Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Kongwa akerwa wanaoshangilia kifo cha Ndugai

Muktasari:

  • Wananchi wa Kongwa wawaombwa kuwa watulivu wakati huu wa msiba na kuwaomba wazazi wakemee vijana kwa kuwa hakuna uadui wa kushangilia mauti.

Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, Simon Mayeka amekemea baadhi ya vijana waliojitokeza kushangilia baada ya kutangazwa kwa taarifa za msiba wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 7, 2025, baada ya kufika nyumbani kwa Ndugai ulipo msiba, Mayeka amesema ni jambo linaloshangaza kwa sababu hiyo si mila wala desturi za Kitanzania.

Hivyo, amewaomba wananchi wa Kongwa kuwa watulivu wakati huu wa msiba na kuwaomba wazazi wakemee vijana kwa kuwa hakuna uadui mtu anapokuwa amekutwa na mauti.

Akizungumzia msiba wa Ndugai, Mayeka amesema umekuwa wa ghafla na umesababisha simanzi kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Amesema anakumbuka karibu wiki nzima Ndugai alikuwa kwenye shughuli zake za kisiasa za mchakato wa kura za maoni za CCM na alionekana akiwa na afya njema.

“Maisha ya binadamu yako mikononi mwa Mungu, kwa hiyo hatuwezi kuhoji sana,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Ameeleza jinsi mbunge huyo wa pili katika Jimbo la Kongwa ambaye ameongoza kwa miaka 25 na kusema yeye na wananchi wamepata simanzi kubwa.

"Ndugai amefanya mambo mengi ya maendeleo kwa wananchi wa Kongwa na alikuwa muumini mkubwa wa elimu kwa kuwa aliamini ni nyenzo muhimu ya kuwainua kuichumi na kwamba, katika kata 22, amesimamia ujenzi wa shule za sekondari 43," amesema Mayeka.

Wakati huohuo, Dickson Malayi aliyekuwa mfanyakazi katika makazi ya Ndugai amesema kifo cha mwanasiasa huyo kimekuwa cha ghafla kuliko walivyotarajia.

Dickson anakiri kuwa kwa muda mrefu sasa, hajamshuhudia Ndugai afya yake ikitetereka.

“Hakuonyesha unyonge na hata kwenye kampeni za kugombea ubunge kwa awamu ya sita, bado alikuwa imara na hata kampeni za juzi, hajawahi kusema anaumwa au kuonyesha unyonge, alikuwa mzima kabisa, sijui sasa,” amesema Dickson.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Mikalile ya Wanyausi, Clement Ndahani amemtaja Ndugai kuwa alama ya wazawa ambayo haitafutika na kwamba, wangetamani kuwa naye zaidi.

Ndahani amesema kifo cha mwanasiasa huyo kimewapa maumivu makali na pengo ambalo halitazibika daima ukizingatia alikuwa mtu anayependa kuhimiza elimu.


Miundombinu

Barabara inayoingia nyumbani kwa Ndugai imekwanguliwa na katapika na kumwagwa maji ili kupunguza vumbi.

Katika barabara hiyo ambayo inakona nyingi kabla ya kufika msiba ulipo, imemwagwa maji jirani na nyumbani huku maeneo mengine yakiwa yamesafishwa.


Viongozi

Magari ya viongozi yanaendelea kuingia nyumbani hapo yakiongozwa na wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma.

Wabunge waliomaliza muda wao pia wanaendelea kufika msibani hapa ni Dk Pius Chaya ambaye alikuwa Mbunge wa Manyoni Mashariki na Mbunge wa kuteuliwa, Dk Bashiru Kakurwa.