Dereva wa aliyekuwa RAS K’manjaro azikwa, viongozi wa dini wakemea mauaji ya albino

Mwili wa dereva wa aliyekuwa Katibu tawala wa mkoa wa Kilimanjaro, Alphonce Edson(54) ukiingizwa kaburini, nyumbani kwake, Kahe, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjro. Picha na Omben Daniel
Muktasari:
- Mchungaji Thobias Msekwa wa KKKT amekemea vitendo vya kikatili, ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino, akisisitiza utajiri haupatikani kwa kuua, bali kwa kufanya kazi halali.
Moshi. Wakati dereva wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa kilimanjaro, Alphonce Edson (54) akizikwa katika makaburi ya familia, Mchungaji Thobias Msekwa ametumia nafasi hiyo kukemea vitendo vya kikatili katika jamii, ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino na kuitaka Serikali kutowafumbia macho wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Mchungaji huyo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Lowiri, Dayosisi ya Kaskazini, amesema hakuna utajiri unaopatikana kwenye viungo vya binadamu na badala yake watu wafanye kazi zinazowaingizia kipato kwa njia halali bila kukatisha uhai wa maisha ya wengine.
Ameyasema hayo leo Jumatatu, Juni 24, 2024, wakati wa ibada ya maziko ya dereva huyo yaliyofanyika katika makaburi ya familia nyumbani kwake, Kahe, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Edson na Katibu Tawala huyo (RAS), Tixon Nzunda aliyezikwa Juni 22, 2024 mkoani Songwe, walifariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Juni 18, saa 8:30 mchana, eneo la Njia panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.
Akihubri katika ibada hiyo, Mchungaji Msekwa amesema dunia ya leo watu wameweka imani kuwa, wakiwa na viungo vya binadamu watapata utajiri, jambo ambalo wamedanganywa.
“Diniani leo ukatili umezidi ndani ya jamii zetu, wengine wamediriki kuamini kwamba wanapokuwa wamepata viungo vya binadamu wanakwenda kuwa matajiri, juzi tumesikia habari ya yule mtoto mwenye ualbino Kagera (Asimwe) amefanyiwa ukatili mbaya sana na baba yake akihusishwa, wakidai wanahitaji utajiri, ndugu zangu tunadanganywa, utajiri hauwezi kuja kama haufanyi kazi.”
Ameongeza kuwa; “Utajiri unakuja kwa mtu kufanya kazi kwa bidii na si katika hali ya kutafuta watu na kuua, hapana. Ninaona Serikali yetu inapiga kelele katika hilo na naomba mkuu wa mkoa, Mungu akusaidie kupambana nalo mkoani kwetu na hata nje ya mkoa wetu."
Amesema mauaji kwa watu wenye ualbino yamekuwa tishio na kuwafanya kuishi kwa wasiwasi bila kujua hatima yao ya kesho.
"Jambo hili limekuwa tishio kwa hawa ndugu zetu wenye ualbino, hawajui kama kesho kutakucha, wanawindwa kama wanyama, huruma haipo, tunaenda mbingu ipi?” amehoji.
Aidha, mchungaji huyo ameonya wananchi kuacha kuishi maisha ya kiburi na kunyanyua mabega na badala yake wote kuishi maisha ya upendo na unyenyekevu wakitambua maisha ya hapa duniani ni mafupi.
"Leo watu wengi wanaishi kwa kiburi, kimabavu, wanatembea wamepandisha mabega utadhani wanapaa, kama dunia hii ni yao, hata akionywa kwa jambo fulani hasikii, ndugu zangu wapendwa, dunia hii ya leo tunapaswa kuishi katika hali ya unyenyekevu na tukimuomba Mungu atusaidie tukijua muda wowote tunaweza kuondoka duniani hapa,” amesema mchungaji huo.
Akisoma historia ya marehemu, mtoto wa marehemu, Aswile Alphonce amesema wamepoteza kiungo muhimu katika familia na kuishukuru Serikali kwa jinsi ilivyobeba msiba huo.
"Tumeumia kwa kumpoteza baba ambaye alikuwa kiungo muhimu kwa familia, lakini tunaishukuru Serikali chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na mkuu wa wilaya hiyo kwa jinsi ilivyotukimbilia tangu tukio la msiba lilipotokea, tunajua familia tumepoteza na ninyi mmepoteza mtumishi, hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea kwa Mungu."
Marehemu Alphonce ameacha mke, watoto sita na wajukuu wanne.
Mapema asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu aliongoza mamia ya waombolezaji kwenye mazishi ya Edson.
Alisema mkoa kuondokewa na katibu tawala na dereva wake ni pigo kubwa kwao na pengo lao halitaweza kufutika kwa urahisi.
Babu amesema Alphonce alikuwa kijana mtulivu mchapakazi na hakuwa mtu wa manung'uniko wakati wa utendaji kazi wake.
"Alphonce alikuwa kijana mtulivu sana na sijapata kusikia amegombana na mtu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa tangu nimeripoti pale, hakuwa mtu wa manung'uniko, hukujua saa ngapi amekasirika au wakati gani ana furaha iliyopitiliza, alikuwa ni mtu wa ajabu sana, mimi pia aliwahi kuniendesha na mkimalizana nae hata saa saba usiku, hakuwahi kulalamika," amesema mkuu huyo wa mkoa.
Babu amesema kifo ni fumbo na kila mmoja anapaswa kutambua kuw dunia kila mmoja anapita, hivyo hakuna haja ya kuonyeshana ubabe ili siku ikifika, waachane kwa wema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema kila mmoja ataondoka saa yake ikifika na kusema kila mmoja anapaswa kufanya kazi kwa bidii ili siku ikifika aweze kukumbukwa.
"Siku na saa itakapofika na sisi tutalala kama Alphonce lakini lipo jambo la kujifunza siku tukilala tutafanyiwa nini,tujifunze kuwa wavumilivu na kufanya kazi kwa bidii ili ikifika ile siku ambayo hatupo, wale wanaobaki wapate ya kusema juu yako," amesema.
Akitoa salamu za pole, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye ameitia moyo familia ya dereva huyo kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa kuwa kila kinachotokea hapa duniani ni kusudi la Mungu.
"Nitoe pole kwa familia kwa kuondokewa na baba, mume, babu lakini nitoe pole kwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kwa kuondokewa na watumishi wako hawa, lakini kwa jamii nzima," amesema.
Akiwatia moyo familia, DC Sumaye amesema duniani hakuna linalotokea ambalo Mwenyezi Mungu hajaliruhusu hivyo akaitaka familia kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwao.
Amesema Alphonce, alitimiza kusudi la Mungu hapa duniani hivyo lililotokea ni mpango wake kila mmoja ataondoka kwa wakati wake.
Naye, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa madereva Tanzania, Venus Wanyangi amesema taarifa za kifo cha dereva mwenzao haikuwa rahisi kuzipokea kwa kuwa muda mchache walikuwa naye katika majukumu yao ya kazi na kwamba ni pigo kwa tasnia yao.
"Siku ya ajali tuliachana naye kama dakika 20, ndio tukaambiwa kwamba ndugu yetu akiwa na bosi wake wamepata ajali mbaya na wamefariki, haikuwa rahisi sana kuikubali ile hali lakini ilibidi tuikubali kwasababu ni kazi ya Mungu."
"Chama kinatoa pole sana kwa familia, kwa mama na watoto wa marehemu, tuko pamoja na ninyi katika changamoto hii, tumpe pole Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuondokewa na watu wawili muhimu kwa wakati mmoja katika ofisi yake," amesema Wanyangi.