DC afurahishwa marekebisho ya vivuko Kigamboni

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sarah Msafiri akikagua vifaa vya uokozi wakati wa ziara ya kuangalia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Septemba 26 kwa wakala wa ufundi na umeme (Tamesa)

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri amesema ameridhishwa na mabadiliko aliyoyakuta kwenye usafiri wa vivuko vya feri baada ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) kutatua changamoto zilizokuwapo

Dar es Salaam. Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya  Kigamboni ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Sarah Msafiri imeridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) baada ya kutekeleza maagizo yaliotolewa Septemba 26, 2018  wakati ziara kwenywe vivuko vya feri.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 10, 2018 wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji amesema amejiridhisha na mabadiliko makubwa aliyoyakuta kwenye eneo la kusubiria abiria lakini hata ndani ya vivuko amekuta mabadiliko.

“Niliagiza kuwapo namba ya dharura ndani ya kivuko na eneo wanalokaa abiria,kuwapo kwa matangazo pamoja na ufungwaji wa runinga ndani ya vivuko na wanaposubiri abiria nimevikuta leo”amesem Sarah.

Amesema kilichobaki ni ufungwaji wa kamera ndani ya kivuko pamoja na kubadilisha runinga kwa kuwa zilizofungwa ni ndogo, hivyo ufungwaji wa runinga kubwa utasaidia kutoa elimu kwa abiria wanaosubiri.

“Nimefurahishwa na hatua mliofikia ili chombo kiwe salama na kuepuka kubeba wahalifu kamilisheni mchakato wa kamera ndani ya vivuko na kubadilisha runinga kwakuwa mlizofunga ni ndogo,”amesema.

Kaimu Mhandisi Mkuu wa Temesa, Japhet Maselle amesema baada ya kupata maelekezo kutoka kwa kamati ya ulinzi na usalama walianza kuyatekeleza ikiwamo ufungwaji wa runinga pamoja na kuandaa utaratibu wa vyombo vya moto kuingia ndani ya kivuko.

“Baada ya ziara ile tulianza utekelezaji mara moja ambapo hadi sasa kwa asilimia kubwa tumeshayatekeleza,tumebakiza ufungwaji wa kamera ndani ya kivuko mchakato unaendelea,”amesema Mhandisi Massele.

Amesema wao kama Temesa watahakikisha yale ambayo hayajatekelezwa wanahakikisha wanayafanyia kazi ikiwamo na changamoto nyingine zitakazojitokeza.

Septemba 26, 2018 kamati ya ulinzi na usalama ilifanya ziara kwenye vivuko vya feri ikiongozwa na mwenyekiti na kutoridhishwa namna vivuko hivyo vinavyotoa huduma hasa cha MV Magogoni kinachobeba watu 2000 na magari 60.

Amesema vifaa vya uokozi vipo lakini hakuna matangazo wala elimu inayotolewa ya namna ya kuvitumia vitendea kazi hivyo pindi linapotokea tatizo.