DC Mtwara ataka utoro shuleni ukomeshwe

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya akionyesha miongozo inayokabidhiwa kwa maofisa elimu na wakuu wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Mtwara. Florence Sanawa

Muktasari:

Maofisa elimu kata na watendaji wa kata na vijiji katika Wilaya ya Mtwara, wametakiwa kufuatilia taarifa za wanafunzi watoro shuleni katika kata 56 ili kudhibiti utoro katika shule za msingi na sekondari.  

Mtwara. Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya amewataka maofisa elimu kata, watendaji na kuhakikisha kuwa wanafatilia taarifa za wanafunzi watoro kata zote 56 ili Kudhibiti utoro na mdondoko ambao uko asilimia 29-35 katika Wilaya hiyo.

Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 19 katika kikao cha kukabidhi miongozo ya elimu ngazi ya Wilaya ambacho kimehudhuliwa na Maafisa elimu kata, wakuu wa Shule za Msingi na sekondari ambapo amewataka kuhakikisha kuwa hatua stahiki zinachukuliwa Kudhibiti utoro mashuleni.

Alisema kuwa maafisa elimu kata wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa watoto wanahudhuria masomo bila kukosa.

"Hakikisheni mnafahamu watoto wangapi hawajafika shule wako wapi, wanafanya nini watoto ambao hawajaenda Shule wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria hakikisheni kata zote 56 Wilaya nzima mnafika na kuleta taarifa," amesema.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nambeleketela iliyoko Wilaya ya Mtwara Hawa Ndale alisema kuwa kwa sasa upo utoro wa rejareja.

“Tulifanya kampeni na Mkuu wa Mkoa hiyo imetusaidia sana kupunguza utoro kwa sasa ni kiasi kidogo hii inatokana na mwamko wa wazazi kupeleka watoto shuleni ni mdogo lakini tunajitahidi kuwaelimisha,” amesema Ndale.

Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Msingi Mlimani wilayani mtwara Hamis Seif alisema kuwa utoro umepungua na ufumbuzi umeshatatuliwa.


“Utoro umeshatafutiwa ufumbuzi na umepungua kwakuwa upo ufuatiliaji mkubwa kuanzia ngazi ya kijiiji halmashauri hivyo mdondoko umepungua.

“Tunafanyakazi kwa ushirikiano mkubwa hilo ndio limesababsiha utoro kupungua hata zile faini zimesaidia utoro kupungua,” amesema Seif.