DC Makilagi atii amri ya Mahakama, aibua jipya

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.

Mwanza. Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ametekeleza amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa kuwasilisha kiapo kinzani kujibu madai dhidi yake katika maombi madogo yaliyoko kwenye shauri namba 68/2023 la kugombania jengo la kanisa.

Kupitia kwa Wakili wa Serikali, Sabina Yongo, Makilagi, ambaye hata hivyo hakuwepo mahakamani ametekeleza amri hiyo iliyotolewa na Jaji Wilbert Chuma Januari 5, 2024, aliyempa siku tano kuwasilisha hati hiyo.

Katika shauri la msingi, mleta maombi, Benson Kitonka, Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God Gospel Church International (AGGCI) anaiomba Mahakama kuipa kanisa hili haki ya kumiliki jengo la Kanisa lililoko eneo la Bugando, jijini Mwanza ambalo kwa sasa linamilikiwa na Kanisa la Evangelical Assemblies of God in Tanzania (EAGT).

Kabla ya kujitenga na kuanzisha Kanisa jipya la AGGCI, mchungaji Kitonka na baadhi ya waumini wake walikuwa waumini wa Kanisa la EAGT na walikuwa wakifanya ibada zao katika jengo linalogombaniwa sasa.

Baada ya mgogoro na hatimaye wachungaji na baadhi ya waumini kujitenga kwa kuanzisha kanisa jipya, mali na fedha ziliamuliwa kubaki chini ya mamlaka na umiliki wa EAGT, uamuzi unaoungwa mkono na taasisi na ofisi za Serikali, ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, msimamo unaopingwa na upande wa Kanisa la AGGCI kupitia kwa mchungaji Kitonka kwa kufungua shauri mahakamani.

Mchungaji Kitonka, anayedai kuwa mmiliki halali wa jengo la kanisa linalogombaniwa anaiomba Mahakama kutoa amri ya kumruhusu yeye na waumini wake kuendelea kufanya ibada katika jengo hilo hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kuamuliwa.

Desemba 20, 2023, Mahakama Kuu kupitia kwa Jaji Stanlay Kamana ilitoa amri ya kuitaka Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kutengua uamuzi wa kuwazuia waumini wa Kanisa la AGGCI kutumia jengo hilo.

Kutokana na amri ya awali kutotekelezwa, waleta maombi kupitia kwa Wakili Gibson Ishengoma wamerejea mahakamani kuomba Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi atekeleze amri ya kutengua zuio dhidi ya waumini na viongozi wa Kanisa la AGGCI kutumia jengo la eneo la Bugando jijini Mwanza.

Hati kinzani yaibua mapya

Akizungumzia hati kinzani iliyowasilishwa na DC Makilagi, Wakili Ishengoma ameiambia Mahakama kuwa, maelezo yaliyoko kwenye hati hiyo iliyopokelewa saa 5:40 asubuhi ya Januari 9, 2024 imeibua hoja mpya, ikiwemo ya AGGCI kutosajiliwa kisheria, hivyo kukosa haki ya ama kufungua matawi au kuendesha shughuli za kiibada wilayani Nyamagana.

Huku akiomba muda wa siku mbili kupitia na kujibu hoja zilizoibuliwa kupitia hati kinzani ya Mkuu wa Wilaya, Wakili Ishengoma alidai Kanisa la AGGCI limesajiliwa kisheria kwa Sheria za Jumuiya sura namba 337.

Wakili huyo ameieleza Mahakama kuwa usajili huo umethibitishwa na Ofisi ya Msajili wa Jumuiya kupitia kwa barua yake ya Oktoba 27, 2023 kwenda Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana.

Wakili wa Serikali, Sabina Yongo anayemwakilisha Makilagi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hakupinga ombi la waleta maombi la kupewa muda wa kujibu hoja.