DC Masindi ahimiza wanawake kukuza uchumi wao
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Peter Masindi akizungumza kwenye uzinduzi wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda
Muktasari:
- Amewataka kutambua kuwa wao ni nyenzo muhimu katika familia zao, uzalishaji na malezi bora, hivyo wasijiingize kwenye mikopo isiyo ya lazima inayoweza kuwaletea migogoro na kuwanyima amani katika familia zao.
Kishapu. Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi amewataka wanawake kutumia Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kujijengea uchumi na kunufaika na fursa za maendeleo huku akisisitiza umuhimu wa kuepuka mikopo isiyo ya lazima na kutekelekeza shughuli za kiuchumi sambamba na majukumu ya kifamilia.
Hayo amebainisha leo Julai 17, 2026 katika hafla ya uzinduzi rasmi wa jukwaa hilo, iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kishapu iliyopo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga huku akiagiza kutengwa kwa eneo kwa ajili ya soko la wanawake kuwasaidia kufanya biashara zao.
“Mnapaswa kutambua kuwa ninyi ni nyenzo muhimu katika familia, uzalishaji na malezi bora, msijiingize kwenye mikopo isiyo ya lazima inayoweza kuwaletea migogoro na kuwanyima amani katika familia zenu. Pia, hakikisheni mnatumia fursa zinazopatikana kujiletea maendeleo endelevu bila kusahau majukumu ya kifamilia,” amesema Masindi.
Ameongeza kuwa: “Kuondoa changamoto ya ukosefu wa eneo la biashara, halmashauri inapaswa kutafuta eneo litakalotengwa kwa ajili ya soko la wanawake ili kuwawezesha kufanya biashara zao katika mazingira bora.”
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Katibu wa jukwaa hilo Wilaya ya Kishapu, Fredina Said kubainisha mafanikio yaliyofikiwa tangu kuanzishwa kwake huku ikieleza changamoto kubwa inayowakabili wanawake katika biashara zao.
“Mbali na mafanikio, changamoto iliyopo ni ukosefu wa eneo maalumu la soko kwa ajili ya wanawake wajasiriamali kuuza bidhaa zao, ambapo hii inachangia kushindwa kujikwamua kiuchumi,” amesema Fredina.
Katika picha ni wanawake wafanyabiashara kutoka wilayani Kishapu, wakiwa katika uzinduzi rasmi wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi wilayani Kishapu. Picha Hellen Mdinda
Naye, mbunge wa viti maalumu ambaye pia ni mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Shinyanga, Dk Regina Malima amewataka wanawake kuhakikisha wanamiliki ardhi, kuwekeza katika shughuli za ujasiriamali na kukuza biashara.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson ameeleza kuwa Serikali imeandaa bajeti na mipango ya kazi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za jukwaa hilo huku akiwataka wadau kuendelea kushirikiana katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Jukwaa hilo lilianzishwa rasmi mwaka 2022 na hadi sasa limefanikiwa kuunda majukwaa katika ngazi za vijiji, kata na wilaya pamoja na kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali, vikundi vya uzalishaji na kutafuta masoko ya bidhaa zao.
Katika juhudi za kuunga mkono jukwaa hilo, Masindi ameongoza harambee iliyofanikiwa kukusanya zaidi ya Sh4 milioni, fedha hizo zitasaidia kuimarisha mfuko wa jukwaa hilo katika Wilaya ya Kishapu.