Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Siha: Toeni taarifa watumishi wanaochelewa kazini wachukuliwe hatua

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu  (katikati mwenye suti nyeusi) akiwasili kwenye mafunzo ya usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa wadau mbalimbali katika wilaya za Hai na Siha. Picha na Bahati Chume.

Muktasari:

  •  Mkuu huyo wa wilaya amesema  kuchelewa vituo vya kazi ni kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Siha. Mkuu wa wilaya ya Siha, Christopher Timbuka amewataka wananchi kutoa taarifa za watumishi wa umma wanaochelewa kufika kazini, ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao.

Timbuka ametoa wito huo leo Mei 15, 2024 wakati wa mafunzo ya usambazaji na uwasilishaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi  ya mwaka 2022 kwa viongozi, watendaji wa wilaya ya Hai na Siha yaliyofanyika Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.

Katika mafunzo hayo, baadhi ya viongozi wa dini walihoji kuhusu watumishi wa umma wanaochelewa kufika kazini, jambo linalokwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuchelewa vituo vya kazi ni kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

“Masuala ya kuchelewa kazini kwa watumishi wa umma, yasiletwe  kama malalamiko kwenye mikutano au vikao kama hivi, mnapoona toeni taarifa kwa viongozi yafanyiwe kazi,” amesema Timbuka.

Amesema kuchelewa kwao kazini kunakwamisha mambo mengi ya maendeleo kwa Serikali na hata kwa wananchi,  kwani mwananchi anawahi mapema ili apate huduma arudi kwenye majukumu yake, lakini anakaa muda mrefu, jambo ambalo amesema halitakiwi kufumbiwa macho.

Hata hivyo, amewashauri watumishi hao kuzingatia muda wa kazi ambao  unafahamika kuwa ni kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa amesema wamepokea ushauri wa viongozi wa dini, hata hivyo amewataka kusisitiza suala la uadilifu, hivyo wasiache kukemea.

“Siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili tunapokuja misikiti au kanisani, viongozi wa dini msiache tukaenda, mtuambie Biblia au Quran inasemaje kuhusu utumishi uliotukuka kwa uadilifu, kwenye suala la nidhamu na uwajibikaji,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurudin Babu amesema lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu  kutafsiri katika kupanga na kuelekeza kufuatilia na kuthamini utekelezaji wa sera na mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

“Semina hii inatuongezea ujuzi na kupata uzoefu wa namna bora ya kutumia matokeo ya sensa katika kutekeleza wajibu wetu wa matumizi sahihi ya matokeo hayo kwa mipango jumuishi ya maendeleo endelevu.”

Mshiriki wa mkutano huo ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Sau wilayani humo, Mdoe Yambazi amepongeza mafunzo hayo akisema yamempa uelewa wa kuendelea kuhakikisha wananchi wa Siha wanapiga hatua za maendeleo hadi vijijini.