Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Digital Iris yarahisisha uchunguzi wa saratani Hospitali ya Mawenzi

Kifaa maalumu cha ‘Digital Iris’ kinachotumika kubaini dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Huduma hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya pamoja na kubaini mapema dalili za saratani ya mlango wa kizazi kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.

Moshi. Badala ya kulazimika kusubiri kwa siku nzima au zaidi ili kubaini viashiria vya mwanzo vya saratani ya mlango wa kizazi, hatimaye ugonjwa huo utabainika ndani ya dakika moja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.

Hatua hiyo, inatokana na kuanza kutumika kwa kifaa maalumu kinachoitwa Digital Iris, chenye uwezo wa kutibu na kubaini dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi ndani ya dakika moja.

Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya wiki ya wauguzi duniani iliyofanyika mjini Moshi leo, Mei 12, 2026, Muuguzi kutoka Kitengo cha Mama na Mtoto wa hospitali hiyo, Irene Mrema amesema kifaa hicho kinatumia huduma ya mgandisho (cryotherapy), jambo linalorahisisha uchunguzi na matibabu ya wagonjwa wenye changamoto hiyo bila maumivu.

“Tumekuwa tukitumia kifaa hiki kutibu saratani ya awali ya mlango wa kizazi. Kina uwezo wa kuonyesha kama mtu ana dalili za awali kwa kumchorea mduara sehemu yenye changamoto, hivyo kutusaidia kubaini haraka kama anahitaji tiba au huduma nyingine,” amesema.

Amesema kifaa hicho pia kimerahisisha utoaji wa huduma za mgandisho kwa kuwa kinatumika kwa urahisi na kina uwezo wa kuwahudumia watu watano au zaidi kwa muda mfupi.

Muuguzi wa kitengo cha saratani hospitalini hapo, Rehema Mbwambo amesema ugonjwa huo unaweza kutibika endapo utagundulika mapema.

Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, Rehema Mbwambo, akionyesha kifaa maalumu cha ‘Digital Iris’ kinachotumika kubaini dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi. Picha na Janeth Joseph

“Kifaa hiki hakiumizi, tumeanza kukitumia na matokeo yake ni makubwa kutokana na watu ambao tumewahudumia. Tukimkuta mama ana tatizo tunatoa  tiba ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi,” amesema.

Amesema huduma hiyo inawafaa zaidi wanawake wenye umri wa miaka 25 hadi 65 na ufanisi wa kifaa hicho umesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

“Hospitali yetu imeboreshwa na ina vifaa vingi ya kisasa. Tukimkuta mama ana shida hatumtumi tena kwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC badala yake tunatumia kifaa hiki kutoa tiba maalumu,” amesema.

Mmoja wa wananchi aliyefika kufanyiwa uchaguzi hospitalini hapo, Halima Juma amesema huduma hiyo ni nzuri na inatumia muda mchache.

“Nimekuja hapa Mawenzi leo kufanya uchunguzi wa mlango wa kizazi, huduma ni nzuri na haichukui muda mrefu hapa ninasubiri majibu,” amesema.