DC Tanganyika aagiza mwenyekiti kitongoji akamatwe

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amemuagiza Ofisa Mtendaji wa kata ya Kasekese, Paschal Masobeji kumkamata Mwenyekiti wa kitongoji cha Kasekese A, Beata Mpandachombo ili arejeshe fedha alizowatoza wananchi  za kuwaandikia barua za uthibitisho kupata vyeti vya  kuzaliwa  vya watoto wao.

Katavi. Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amemuagiza Ofisa Mtendaji wa kata ya Kasekese, Paschal Masobeji kumkamata Mwenyekiti wa kitongoji cha Kasekese A, Beata Mpandachombo ili arejeshe fedha alizowatoza wananchi  za kuwaandikia barua za uthibitisho kupata vyeti vya  kuzaliwa  vya watoto wao.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo leo Ijumaa Novemba 26. 2021 wakati akizindua mpango wa usajili na kupata vyeti vya kuzaliwa watoto chini ya umri wa miaka mitano wilayani humo akidai kuwa alichokifanya mwanyekiti huyo wa kitongoji ni kinyume cha sheria.

“Nimepata taarifa kuna mwenyekiti wa kitongoji amewatoza fedha wananchi Sh2000 za kuwaandikia barua, kwahiyo fedha iliyochukuliwa lazima irudi jua halijazama,”amesema Buswelu.

 “Mtafute umkamate aje hapa umenielewa? asiporudisha hizo fedha Takukuru chukueni mkondo wenu, tunataka kufanya kazi kwa mujibu wa sheria siyo mtu kujiamulia,”

Amesema kiongozi yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo utakuwa mwisho wake wa kufanya kazi na kwamba barua  hizo zinatolewa bure na kusajili watoto kupata vyeti vya kuzaliwa  hakuna malipo.


Mbali na hilo ametoa onyo kali kwa watendaji wote Wilaya ya Tanganyika kutowapa majukumu wenyeviti wa vijiji au vitongoji kuwaandikia barua za utambulisho wananchi isipokuwa zinatakiwa kuandikwa na maofisa watendaji wa vijiji.

“Siyo majukumu yao, rai nyingine kwa viongozi wa vijiji tafuteni utaratibu wa kuziwezesha ofisi za vijiji ziwe na vitendea kazi ili wananchi wapewe huduma bure,”amesema Buswelu.

Mkazi wa kitongoji cha Kaskse A, Mipawa Joseph ambaye ni miongoni mwa waliotozwa fedha za kuandikiwa barua hizo amedai mwenyekiti huyo alimtoza Sh2000.

Ester Lumalisha amesema “Mimi nilienda kwa mwenyekiti akadai nitoe Sh3000 kuniandikia barua nilimpa kwasababu nilikuwa sifahamu, namshukru mkuu wa wilaya, hapa nasubiri kurudishiwa,”amesema ester.

Kwaupande wake Ofisa Mtendaji wa kata ya Kasekese, Paschal Masobeji amekiri kuwepo tatizo hilo akidai kuwa Novemba 24, 2021 alipata taarifa hizo kwa mratibu wa usajili kwamba wananchi wanalalamika kutozwa fedha.

“Baadhi ya wananchi walimueleza mwenyekiti anawatoza fedha kuwaandikia vitambulisho, baada ya kunishirikisha hili nilitafuta mgambo wakaenda kumkamata wakamleta ofisini,”

“Nilikusanya karatasi alizoandika nikapiga hesabu zikafika Sh34, 000 nilipomhoji alidai wananchi walisema wanamsaidia, nikamuamuru akazitoa, waliofika jana nimewarudishia zimeisha,”amesema Masobeji.

Ameongeza kuwa kwakuwa jana walifika wananchi wachache bado malalamiko hayo yanaendelea kutolewa, atamkamata ili arejeshe kutekeleza agizo la mkuu wa wilaya na kwamba dosari hiyo haitajitokeza tena.

Katika wilaya ya Tanganyika watoto chini ya umri wa miaka mitano watakaosajiliwa ni 48,000.