DC Mwaipaya aanika vipaumbele vyake

DC Mwaipaya aanika vipaumbele vyake

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Abdallah Mwaipaya amesema moja  ya vipaumbele vyake ni  kusimamia mapato ya halmashauri hiyo kwa kushirikiana viongozi wa ngazi zote lengo likiwa ni kuleta maendeleo na kutatua kero za wananchi. 

Mwanga. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Abdallah Mwaipaya amesema moja  ya vipaumbele vyake ni  kusimamia mapato ya halmashauri hiyo kwa kushirikiana viongozi wa ngazi zote lengo likiwa ni kuleta maendeleo na kutatua kero za wananchi.

Mwaipaya amesema hayo leo Jumamosi Juni 26, 2021 katika kikao chake cha kwanza na wakuu wa idara na madiwani wa halmashauri ya Mwanga kwa lengo la kuweka msingi bora wa uwajibikaji kwa watendaji hao.

Moja ya vyanzo vya mapato katika halmashauri hiyo ni bwawa la nyumba ya Mungu ambalo likisimamiwa kwa ufanisi na kuwekwa mipango mikakati ya miradi thamani ya mapato itaonekana.

"Kikubwa zaidi kilichonileta hapa Mwanga ni kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ili wananchi wapate maendeleo na kuondokana na kero mbalimbali ikiwemo usimamizi wa mapato na matumizi kwa njia halali na rafiki kwa wananchi ili fedha zitatue kero za afya, elimu, maji na tatizo la wanyama wavamizi.”

“Moja ya kero kubwa iliyopo Mwanga ni hospitali ya Wilaya pamoja vituo vya  afya ikiwemo Kisangara kukosa jokofu,  jengo la kuhifadhia maiti. Ikitokea mtu amefariki dunia mnaanza kufikiria kumpeleka Himo au Moshi jambo hili ni tatizo, ,tutalifanyia kazi haraka ili wananchi wapate huduma hiyo hapahapa Mwanga,” amesema.

Amewataka watendaji wa halmashauri hiyo na viongozi mbalimbali kuanzia ofisi yake, ya mbunge, mwenyekiti wa halmashauri na madiwani kuwa na mahusiano mazuri kazini.