Prime
Deni la Sh18,000 lageuka kesi ya mauaji, Mahakama yabadilisha shtaka
Muktasari:
- Urafiki wa karibu kati ya Ally Athumani na Aidan Daudi uliishia kwenye umwagaji damu baada ya mabishano ya deni la Sh18,000 la mauzo ya kadi ya kumbukumbu na paneli ndogo ya sola, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma, imemkuta Ally na hatia ya kumuua mwenzake (Aidan) bila kukusudia.
Arusha. Kilichoanza kama makubaliano ya kuuza bidhaa zenye thamani ya Sh18,000 kati ya marafiki wawili wa karibu, Ally Athumani na Aidan Daudi, kiliishia kwa mmoja kupoteza maisha baada ya mabishano kuhusu fedha kugeuka shambulio la kisu.
Hata hivyo, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma, imebaini kuwa ingawa Ally ndiye aliyesababisha kifo cha rafiki yake, upande wa mashtaka haukuthibitisha kuwapo kwa nia ya awali ya kuua.
Kutokana na hilo, mahakama ilibadili shtaka la mauaji na kumtia hatiani Ally kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Hukumu hiyo ilitolewa Juni 30, 2026, na Jaji Augustine Rwizile. Nakala ya hukumu iliyochapishwa katika tovuti ya Mahakama inaonesha Ally ametiwa hatiani kwa kosa hilo, lakini haijataja adhabu aliyopewa.
Kwa mujibu wa vifungu vya 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu, kosa la kuua bila kukusudia linaweza kuadhibiwa hadi kifungo cha maisha.
Awali, Ally alikuwa akikabiliwa na shtaka la mauaji, kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kumuua Aidan Daudi kinyume cha sheria Julai 19, 2024, katika eneo la Ujiji, Wilaya ya Kigoma.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, siku ya tukio Ally alimkabidhi Aidan kadi ya kumbukumbu (memory card) na paneli ndogo ya sola zenye thamani ya Sh18,000 ili aviuze kwa niaba yake, wakikubaliana kuwa fedha zingekabidhiwa baada ya bidhaa hizo kupata wanunuzi.
Baadaye usiku, Ally alifika nyumbani kwa Aidan na kumwita nje wakati marehemu alikuwa akila chakula cha jioni pamoja na mkewe, Hamisa Almas, na shemeji yake, Kitwana Almas.
Hamisa aliiambia Mahakama kuwa muda mfupi baada ya wawili hao kutoka nje, alisikia wakibishana kuhusu fedha za mauzo ya bidhaa hizo. Muda mfupi baadaye, alimsikia mumewe akipiga kelele akiomba msaada.
Alipotoka nje, anasema alikuta mumewe ameanguka chini akivuja damu nyingi, huku akimwona Ally akiondoka eneo la tukio akiwa ameshika kitu kilichoonekana kuwa kisu.
Majirani nao walipotoka kwenye nyumba zao, walimkuta Aidan akiwa amelala kwenye dimbwi la damu kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Maweni, ambako baadaye alifariki dunia.
Ripoti ya uchunguzi wa daktari ilionesha kuwa kifo kilisababishwa na kupoteza damu nyingi baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kukatika kwa mshipa mkubwa wa damu.
Mahakama ilielezwa kuwa baada ya kukamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Kigoma, Ally alitoa maelezo ya onyo yaliyokubaliwa kama ushahidi.
Katika maelezo hayo, alikiri kumkabidhi marehemu bidhaa hizo ili aziuze na kwamba alipofuatilia fedha zake, yalizuka mabishano yaliyomfanya amchome kisu kabla ya kukimbia na kwenda kukificha kisu hicho nyumbani kwake.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano, akiwamo mke wa marehemu, pamoja na vielelezo viwili, ambavyo ni ripoti ya uchunguzi wa maiti na maelezo ya onyo ya mshtakiwa.
Katika utetezi wake, Ally alikana kutenda kosa hilo. Alidai kuwa siku ya tukio alikuwa Kibirizi akiendelea na shughuli zake na akasisitiza kuwa hamfahamu marehemu. Pia, alidai ushahidi wa Hamisa haukuwa wa kuaminika kwa sababu alitoka nje baada ya tukio kutokea.
Mama yake Ally, aliyejitambulisha mahakamani hapo kwa jina la Hadija Sehelami, alitoa ushahidi wa kumtetea, akidai kuwa usiku huo mwanawe alikuwa nyumbani, polisi walipofika kumkamata na kwamba hakuwa na taarifa zozote zinazomhusisha na mauaji hayo.
Akitoa uamuzi, Jaji Rwizile alisema utetezi wa mshtakiwa ulikuwa na upungufu mkubwa kwa kuwa ushahidi ulionesha wazi kuwa alimfahamu marehemu na mke wake, jambo lililopingana na madai yake mwenyewe.
Jaji alisema ushahidi wa Hamisa uliaminika kwa sababu alimfahamu Ally kwa muda mrefu, kulikuwa na mwanga wa kutosha katika eneo la tukio na alimwona mshtakiwa kabla na baada ya shambulio.
Mahakama pia ilikubaliana na ushahidi wa kitabibu kuhusu chanzo cha kifo pamoja na maelezo ya onyo ya mshtakiwa, ikibaini kuwa yalitolewa kwa hiari na yalikuwa yanaendana na ushahidi mwingine uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa Jaji Rwizile, ushahidi huo ulithibitisha pasipo shaka kuwa Ally ndiye aliyemchoma kisu Aidan na kusababisha kifo chake.
Hata hivyo, mahakama ilipochambua iwapo kulikuwa na nia ya awali ya kuua, ilizingatia mazingira ya tukio, ikiwamo ukweli kwamba wawili hao walikuwa marafiki wa karibu, hawakuwa na mgogoro wa muda mrefu na mabishano yalizuka ghafla kuhusu fedha za mauzo ya bidhaa hizo.
Mahakama pia ilibaini kuwa marehemu alichomwa mara moja tu kwa kisu na hakuna ushahidi ulioonesha kuwa Ally alikuwa amepanga kumuua kabla ya tukio.
Kutokana na mazingira hayo, Jaji Rwizile alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa mshtakiwa alisababisha kifo cha marehemu, lakini haukufanikiwa kuthibitisha kiungo muhimu cha nia ya awali ya kufanya mauaji.
Kwa msingi huo, mahakama ilitumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 319(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kubadili shtaka la mauaji na kumtia hatiani Ally kwa kosa la kuua bila kukusudia, kinyume cha vifungu vya 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu.