Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Liwale amtuhumu mwenyekiti wa kijiji kuuza ardhi, mwenyewe akana

New Content Item (3)

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kipelele kata ya Mirui wakiwa kwenye mkutano wa Mkuu wa wilaya ya Liwale Goodluck Mlinga alipotembelea kijijini hapo hivi karibuni .

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipelele, Abdulahman Mnoile amekanusha madai ya kuuza ardhi ya kijiji, akisema watuhumiwa ameshawaripoti kwa maandishi.

Mtwara. Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Goodluck Mlinga amemsimamisha kazi Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipelele, Abdulahman Mnoile na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumchunguza kwa madai ya kuuza ardhi ya kijiji kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Mnoile amekanusha madai hayo, akisema watuhumiwa wa uuzaji wa ardhi hiyo ameshawaripoti kwa maandishi.

“Wapo vijana wamejipa jukumu ambalo sio lao na tumewaonya mara kadhaa mpaka kwa maandishi… pia nimepeleka kwa mtendaji wa kata yetu ili kutupa msaada kuhusu hawa vijana.

“Mimi sihusiki na uuzwaji wa viwanja, lakini nimedhalilika kwa kufukuzwa mbele ya wananchi wangu. Nimeumia sana, hawakutaka hata kunisikiliza upande wangu,” amesema Mnoile.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu Desemba 4, 2023, mkuu huyo wa wilaya amesema mwenyekiti huyo na wenzake wamekuwa wakituhumiwa kuuza ardhi, hali iliyosababisha baadhi ya wanakijiji kukosa mashamba ya kulima katika msimu huu.

Amesema uuzwaji wa ardhi hiyo umeleta   malalamiko, kwani zaidi ya ekari 1,400 zinadaiwa kuuzwa kiholela, bila wenye mashamba kushirikishwa.

Aidha, ameongeza kuwa kisheria kijiji kinaruhusiwa kuuza ardhi ekari 50 kwa utaratibu wa kuleta maombi na kujadiliwa na mkutano wa kijiji.

“Sisi baada ya kupata taarifa za hao mawakala tuliwakamata, wakati Serikali ya kijiji ikafanya jitihada na kuwatorosha na hata baada ya kuwakamata wakawekewa dhamana polisi.

“Kwa hili tuona kama tunashindana nao, haiwezikani Serikali iweke vongozi kwa ajili ya kutatua kero za wananchi, badala yake wao ndio waongeze kero kwa wanachi wenzao,” amesema Mlinga.

Diwani wa Kibutuka, Faraji Said amesema ardhi kubwa imeuzwa kwa wafugaji kwenye maeneo ambayo si ya wafugaji, zaidi ya kaya 200 zimeingia na kuweka makazi.

“Kuna uvamizi wa msitu umekuwa mkubwa, hatuoni jitihada zozote za Serikali kutusaidia. Tunaishi kwa mashaka kwa kutishiwa haki yetu, lakini tunakosa msaada,” amesema Said.