DC ataka wafanyabiashara wajipange kabla hawajapangwa

DC ataka wafanyabiashara wajipange kabla hawajapangwa

Muktasari:

  •  Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amewataka wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga kuanza kujipanga katika maeneo yaliyotengwa kabla kamati aliyounda kuanza kazi hiyo.



Mwanza. Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amewataka wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga kuanza kujipanga katika maeneo yaliyotengwa kabla kamati aliyounda kuanza kazi hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza katika ziara yake yenye lengo la kutoa elimu kwa wamachinga kuhusu utaratibu utakaotumika kuwapanga kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Makilagi ametaja malengo matatu ya kuwapanga wafanyabiashara hao kuwa ni pamoja na kuongeza ukisanyaji wa mapato kutoka kwa machinga na wafanyabiashara wanaomiliki maduka ndani ya jiji hilo kulingana na ukubwa wa biashara wanazofanya.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni kuimarisha usalama wa wafanyabiashara na wateja wao pindi wanapofika katika masoko yaliyopo ndani ya jiji hilo kununua bidhaa na huduma mbalimbali.

"Ili kuwa machinga lazima uwe na vigezo ikiwemo biashara yako kuwa na mtaji usiyozidi milioni nne, sasa kama unajijua mtaji wako unazidi kiasi hicho cha fedha naomba ujiongeze mapema ukajipange katika maeneo tutakayowatajia kesho Septemba 23 mwaka huu," amesema Makilagi.

Amesema sababu nyingine ya kuwapanga upya wafanyabiashara ni kuimarisha usafi wa mazingira ndani ya jiji hilo.

Ametolea mfano machinga waliopanga bidhaa zao na wanaouza vyakula katika mabanda yaliyojengwa juu ya mitaro na maeneo ya waenda kwa miguu, akisema wanachangia katika uchafuzi wa mazingira.

"Unakuta kuna mama lishe wameweka vibanda kila sehemu na wanalisha watu vyakula katika mazingira yasiyo salama. Tunahitaji tuwe na utaratibu unaoweza kumsaidia mteja kutambua akihitaji nguo atazipata wapi, hivyo hivyo kwa chakula, mboga mboga, na bidhaa nyingine," amesema

Pia amesema kamati aliyoiunda inayojumuisha viongozi wa wafanyabiashara hao imeshapendekeza maeneo 45 ya kutumika na wafanyabiashara hao, huku akiahidi kwamba shughuli ya kuwapanga haitakuwa na upendeleo.

"Tutatumia mfumo wa bahati nasibu kwa kuandika karatasi maalumu zenye namba ya eneo na kila mtu atachukua kikaratasi chake. Utakapopangwa ndiyo sehemu yako," amesema.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wamachinga (Shiuma) mkoa wa Mwanza, Said Tembo amewataka wafanyabiashara hao kuwa watulivu katika kipindi ambacho serikali inatafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.

"Niwaombe mtuamini viongozi wenu kwamba tutahakikisha maeneo ambayo tunapelekwa yana wateja wa kutosha na kuna uhakika wa biashara," amesema Mwita.

Naye mfanyabiashara katika mzunguko wa Nyerere, Bhoke Marwa ameonesha kutilia hofu utaratibu huo huku akidai kwamba unalenga kuwaondoa maeneo ya mjini ambapo kuna uhakika wa kupata wateja wa bidhaa zao.