DC Msando asitisha utalii vyanzo vya maji

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

Kusitisha kwa shughuli za utalii katika vyanzo vyote vya maji katika Mto Morogoro kunatokana na kujitokeza kwa matukio ya vifo vinavyotokana na kuzama maji. Pia kudondokewa mawe kwa sababu ya kutochukua tahadhari.

Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Morogoro (DC), Wakili Albert Msando amesitisha shughuli zote za utalii katika vyanzo vya maji katika Mto Morogoro baada ya mwanafunzi wa Chuo cha Liti kilichopo Wilaya ya Morogoro kufariki dunia kwa kuzama maji akiogelea na wenzake Mei 15 mwaka huu mkoani hapa.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini hapa, Wakili Msando amesema mwanafunzi huyo ametambuliwa kwa jina la John Benako (20) na alikumbwa na umauti akiwa na wenzake watatu wakiogelea ndani ya maji eneo la chanzo cha maji cha Mambogo mchana.
Wakili Msando amesema wanafunzi hao walienda kwa ajili ya kufanya utalii wakiwa saba na watatu kati yao waliingia kwenye maji na kuanza kuogelea lakini baada ya muda mchache mmoja wao alitoweka na juhudi za kumtafuta zilianza bila mafanikio wakitumika askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Mpaka sasa vifo vya watu watano vimetokea katika eneo hilo kwa kufariki na wengi wao ni wageni kwa sababu hawatambui eneo gani lina kina kirefu cha maji na salama hivyo namuagiza Mkurugenzi wa Bonde la Wami-Ruvu kusimamia agizo langu la marufuku ya wananchi wote kufanya utalii katika Mto Morogoro hasa maeneo ni hatarishi mpaka Kamati ya Ulinzi na Usalama itakapoweka utaratibu nzuri ili kuepusha matukio ya watu kufa maji,”amesema Wakili Msando.

Wakili Msando amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama itakaa na itakapojiridhisha wataweka utaratibu nzuri wa wananchi kufanya utalii ambapo kwa sasa wenyeviti wa serikali za vijiji, watendaji kata kujiunga kusimamia pia agizo hilo mpaka pale watakaporuhusu kufanyika shughuli za utalii kwa utaratibu nzuri.

Mkaguzi wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Emmanuel Ochieng amesema walipata taarifa saa 9:45 alasiri kwa kutoweka kwa wanafunzi aliyekuwa akiogelea na wenzake na baada ya kufika eneo la tukio walianza kusoma mazingira na kuanza kumtafuta.

Mkaguzi Ochieng amesema kwa siku ya kwanza hawakuweza kupata mtu hai wala mwili ambapo waliondoka saa 12 jioni ya jana na leo walianza kazi ya kutafuta mwili ambapo kati ya saa 3 hadi saa 4 asubuhi mwili wa kijana huyo waliuona na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi.

Mkurugenzi wa Bonde la Wami-Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi amesema wamesikitishwa na tukio lililotokea lakini wamepokea maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kusitisha shughuli za utalii kutokana na jamii kutumia vivutio vya utalii kufanya sherehe mbalimbali.

Mhandisi Mmasi amesema kumekuwa na watu kuzama katika maji, kudondokewa na maji katika maeneo yenye vivutio vya utalii.