DC Kaliua aagiza mwalimu wa sekondari akamatwe

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua (DC), Paul Chacha akizungumza na madiwani na watendaji wa Wilaya ya Kaliua. Picha na Robert Kakwesi.

Muktasari:

  • DC Kaliua aamuru mwalimu wa Sekondari akamatwe kwa madai ya kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha pili na kisha kumuoa.

Tabora. Mkuu wa Wilaya ya Kaliua (DC), Paul Chacha ameagiza kukamatwa kwa mwalimu wa shule ya sekondari kwa tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha pili na Kisha kumuoa.

Akizungumza na madiwani na watendaji katika wilaya hiyo, Chacha amesema kuwa mwalimu huyo (jina linahifadhiwa) pia anatuhumiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita.

Chacha amesema kuna vitendo vya baadhi ya watu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi lakini mbaya zaidi ni pale walimu nao wanapojiingiza katika vitendo hivyo.

Ameagiza kukamatwa kwa mmwalimu huyo huku akilaani tabia ya watu kujihusisha na vitendo vya ngono na wanafunzi.

"Naagiza Mwalimu huyo akamatwe mara moja na mwanafunzi hata kama amejifungua mtoto, arudi shule kuendelea na masomo," amesema.

Mkuu huyo wa Wilaya amewataka watendaji wa Serikali wilayani humo kuwa wakali na kukemea vitendo hivyo visikithiri.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Japhael Lufungija amewataka viongozi na watendaji kutimiza wajibu wao katika kuwalinda watoto wa shule kupata ujauzito.

"Tushirikiane wote kwani hili sio Jambo la mkuu wa wilaya pekee bali ni letu wote," amesema.