Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Daladala Arusha wasitisha mgomo, wengine wasusa

Guta zikiendelea kubeba abiria katika stendi ya Kilombero jijini Arusha leo Jumanne Agosti 15, 2023 katika mgomo wa daladala kubeba abiria wakishinikiza kuondolewa kwa bajaji katika maeneo ya mjini. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Mgomo huo ulioanza jana Agosti 14, 2023 ilihusisha madereva wote wa jiji la Arusha na Arumeru kushinikiza kuondolewa kwa bajaji zinazopita katika njia zao, kwani zinawanyima abiria.

Arusha. Wakati uongozi wa madereva wa Daladala jijini Arusha na Wilaya ya Arumeru ukitangaza kusitisha mgomo waliouanza jana Agost 14, 2023, baadhi ya madereva wamegoma kurejesha magari wakisema ni usaliti.

Mgomo huo wa jana ni wa tatu mwaka huu, ambapo madereva hao wamekuwa wakilalamikia uwepo wa pikipiki za matairi matatu maarufu kama bajaji katika njia wanazopita, wakisema zinawanyima abiria.

Jana madereva hao walimlalalamikia Mkuu wa mkoa huo, John Mongela wakisema ameshindwa kutekeleza makubaliano yao yaliyotokana na mgomo wa Julai 3, wakitaka Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati.

Hata hivyo, akizungumza jana na Mwananchi, RC Mongela alisema ameshatuma timu yake kushughulikia mgogoro huo.

Akizungumza leo asubuhi Agost 15, Katibu wa mwenezi wa madereva daladala Mkoa wa Arusha, Mussa Njuga amesema jana Agosti 14 Mkuu wa Mkoa, John Mongela aliwaita usiku kikao pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama, ambapo wamekubliana kurudisha huduma, huku Jeshi la Polisi likipewa jukumu la kusaka bajaji zinazofanya kazi kinyume na utaratibu.

"Tumeamua kusitisha mgomo baada ya kuitwa na Mkuu wa Mkoa na Kamati Ulinzi na Usalama, ambapo wamekubaliana kukamata bajai zote zilizoko nje ya mfumo wa kisheria ikiwemo kutokuwa na lesseni na zile zilizoko kisheria zirudishwe kwenye vituo vyao wasubiri kukodiwa," amesema.

Amesema kabla ya mgomo huo walimwandikia walimwandikia barua Mkuu wa Mkoa kumkumbusha utekelezaji wa tamko lake na kumweleza bado mwingiliano kati yao na bajaji ni mkubwa.

Hata hivyo, kauli hiyo ya kiongozi huyo wa daladala imeibua sintofahamu baada ya baadhi ya madereva kugoma kurudisha magari yao barabarani.

Mmoja wa madereva Cherlea Swai amesema ruti anayofanyia kazi ya Sombetini – Ngureso, bado kuna bajaji nyingi zinaendelea na kazi, hivyo haoni sababu ya kurudisha gari kwa hali hiyo.

"Hawa viongozi wetu wanatusaliti maana tulikubaliana kuwa hadi bajaji ziondolewe kwenye kazi yetu ndio turudi, sasa nashangaa bila hata utekelezaji wameanza kurudisha huduma wakati hizi ahadi tulishapewa migomo miwili iliyopita na utekelezaji hakuna," amesema.

Awali Ofisa Mfawidhi wa Latra mkoa wa Arusha, Joseph Michael wakati akizungumza  na wasafirishaji wa daladala katika soko la Kilombero aliwataka kuendelea kutoa huduma wakati  serikali inaendelea kufanyia kazi swala lao na asiyetekeleza atafutiwa leseni .

"Rudisheni huduma wakati Serikali inafanyia kazi madai yenu na msipofanya hivyo tutafutia leseni wagomeaji na kupewa wengine ambao wameomba leseni muda mrefu ili wao waweze kufanya kazi ya kuhudumia abiria bila aidha yoyote," amesema Joseph.

Hawa Msangi abiria kutoka Kwa Mrombo alisema kuwa wamefurahia huduma ya usafiri kurudi huku akidai kuwa mgomo wa daladala ulilenga ubinafsi dhidi ya wenzao wa bajaji

"Kugoma kwa sababu ya wenzako kufanya kazi sioni kama ni sawa kwa sababu usafirishaji ni biashara huria na anaechagua kupanda ni abiria hivyo Serikali iangalie upya juu ya swala hili bila kuonea yoyote," amesema.