DCEA yanasa bangi ‘skanka’ iliyosindikwa kilo 423 Dar

Muktasari:

  • Kiwango cha kikubwa cha bangi aina ya skanka kimekamatwa katika operesheni iliyowezesha kubaini kiwanda cha kuzalisha biskuti za bangi Kawe.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kiwanda cha kusindika biskuti zinazochanganywa na bangi kali aina ya skanka.

Sambamba na hatua hiyo, DCEA imewakamata watu 16 wanaotuhumiwa kuhusika na mtandao wa kutengeneza biskuti hizo na bidhaa nyingine zinazounganishwa na bangi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kufuatia hatua hiyo, DCEA imetoa tahadhari kwa wananchi ikiwataka kuwa makini na bidhaa mbalimbali za vyakula zinazopendwa na watoto ambazo zimekuwa zinachanganywa na skanka, yaani bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu.

Skanka inaelezwa kuwa na kiwango kikubwa cha sumu cha zaidi ya asilimia 45 ikilinganishwa na ya kawaida yenye sumu asilimia kati ya 3 hadi 10.

Vyakula vinavyochanganywa na skanka na vinapendelewa kutumiwa na watoto mbali na biskuti, ni keki, jamu, sharubati na tomato sauce.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema mbali na bidhaa hizo za vyakula ambazo zinawalenga zaidi watoto, skanka pia imekuwa ikichanganywa kwenye sigara na shisha.

Hayo yamebainika wakati kukiwa na ongezeko la watu wenye matatizo ya afya ya akili, wengi wao wakiwa ni vijana na watoto wenye umri kuanzia miaka 15 na matumizi ya bangi yakitajwa kuwa moja ya sababu.

Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, mchanganyiko wa bangi na vyakula hivyo, unafanyika kwa lengo la kurahisisha uuzwaji wa dawa hizo kwa kificho na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya kupitia watoto.

Alisema baada ya kazi kubwa ya kudhibiti uingiaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini, wafanyabiashara wa dawa hizo wameendelea kubuni njia mpya, ikiwemo kuzichanganya kwenye vyakula na bidhaa nyingine ili kutengeneza kizazi kipya cha watumiaji.

Katika operesheni zake kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi, Mamlaka hiyo ilibaini eneo lenye kiwanda bubu cha kutengeneza biskuti hizo lililopo Kawe, Dar es Salaam na kuwakamata wahusika na kujihakikishia bidhaa hizo haziingii sokoni na kuathiri watoto na vijana wengi zaidi.

Novemba 18, 2022 gazeti la Mwananchi liliripoti kuhusu hofu ya kuwepo kwa biskuti zinazotengenezwa kwa kuchanganywa na bangi na baadhi ya wanafunzi wa vyuo jijini Dar es wakikiri kuzitumia.

“Katika eneo la Kawe tuliwakamata watuhumiwa wakiwa katika uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.

“Hawa tumeshawapeleka mahakamani na tunatoa wito kwa wananchi watupe taarifa za uwepo wa viwanda vya aina hii au watu wanaojihusisha na biashara hii ili kuhakikisha bidhaa hizi hazipatikani mtaani,” alisema Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema katika operesheni zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi, wamekamata kilo 423.54 za skanka, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi cha dawa hizo kuwahi kukamatwa nchini.

Alisema kati ya mzigo huo, kilo 158.54 zilikamatwa jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Kigamboni na Kawe zikiwa zimehifadhiwa kwenye mabegi na kilo 265 zilizosalia zilikamatwa katika matukio tofauti mikoa ya nyanda za juu kusini zikiwa zimefichwa ndani ya magari kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kwenda jijiji Dar es Salaam.

Tahadhari ya DCEA

Kamishna Lyimo alitoa wito kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo kuwa makini na vyakula wanavyovitumia na kuacha kufuata mikumbo isiyofaa, ikiwemo kutumia vilevi na vitu wasivyovijua, hali ambayo inaweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

“Hata wale vijana wanaotumia sigara na shisha unaweza kujikuta unasafiri umbali mrefu kufuata shisha kwa hisia kwamba ina ladha nzuri, kumbe inachanganywa na skanka na baada ya muda akili inavurugika kabisa,” alisema Kamishna Lyimo.

David Mollel, ambaye ni miongoni mwa vijana waliowahi kutumia dawa za kulevya, ikiwemo bangi, alisema operesheni za aina hiyo zinapaswa kuwa endelevu ili kuwanusuru watoto na vijana wengi kuangukia kwenye uraibu wa dawa hizo.

Madhara ya bangi

Akizungumzia madhara ya tatizo hilo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Wallace Karata alisema matumizi ya bangi hubadilisha utendaji kazi wa ubongo na kumfanya mtumiaji awe tofauti.

“Kuna magonjwa ya akili ambayo yamejificha, inawezekana mtoto kwenye familia yake kuna ugonjwa wa akili wa kurithi, sasa akitumia bangi anaenda kuyaamsha. Hiyo skanka madhara yake ni makubwa na yanatokea kwa haraka zaidi.

“Mtu anaweza kuona maruweruwe, kusikia sauti zinazomhamasisha kufanya chochote, kama ni mtoto anajiona mkubwa na mwenye nguvu na uwezekano wa akili ya mtumiaji kuchanganyikiwa ni mkubwa,” alisema Dk Karata.

Si hivyo tu, bangi inapotumiwa na mtoto au kijana inaathiri uwezo wake wa kufikiri na kuharibu mfumo wa kumbukumbu.

Dk Karata anaungna na Firmina Scarion, daktari mwenzake wa magonjwa ya akili, aliyesema bangi ikitumiwa kupita kiasi inaamsha mfumo wa ubongo na kusababisha kubadilika kwa tabia, kumbukumbu na kupelekea hisia za raha iliyopitiliza.

“Matatizo yanayowakuta sana vijana wa namna hii ni pamoja na kujihusisha kwenye vitendo vya kamari, wizi na vitendo vingine vya kujipatia pesa ili wapate fedha waendelee kununua na kutumia bangi. Wanaweza pia kupelekea magonjwa mengine ya akili kama kuwa na wasiwasi uliopitiliza,” alisema Dk Firmina.