hailengi kupambania nafasi ya kuwa chama kikuu cha upinzani nchini, bali kiu yake ni kushinda uchaguzi na hatimaye kishike dola.

Kauli ya chama hicho, inajibu mitazamo ya wadau mbalimbali na baadhi ya wanasiasa wanaosema, hatua ya chama hicho kukubali kushiriki uchaguzi, kinalenga kuwa chama kikuu cha upinzani.

Ukiacha mitazamo ya wadau hata vyombo mbalimbali vya habari, vimewahi kutabiri kuwa, huenda chama hicho kikawa mfalme mbele ya vyama vya upinzani nchini.

Hayo yanaendelea katika wakati ambao, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekuwa kikijinasibu kuwa ndio chama kikuu cha upinzani Tanzania.

Hayo yameelezwa leo, Ijumaa Julai 4, 2025 na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alipozungumza na viongozi na makada wa chama hicho wa Jimbo la Busega katika mkutano wa ndani, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya Operesheni Majimaji Linda Kura.

Katika kuijenga hoja yake hiyo, kiongozi huyo anasema wakati wadau mbalimbali wakidhani chama hicho kinalenga kuwa chama kikuu cha upinzani, hiyo si shabaha yao.

Badala yake, amesema dhamira ya ACT Wazalendo ni kushinda uchaguzi na hatimaye kushika dola ili kuwaongoza Watanzania kwa misingi ya haki, uwazi na uwajibikaji.

"Tunasikia watu wanasemasema huko mitandaoni eti tunataka kuwa chama Kikuu cha upinzani, sio lengo letu kuwa na nafasi hiyo, malengo yetu ni kushika dola," amesema.

Kwa sababu malengo yao ni kushika dola, Dorothy amesema tayari wanatambua ili kulifikia lengo hilo, kunahitajika umakini, ujasiri na kujua nini wanachokitaka yote hayo wanayo.

"Tumeamua kushiriki uchaguzi na kushinda. Tumejipanga kisayansi kuhakikisha tunashindwa. Yale mambo ya unaingia kwenye uchaguzi hujui udhaifu wa mpinzani wako mwaka huu hayatakuwepo," amesisitiza.

Ameambatanisha kauli yake hiyo na msisitizo wa umuhimu wa kushiriki uchaguzi, akisema ndiyo msingi wa kupatikana kwa viongozi, kujenga thamani ya kura na kuwapigania wananchi na masilahi yao.

"Tukiamua kuitafuta haki yetu, hakuna anayeweza kutushinda. Hakuna anayeweza kuizidi nguvu ya umma kwenye haki. Tunataka kuhakikisha atakayepata kura nyingi kwenye uchaguzi anatangazwa na hilo linatimia," amesema.

Dorothy ambaye pia ni mtia nia ya nafasi ya urais kupitia chama hicho, amesema mageuzi yote duniani, huja kwa mapambano na chama hicho kinaamini katika ushindi ni sayansi.

Amesema kunahitajika ukakamavu na ujasiri katika mapambano ya kufikia hayo, kwani vijana watapokea vitisho vingi.

Kwa upande wa waziri kivuli wa katiba na sheria wa chama hicho, Peter Madeleka amepingana na msimamo wa Chadema wa kususia uchaguzi, akisema hakuna aliyewahi kufanikiwa kwa mwenendo huo.

Ametolea mfano nyakati zote ambazo vyama vya upinzani vilithubutu kususia uchaguzi, Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichukua nafasi zote na kutumia fursa hiyo kujiimarisha zaidi kwenye dola.

"Hakuna mtu yeyote duniani aliyefanikiwa kuzuia uchaguzi. Hatuwezi kukimbia uchaguzi kwa sababu Serikali iliyopo madarakani imemaliza muda wake, tukashindane tuishinde tushike dola," ameeleza.