DC Chunya ataka wasimamizi mapato kumulikwa

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka amewataka wataalamu wa mapato kuhakikisha wanakwenda maeneo ya ukusanyaji mapato na kujiridhisha kama wasimamizi wa mapato waliopo kwenye vituo wanakwenda sawa ili kuzuia upotevu wa mapato.

Chunya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka amewataka wataalamu wa mapato kuhakikisha wanakwenda maeneo ya ukusanyaji mapato na kujiridhisha kama wasimamizi wa mapato waliopo kwenye vituo wanakwenda sawa ili kuzuia upotevu wa mapato.

Sambamba na hilo, Mayeka amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya soko la madini ya dhahabu, akidai kuwa hivi karibuni wamekamata watu wakiwa wanatorosha dhahabu kilogram 400.

DC huyo ameyasema hayo wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwa wa Halmashauri ya Chunya, ambapo amesema kuwa dhahabu, mazao ya misitu au ya chakula, yanapotoroshwa, Serikali hukosa mapato na hivyo kufanya halmashauri kutofikia malengo iliyowekea.

"Serikali tayari iliweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa madini ya dhahabu kwa kujenga soko la kuuzia dhahabu, ambapo kila mchimbaji ana kwenda na kuuza madini yake, hapo wananchi watumie fursa hiyo...utakapo kamatwa unatorosha dhahabu sheria itafuata mkondo wake,” amesema na kuongeza;

“Mara kadhaa nimekutana na magari yaliyobeba mazao, nikijaribu kufuatilia naona kuna tofauti kubwa kati ya kile kilichopo kwenye gari na kile ya kilichopo kwenye risiti wahusika wa mapato hakikisheni mnafuatilia kwa makini kwa watu mliowaweka kwenye mageti ili kujiridhisha kama kuna uhalisia.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Noel Chiwanga, amewataka madiwani kuweka mikakati bora ili kudhibiti mianya ya utoroshaji mazao ya misitu na hivyo kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato.

Akitoa salama za chama hicho kwenye kikao cha baraza hilo amesema mazao ya misitu yamekuwa yakisafirishwa na kuuzwa nje ya wilaya Chunya hivyo kusababisha upotevu wa mapato.

"Kumekuwa na kundi la wanaobeba magunia ya mkaa kwa pikipiki na kusafirisha kwenda kuuza Mbeya Mjini, wanapata kwenye mageti bila shida yeyote, lakini mwananchi wa Chunya akiwa na debe moja la mkaa hunyanyaswa,” amesema na kuongeza kuwa;

“Hii haikubaliki lazima kama halmashauri iweke mikakati ambayo itasaidia kupunguza utoroshaji wa mazao ya misitu ikiwepo hao wanaobeba mkaa kwa pikipiki. Chunya ina rasilimali nyingi...tuna misitu ya asili, humo tunapata asali, dhahabu...wengine hawalipi ushuru, kama madiwani lazima muwe makini kufuatilia hilo.”