Akamatwa na misokoto 897 ya bangi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi wilayani Simanjiro mkoani Manyara, linamshikilia Richard Dhahabu (61) mkazi wa Ngage wilayani Simanjiro kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi misokoto 897.

Simanjiro. Jeshi la Polisi wilayani Simanjiro mkoani Manyara, linamshikilia Richard Dhahabu (61) mkazi wa Ngage wilayani Simanjiro kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi misokoto 897.

Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Manyara, ACP George Katabazi amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa Septemba 16, 2023 Kijiji cha Ngage, Wilaya ya Simanjiro.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara tunaendelea na msako na operesheni mbalimbali za kukamata makosa na uhalifu ukiwemo dawa za kulevya bangi, mirungi na dawa za  viwandani," amesema ACP Katabazi

Amesema Septemba 16, 2023 usiku huko kijiji cha Ngage wilayani Simanjiro, alikamatwa Richard Dhahabu (61) akiwa na dawa za kulevya aina ya bangi misokoto 897 sawa na uzito wa nusu kilo.

"Mtuhumiwa amefikishwa kituo cha Polisi kwa taratibu zingine za kisheria kwa sababu alikuwa na bangi hiyo kinyume cha sharia," amesema ACP Katabazi.

Kamanda Katabazi ametoa vito kwa vijana ambao wengi wao ndiyo wanaoathirika na dawa hizo za kulevya kuacha kutumia kwani zinapoteza nguvu kazi ya Taifa huku nao wakati mwingine wakipoteza maisha kwa kujihusisha na ulevi huo.

"Vijana wengi ndio watumiaji wa kubwa wa dawa za kulevya na kuua nguvu kazi ya Taifa hivyo sasa hawana budi kuacha kwa kuwa madhara hayo ni makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla," amesema ACP Katabazi.

Pia ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara waachane na biashara ya dawa za kulevya  kwa sababu ni hatari kwa maisha yao na watoto wao akidai kuwa wataadhibiwa kwa kujihusisha na biashara hiyo haramu watakapo bainika," amesema.

"Jeshi la Polisi tunaendelea na msako…tutawakamata wale wote wanao jihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya na kuwafikisha mahakamani na sheria ifuate mkondo wake," amesisitiza ACP Katabazi.