DC Malisa aagiza uchunguzi wa shule kudaiwa kupika chakula chenye wadudu

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa (katikati) akisikiliza kero za wananchi katika kata ya Isyesye Jijini Mbeya baada ya kuanza kutembelea kata kwa kata. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Jiji la Mbeya, Joyce Kaguo amesema watafuatilia suala hilo, huku akidai kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kuwapatia watoto hela badala ya kuchangia chakula shuleni.

Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ameagiza kuanza uchunguzi wa malalamiko ya wazazi wakidai wanafunzi wa Shule ya Sekondari Isyesye wanalishwa chakula chenye wadudu.

Hata hivyo, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Jiji la Mbeya, Joyce Kaguo amesema watafuatilia suala hilo, huku akidai kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kuwapatia watoto hela badala ya kuchangia chakula shuleni.

Malisa alitoa agizo hilo jana Mei 29 2024 kwa Mganga Mkuu wa Jiji, Yesaya Mwasubila baada ya kumsimamisha kujibu malalamiko hayo.

Hatua hiyo imekuja baada ya  mzazi Agness Daniel (45) kumweleza mkuu wa wilaya huyo kuwa watoto wao wanapitia changamoto ya kulishwa makande yenye wadudu na kusababisha waugue homa ya matumbo na kuhara.

"Mkuu wa wilaya tunashukuru kwa kuja kusikiliza kero zetu, kuna Shule ya Sekondari Isyesye hii ni ya Serikali, watoto wetu wanalishwa chakula aina ya kande zina wadudu,” amesema.

Hata hivyo, Agnes amesema anashanga kwa nini watoto walishwe chakula kibovu na cha aina moja wakati wanachangia Sh10,000 kila mwezi kwa ajili ya chakula cha mchana.

"Sio kwamba naongea kwa kubahatisha, mimi mwanangu anasoma hapo amesumbuliwa sana na tumbo nilipomwambia asimame kula chakula cha shule afya yake imeimarika,” amedai mzazi huyo.

Ameiomba Serikali iingilie kati huku akisema itafika wakati wazazi watagoma kuchangia fedha za chakula kwa kuwa afya za watoto wao ziko hatarini.

Aneth Jackson amesema kutokana na usalama mdogo wa uandaaji wa vyakula shuleni, Serikali isitishe michango ya chakula kwa wazazi na itafutwe njia mbadala itakayowezesha wanafunzi kupata chakula salama shuleni.

"Serikali ilikuja na mpango mzuri sana wa wazazi  tuchangie fedha ya chakula cha mchana na tukaridhia, lakini chakula chenyewe wanacholishwa hakina ubora,” amesema Jackson.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo Malisa ameutaka uongozi wa halmashauri kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini uhalisia na kuchukua hatua stahiki.

"Hizi ni tuhuma, kaimu mkurugenzi unda timu ianze uchunguzi mara moja, haiwezekani  Serikali inatoa maelekezo wazazi wanachangia fedha zao kwa moyo mmoja halafu yanakuja mambo ya ajabu kama haya,” amesema Malisa.

Pia, ameagiza viongozi wa kata na mitaa kuwa na utaratibu wa kuitisha mikutano ya wananchi kujadili masuala ya maendeleo na kubaini changamoto na kuzitatua badala ya kusubiri viongozi wa ngazi ya juu.

Mganga Mkuu wa Jiji, Dk Mwasubila amesema,"hili nitalifanya kwa kushtukiza maana kwa sasa watajipanga kupika chakula kizuri, Sera ya Elimu inaelekeza wanafunzi kula vyakula vya aina ya makundi matano."

Diwani wa Isyesye, Ibrahim Mwampwani amesema atafanya ziara kushtukiza ili kubaini uhalisia wa chakula shuleni hapo.