DC Ulanga atangaza ukomo wa maendeleo kijiji cha Epanko

Morogoro. Wananchi wa Kijiji cha Epanko kata ya Nawenge Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro wametakiwa kuacha kufanya shughuli zozote za maendeleo ili kupisha uchimbaji wa madini ya Kiywe maarufu Graphite utakaofanywa na mwekezaji kampuni ya Duma TanzGraphite Ltd.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Dk Julius Ningu alitangaza ukomo wa maendeleo ndani ya eneo la mradi wa utapofanyika uchimbaji huo na kutoa siku 60 za kufanyiwa uthamini wa ardhi, mali na makaburi kwa kila mwananchi anayehusika.

Dk Ningu alisema hayo jana katika kijiji cha Epanko wakati akizungumza na wananchi hao ambapo alieleza kuwa ametangaza ukomo huo kwa mamlaka aliyopewa na sheria ya uthamini 2016 na kanuni zake za 2018.

Mkataba kati ya Mwekezaji wa kampuni Duma TanzGraphite Ltd na Serikali ya Tanzania ulisainiwa Ikulu jijini Dodoma kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho huku Mkuu wa Wilaya ya Ulanga akihudhulia wakati wa utiaji saini mkataba huo.

Amewataka wananchi kijijini hapo hasa wale waliopitiwa na mradi huo kuacha kufarakana na badala yake washirikiane kwa pamoja wakati wa zoezi la utathmini wa ardhi, mali, na makaburi mpaka litakapokamilika.

“Tafadhali toa ushirikiano wako kwa wataalamu watakaohusika na zoezi hili utathmini kumbuka utathmini wa ardhi utatusaidia kujenga mustakabali kwa wilaya yetu, kuvutia wawekezaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesema mkuu huyo wa wilaya ya Ulanga

Dk Ningu ametoa wito kwa wananchi kijijini hapo kuwa wavumilivu wakati wa zoezi hilo kutokana na mchakato huo ambao unaweza kuchukua muda lakini ni muhimu kufanywa kwa umakini ili kupata matokeo sahihi.

Amesema Watu watapokea fedha, wasifike kwenye mafarakano kwa sababu ya zoezi la linaloenda kufanyika, akataka vikosi kazi kufanya kazi kwa uwazi na kutoachwa mtu yoyote kumuhusisha kwenye zoezi.

Amesema utathmini utafanyika kwa uwazi na ushirikishwaji wa wananchi wote kwa kufuata utafiti wa viwango kulingna na soko la sasa na bei iliyopendekezwa na kuidhinishwa na ofisi mthamini mkuu wa serikali ni sh laki tano kwa hekari moja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Duma Tanzgraphite Ltd Christer Mhingo amesema ameahidi kushirikiana na wananchi na kwamba uwekezaji unaowekwa kwenye eneo hilo na kampuni hiyo utakuwa wenye manufaa ya Tanzania katika kuleta maendeleo sekta ya madini nchini.

“Nimefurahishwa na namna mlivyotupokea, naimani tumeanza vyema naahidi kushirikiana nayi kwa uaminifu kama kampuni hatutawaangusha,”amesema Mhingo

Mthamini mteule Mkoa wa Morogoro (Authorised Regional Valuer), Adelfonce Mtima amesema kwa mujibu wa sheria za ardhi msimamizi mkuu wa ardhi ya Tanzania ni Rais wa Tanzania kutoka na sheria zinazomuongoza, hivyo baada ya mwaka 1999 mwananchi ana haki ya kulipwa fidia kwa mali zake.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Property Matrix Babylon Mwakyambile, iliyopewa na serikai dhamana ya kuwafanyia wananchi utathmini amewaomba wananchi kuwepo kwenye maeneo yao pindi watakapopita kutathmini ili kuweza kupata taarifa sahihi ya eneo na mali za mtu husika.

Mwakyambile amesema kampuni itakuwa na dodoso za aina mbili ambazo ni zile za sheria ya kitaifa(Tanzania) pamoja na zile za kimataifa, ingawa mwekezaji ameeleza kulipa fidia kwa wananchi kwa kutumia sheria ya kimataifa.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ipanko, Hilda Linuma amewahakikishia wananchi kuwa viongozi watasimamia kikamilifu zoezi zima na ameiomba kampuni kuhakikisha inatoa taarifa mapema pindi panapotokea mabadiliko.

Linuma amesema watahakikisha wanasimamia na kuunda kikosi kazi huru ambacho kitasimamia kwa karibu maslahi ya wananchi wa Ipanko.

Mwenyekiti huyo amesema kijiji cha Epanko kina jumla ya wakazi 2,546, wanaume wakiwa 1,215 na wanawake 1,331 huku kaya zikiwa 646 na vitongoji sita (6) ambavyo ni Luli, Itatira, Mbera, Kazimoto, Epanko B na Epanko A.