Wananchi wachepusha maji Mto Mara kumwagilia bangi

Muktasari:
- Bangi yaendelea kuwa mfupa mgumu Tarime, Mto Mara ukigeuzwa kitovu cha kilimo na uchakataji wa zao hilo haramu. Maji yachepeshwa kumwagilia mashamba ya bangi.
Dar es Salaam. Operesheni maalumu iliyofanywa katika Bonde la Mto Mara imebaini bonde hilo linatumika kama kitovu cha kilimo na kuchakata zao la bangi kukiwa na viwanda vinavyochakata na kufungasha dawa hizo haramu kabla ya kusafirishwa sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Operesheni hiyo iliyofanyika kwa siku sita na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi licha kubaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi ilikuta pia viwanda vidogo viwili vinavyotumika kuchakata na kufungasha bangi kabla ya kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mbali na kilimo hicho ilibainika pia kuwa wakulima katika eneo hilo wamekuwa wakichepusha maji ya mto na kuyaelekeza kwenye mashamba yao kwa ajili ya kumwagilia zao hilo haramu.
Akizungumzia hilo Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo amesema operesheni hiyo imebaini kuwa wakazi wa eneo hilo wamelifanya Bonde la Mto Mara kama sehemu maalumu kwa ajili ya kilimo cha bangi na kutoruhusu mtu yeyote asiye mkazi kuingia kwenye bonde kama sehemu ya kuficha uhalifu wao.
‘‘Kitendo kinachofanywa na wananchi waliopo katika eneo la Mto Mara ni kinyume kabisa na sheria, viongozi wa serikali na wananchi ambao siyo wakazi wa hapa hawaruhusiwi kabisa kuingia eneo la bonde. Uwepo wa daraja lililopo katika mojawapo ya vijito vinavyopeleka maji Mto Mara, linatumika kama kizuizi cha watu kwenda kwenye hifadhi ya bonde la mto maeneo yanayolimwa bangi.
“Ili mtu avuke anatakiwa kujieleza nia na madhumuni ya kuvuka kuelekea upande wa pili na wahusika wasiporidhika na maelezo hawakuruhusu kuendelea na safari,’’ amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Amesema baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vijiji vinavyopakana na bonde hilo pamoja na wananchi waliojimilikisha bonde hilo muhimu kwa uchumi wa taifa, wamekuwa wakikodisha na kuuza mashamba ya kulima bangi ndani ya hifadhi ya bonde hilo.
Kamishna Jenerali Lyimo ameeleza kuwa Mto Mara ni muhimu katika ikolojia ya Mbuga ya Serengeti hivyo kuna kila sababu ya wizara zinazohusika kushirikiana na DCEA kutokomeza kilimo cha bangi katika eneo hilo.
‘‘Tukiacha kilimo cha bangi kiendelee hivi na kuwaacha wananchi waendelee kuchepusha maji ya mto kumwagilia bangi mwisho wa siku itaharibu ikolojia katika Mbuga ya Serengeti na mto kwa ujumla. Ni vyema tukashirikiana kuhakikisha eneo hili linasimamiwa vyema ili kufanikisha kusitishwa kwa kilimo cha bangi,” amesema Lyimo.
Diwani wa kata ya Tulwa Chacha Machugu ametaka viongozi wa serikali za mitaa wanaosaidia kuendelea kwa kilimo cha bangi wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa watu wengine.
‘‘Tutashirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha bangi hailimwi Tarime na yeyote atakayekiuka miongozo na sheria za nchi atawajibishwa kwani sote tunaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia niwaombe viongozi wa dini wasaidie kuwaambia waumini wao dawa za kulevya hazitakiwi,” amesema Machugu.
Baadhi ya wakazi wa Tarime walizungumzia opereshi hiyo wakieleza kuwa hali ya umaskini inawafanya vijana wengi kujikita kwenye zao hilo wakiamini itawapa fedha za haraka.
Magreth Ally amesema vijana wengi wanalima bangi kwa madai ya kupata fedha kwa haraka hivyo aliiomba Serikali kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kuelekeza na kuwezesha kilimo cha mazao mbadala ili kuepusha kurithishana kilimo cha bangi.
Naye Isaya Banda ameiomba Serikali kufanya operesheni endelevu katika maeneo yote ili kutokomeza bangi kwani vijana wengi wameathirika na matumizi ya dawa hizo. Pia, amewaomba wananchi kuwafichua wanaojihusisha na kilimo na biashara ya bangi.
Katika operesheni hiyo viwanda vidogo viwili vya kuchakata bangi na hekari 807 za mashamba ya bangi zimeteketezwa , gunia 507 za bangi kavu na gunia 50 za mbegu za bangi zimekamatwa sambamba na watuhumiwa 11.